• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tarishi Liu Chengjiang

    (GMT+08:00) 2011-07-17 19:05:56

    Ni saa moja na nusu asubuhi katika majira ya baridi, hali ya joto ni nyuzi sifuri sentigredi.

    Liu Chengjiang, tarishi mwenye umri wa miaka 30 na kitu hivi, anafika kazini kwa pikipiki, na anavaa kofia ya chuma, glovu na kitambaa cha ngozi cha kuhifadhi joto kwenye miguu, wafanyakazi wenzake wamefika vilevile wakiwa wamevaa sare. Matarishi hao wanakusanyika hapa kila asubuhi kwa ajili ya kuchukua vifurushi watakavyosambaza. ..

    Liu anafanya kazi kwenye kampuni maarufu ya usafirishaji wa vifurushi ya China, ambayo ina matarishi wapatao 200, ambao wanapeleka vifurushi vyenye bidhaa zinazonunuliwa kwenye maduka yanayouza bidhaa zake kwenye mtandao wa internet. Kila tarishi anawajibika kupeleka vifurushi kwenye eneo la kilomita kadhaa. Leo asubuhi, Liu ana vifurushi zaidi ya 30, na anapaswa kuvipeleka kabla ya adhuhuri, kisha arudi kuchukua vingine.

    "Kwanza, nachagua vifurushi vya eneo langu, kisha navifunga kwa utaratibu maalumu. Njia za kupeleka vifurushi hivyo zimepangwa makusudi ili kuhakikisha vinafikishwa haraka iwezekanavyo. Siwezi kupoteza muda".

    Ni saa mbili. Liu anaweka vifurushi kwenye kiti cha nyuma cha pikipiki na kuwasha injini. Kituo cha kwanza ni jengo la ofisi lililopo umbali wa kilomita 2 kutoka hapa.

    Liu anagonga mlango, lakini hakuna mtu anayejibu. Inaonekana kuwa mpokeaji wa kifurushi bado hajafika ofisini.

    Mwanamke mmoja aliyepo ofisi jirani anasema atasaini na kupokea kifurushi hicho kwa niaba yake, lakini Liu anakataa. Anampigia simu mteja wake ili aweze kuthibitisha mtu anayeweza kumsaidia kupokea. Lakini mtu anayetambuliwa pia hayupo ofisini, hivyo Liu anapaswa kukipeleka tena baadaye.

    "katika hali kama hiyo, ninapaswa kwanza kuomba ruhusa kutoka kwa mteja wangu. Mtu anayetambuliwa na mteja tu ndiye anaweza kusaini na kuchukua kifurushi."

    Liu anasema inamlazimu arudi tena, hata hivyo ni lazima ahakikishe kuwa kifurushi kinapelekwa salama kwa mteja bila matatizo.

    Kituo kinachofuata ni jengo la ofisi ambapo matarishi hawaruhusiwa kuingia. Liu anampigia simu mteja na kumwambia aende chini kupokea kifurushi. Anapaswa kusubiri kwa dakika tano katika baridi.

    Kwa kuwa Liu anaonekana mara kwa mara kwenye eneo hilo, hivyo wateja wake wengi wanamfahamu, baadhi yao wanamuelewa vizuri hivyo huona hakuna haja ya kukagua vitu vilivyopo ndani ya vifurushi, lakini Liu kila mara anawashauri kukagua vifurushi vyao mbele yake.

    Kwengineko Liu anakoelekea ni kwenye eneo la makazi kupeleka vifurushi zaidi. Anaendesha pikipiki kwa haraka ili kuokoa muda, hii inamfanya aone baridi zaidi kutokana na upepo unaovuma. Hadi kufikia saa nne asubuhi, tayari alikuwa ameshapeleka vifurushi vingi. Anaweza kupata Yuan 3 sawa na senti 50 za kimarekani kwa kila kifurushi anachopeleka.

    "Natoa Yuan elfu tano kwa ajili ya matumizi ya familia yangu kila mwezi, yakiwemo matumizi ya kila siku na malipo ya mkopo. Mwaka jana niliweka akiba ya Yuan elfu 60.si mbaya."

    Liu anapata wastani wa Yuan laki 1.2 kwa mwaka, kiasi ambacho ni mara tatu zaidi kuliko mshahara wanaopata wale wenye kazi nzuri.

    Inasemakana kuwa hapa Beijing, kuna mamia ya kampuni za usambazaji wa vifurushi za aina mbalimbali, na makumi ya maelfu ya matarishi. Baadhi ya matarishi wanasambaza vifurushi kwa pikipiki au baiskeli za betri, na wengine wanaendesha baiskeli za kawaida, wanaweza kupata fedha nyingi zaidi kuliko Liu Chengjiang.

    "ukilinganisha na mimi, wanapaswa kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kila siku. Wanafanya kazi kutoka asubuhi hadi saa tatu au nne usiku. inachosha sana na kwangu mimi inapoteza sana muda."

    Liu alihamia Beijing miaka 12 iliyopita akitokea mkoa wa Hubei, katikati ya China, sasa ana mtoto mwenye umri wa miaka 9. kabla ya hapo alikuwa ni muuzaji bidhaa, ana uzoefu mkubwa wa kuwasiliana na watu wa aina mbalimbali. Kazi yake ya sasa amekuwa akiifanya kwa mwaka mmoja na hivi karibuni amenunua nyumba mpya kwenye kitongoji cha Beijing.

    "tunakula kwa haraka kadiri tuwezavyo"

    Liu anaendelea na kazi zake mchana na kutoka kazini saa 10 au 11 jioni, kisha anarudi nyumbani kumsadia mwanawe masomo yake.

    Mke wa Liu ana duka kwenye soko kubwa jijini Bejing. Liu anasema ikilinganishwa na wafanyakazi wengine waliohamia hapa, anaona ana bahati na kujivunia kuishi pamoja na jamaa zake kwenye mji mkuu. Anapamba nyumba yake mpya na kupanga kuwashawishi wazazi wake wahamie hapa pia."

    "sitarajii kufanya kazi hii kwa muda mrefu. Sasa nafanya kazi hiyo kwa sababu nalazimika kuweka pesa za akiba. Katika miaka kadhaa ijayo, natarajia kumsadia mke wangu kupanua duka lake kwa kutumia akiba yangu. Hii ni ndoto yangu kubwa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako