• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku moja kwenye ukumbi wa mazoezi

    (GMT+08:00) 2011-07-17 19:01:46

    Ni saa 3 asubuhi siku ya Jumamosi. Zhou Yi'nan anapanda subway kuelekea ukumbi wa mazoezi na kuanza siku yake ya kazi. Anafanya kazi kutoka Jumatatu hadi Jumamosi.

    Zhou amevaa koti jeusi, miwani myeusi, kofia nyeusi na ana tabasamu kubwa. Ingawa ana umri wa zaidi ya miaka 30, lakini anaonekana kama ana umri usiozidi miaka 25. ..

    Inamchukua takriban muda wa saa moja kufika kwenye ukumbi wa mazoezi, ambao ni sehemu yake ya pili kufanya kazi tangu alipoanza kufundisha mazoezi ya kujenga mwili miaka sita iliyopita jijini Beijing. Alisoma kozi ya masoko kwenye chuo kikuu, na ilimchukua miaka mingi kutambua kuwa kazi anayotaka kufanya zaidi ni kufundisha mtu jinsi ya kujenga mwili.

    "Mwanzoni kabisa nilifanya mazoezi ya viungo ili niwe na nguvu. Wakati ule, kila mmoja alidhani kuwa naonekana kama msichana kutokana na umbo dogo nililokuwa nalo. Hicho ni kitu pekee nilichopendelea. Baada ya kuhitimu chuo kikuu, nikawa mfanyabiashara lakini biashara haikuendelea vizuri. Kwa kuwa sikuacha kufanya mazoezi kwenye ukumbi wa mazoezi, na kupata tuzo kadhaa kwenye mashindano ya kujenga mwili. Nikaona naweza kupata kazi kwenye ukumbi wa mazoezi, wazo ambalo limekuwa zuri sana"

    Zhou anavaa nguo za kufanyia mazoezi na kuanza mazoezi ya kupasha moto mwili. Zhou anasema ana mteja mmoja kutoka Marekani anayemfuata kila Jumamosi saa 5 asubuhi. Anapotoka ofisini, anakuta mwanafunzi wake anamsubiri.

    Hili ni darasa la pili la msichana huyo mmarekani. Zhou anamshauri afanyiwe tena upimaji wa kina kuhusu mwili wake ili kuangalia kama kuna mabadiliko yoyote.

    Upimaji unaonesha kuwa msichana huyo anapaswa kupunguza uzito wa kilo tano ili kuwa na hali nzuri zaidi, na mafuta ndani ya mwili wake yamezidi kiwango kinachotakiwa, hali ambayo inamaanisha kuwa anahitaji kufanya mazoezi ya nguvu zaidi.

    Wakati wakielekea sehemu ya kufanyia mazoezi, msichana huyo anaonesha kujiamini kuwa anaweza kukamilisha hatua zote, hata hivyo baada ya muda, inaonekana kuwa msichana huyo anataka kuacha.

    (sauti darasani)

    "mara ngapi nimefanya?"

    "bado unahitaji kufanya mara tano zaidi."

    "siamini ni uso wangu ninauangalia, unatisha!."

    Muda unakwenda. saa moja baadaye na baada ya kunywa chupa mbili za maji ya kunywa, msichana huyo anaondoka kwenye ukumbi wa mazoezi akiridhika na mazoezi ya leo. Zhou anasema kazi ya kuwa mwalimu wa mazoezi ya kujenga viungo inamchosha kidogo, lakini bahati nzuri watu wa aina mbalimbali anaowafundisha wanaifanya iwe na furaha.

    "watu wengi wanaona kuwa mwalimu wa mazoezi ya kujenga mwili anapaswa kuwa na mbinu nzuri za kiufundi, lakini naona mbinu ya mawasiliano ni muhimu zaidi. Siyo kila mtu anaweza kufahamu sana mazoezi ya kujenga mwili. Wanawake wanakuja kwa ajili ya kupunguza uzito na wanaume wanataka kujenga misuli. Lengo letu ni kuwasaidia kutimiza malengo yao kwa kuzingatia afya na ufanisi. Tunahitaji kuwaambia njia sahihi na kuondoa mawazo potofu waliyonayo kuhusu kufanya mazoezi. Si vizuri kuwa mwembamba sana au na nguvu sana. Kila mmoja anahitaji uwiano kwenye mwili wake. Tunawasaidia kufanya vizuri zaidi."

    Ni saa 7 mchana. Wakati wa kula chakula cha mchana umefika. Zhou anasema huwa anakula chakula chepesi. Kwa kifungua kinywa, anakunywa kikombe cha mtindi. Kama akiona njaa kidogo kabla ya chakula cha mchana, anaweza kunywa maziwa au kunywa uji wa nafaka (cereals). Katika chakula cha mchana, huwa anakula saladi, nyama ya ng'ombe na mayai mawili. Wakati wa adhuhuri anakula matunda. Anasema baadhi ya wakati anakula siyo kutokana na kuona njaa bali kwa sababu wakati wa chakula umefika.

    "Sasa sina hamu kubwa ya chakula. Baadhi ya wakati naona wakati wa kula chakula umefika, hivyo ninakula. Mara chache sana nakula vyakula visivyosaidia afya kama vile chakula cha haraka na vya kubanikwa. Kama nikila vyakula hivyo, naweza kusafisha mwili wangu katika siku mbili zifuatazo. Nimekuwa na tabia hiyo kwa zaidi ya miaka kumi, sasa nimezoea."

    Baada ya chakula chepesi, Zhou anarudi kwenye ukumbi wa mazoezi. Sasa anawaongoza walimu wengine watatu. Kila siku wakati wa mchana, wanafanya mkutano kwa ajili ya kupitia mipango yao ya siku nzima.

    Kwa kawaida, Zhou ana miadi na mtu mmoja au wawili kwa siku. Katika muda wa ziada, anafanya mazoezi ya kujenga mwili mwenyewe. Zhou ana utaratibu wake binafsi wa mazoezi. Wakati akijenga misuli yake kutoka kichwa hadi kidole cha mguu, tabasamu kubwa haiondoki usoni mwake.

    Zhou anasema anahitaji kuongeza uwezo wake katika mambo mbalimbali. Anataka kusoma vitabu vingi zaidi kuhusu lishe na anatarajia kushiriki kwenye shindano jingine la kujenga mwili. Anatarajia kuwa iko siku atakuwa na ukumbi wake wa mazoezi. Lakini sasa anafurahi kuboresha mbinu zake, na kuwafundisha wengine kufanya hivyo.

    Siku yake Zhou Yi'nan imeisha, mwalimu wa mazoezi ya viungo jijini Beijing.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako