• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku moja katika maisha ya mwongoza bendi ya okestra wa Tibet

    (GMT+08:00) 2011-07-17 19:52:47

    Ni saa 3:30 asubuhi, katika ukumbi ambao kundi la waimbaji na wacheza dansi katika mkoa unaojiendesha wa Tibet hufanya mazoezi, mwanamume mmoja anazungumza na baadhi ya wanamuziki kwa lugha ya kitibet. Jamaa huyo mnyenyekuvu na mpole ndiye Bw Bianba. Yeye na wasanii wenzake wako kwenye pilikapilika za kuandaa maonyesho yaliyokuwa yafanyike kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai. Walikuwa wataonesha simfoni iitwayo "Chun Gu Fei Yang", ambapo ngoma za jadi za kitibet zitachukua nafasi muhimu. ..

    Bw Bianba alitunga muziki simfoni mwenyewe. Kwenye muziki wake, anatumia ala za muziki za jadi za kitibet kama vile tongqin yenye urefu wa mita 4 na ngoma za aina mbalimbali zilizotumika kwenye matambiko ya kidini na bendi ya kifalme.

    "Ala hizo za muziki haziuzwi kwa bei kubwa. Nyingi kati yake tumeazima kutoka kasri la Potala, kila moja ina historia ya zaidi ya miaka 1,000."

    Bw Bianba anatunga muziki wake kutokana na kuvutiwa na muziki katika hekalu la kibudha mkoani Tibet, ambapo alirekodi masomo ya watawa wa kiume, hivyo kuyatumia kama ni sauti ya marejeo kwenye muziki wake. Alichanganya sauti hizo kwa kutumia ngoma za aina tofauti za kitibet na ala za muziki za kupuliza kwa ajili ya kutunga aina pekee ya kitibet.

    "Muziki wa jadi wa kitibet unazingatia uimbaji sambamba na uchezaji dansi. Tofauti na muziki wa magharibi, muziki wetu huwa una sauti kubwa na unatumia nguvu. Lakini nimetumia teknolojia ya utungaji muziki ya kimagharibi kueleza muziki wetu wa jadi ili uwafikie watu wengi zaidi."

    Wasanii wote kwenye bendi hiyo ni Watibet ambao wamepata mafunzo rasmi ya muziki nje ya Tibet. Lakini bendi hiyo haifanyi maonesho mengi ya kibiashara kutokana na kuwepo kwa soko dogo huko Tibet. Ushuru unaotozwa katika barabara kuu ni mkubwa kama kuna safari ya kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya maonyesho. Kimsingi, bendi hiyo inafadhiliwa na serikali.

    Mazoezi yanamalizika saa tano asubuhi. Bw Bianba anaridhika sana na matokeo ambapo kila msanii kwenye bendi hiyo anatoa ushirikiano mzuri na kuelewa muziki wake.

    Mchana Bw Bianba hana pilikapilika nyingi, kwa hiyo anatumia muda wa mchana kutunga muziki au kuwafundisha wengine muziki.

    Mchana huu, anakwenda kwenye ofisi ya idara ya utamaduni ya Tibet kukutana na mtunzi wa nyimbo wa huko. Watu hao wawili watashirikiana kutunga kibwagizo kwa ajili ya kuadhimisha miaka 60 ya ukombozi wa Changdu.

    "Changdu ni sehemu ya kwanza iliyokombolewa mkoani Tibet mwaka 1950. Maonesho ya muziki yatafanyika kuadhimisha ukombozi wake. Kibwagizo hicho kinachotungwa nasi kitaimbwa mwishoni mwa maonesho."

    Baada ya majadiliano ya muda mfupi, Bw Bianba anaamua aina ya muziki ya kibwagizo hicho.

    "nyimbo za jadi za Tibet zinafanana na muziki pop. Rock na jazz havina soko hapa, hivyo kibwagizo hicho kinapaswa kuwa wazi na kufuata sifa ya jadi. Kila mtibet ataweza kukielewa."

    Bw Bianba alizaliwa katika familia ya kawaida mjini Lhasa. Alipokuwa na umri wa miaka 14, alipelekwa kujifunza kupiga ala ya jadi erhu, ambayo ni fidla yenye nyuzi mbili, kwenye shule ya usanii ya Beijing iliyoanzishwa na Chuo kikuu cha Makabila cha China. Baadaye alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Muziki cha Shanghai kuendelea na masomo yake.

    "Sikujua kwa nini nilichaguliwa. Hakuna mtu yeyote kwenye familia yangu anayefahamu muziki. Hawakunipa mafunzo yoyote kuhusu muziki. Labda nina uwezo fulani wa muziki. Nani anajua?"

    Baada ya kuhitimu, Bw Bianba alirudi katika maskani yake na kupiga kinanda cha erhu kwenye kundi la waimbaji na wachezaji dansi mkoani Tibet. Lakini mwamuziki huyo kijana hakuridhika.

    "nilipenda kupiga kinanda cha erhu nyumbani, lakini nilihisi siwezi kueleza hisia zangu vizuri, hivyo mwaka 1985 nilirudi Shanghai na kumfuata mwongozaji Zhang Guoyong, ambaye ni professa wa Chuo cha Muziki cha Shanghai. Katika muda wa miaka minne, nilisoma kwa bidii na kuelewa zaidi muziki wa magharibi."

    Kutokana na kutaka kutangaza muziki wa magharibi mkoani Tibet, Bw Bianba alirudi Lhasa, lakini aliona kuwa kuna fursa chache sana za kuonyesha muziki wa magharibi."

    "Kulikuwa hakuna soko la muziki wa magharibi mkoani Tibet, kwani Tibet ina watu wachache, hivyo ni vigumu kuwashawishi kuukubali muziki wa magharibi."

    Ili kuboresha hali hiyo, Bw Bianba na wanamuziki wengine wa Tibet walianza kutunga muziki wa kitibet kwa kutumia ala za muziki za magharibi. Walifanaya maonesho majumbani, kwenye maeneo ya shule na katika sehemu kubwa mjini Lhasa.

    "katika miaka ya 80, baadhi ya wanamuziki wa Tibet walianza kukusanya ala za muziki za jadi zilizohifadhiwa kwenye mahekalu na nyumbani mwa familia za musiki za jadi, kwa ajili ya matambiko. Tunatunga muziki kwa kutumia ala hizo na kuzirekebisha ili ziendane na maisha ya sasa.

    Mwaka 2002, bendi ya Philharmonic Okestra ya Tibet ilianzishwa kwa msaada wa serikali kuu. Kila mkesha wa mwaka mpya inapofika, bendi hiyo inafanya maonesho kuadhimisha mwaka mpya yanayotangazwa kwenye televisheni ya Tibet, ambapo kunakuwa na mchanganyiko wa muziki wa magharibi na wa kitibet.

    Bw Bianba anafurahi kuona wazazi wengi wa Tibet wanawapeleka watoto wao kujifunza ala za muziki za magharibi au za jadi za kitibet.

    "Hali imebadilika sana. Familia za kitibet zimeanza kuona umuhimu wa elimu ya muziki kwa watoto. Hivi karibuni kitivo cha muziki kilianzishwa kwenye Chuo Kikuu cha Tibet. Wasanii wengi wa bendi yetu pamoja na mimi, tunafundisha kwenye kitivo hicho, ambacho kimekuwa chimbuko la vijana wengi wenye vipaji vya muziki.

    Baada ya siku moja ya kazi, Bw Bianba anarudi nyumbani karibu na ukumbi wa mazoezi wa kundi la waimbaji na wachezaji dansi wa Tibet. Anafuga ndege mmoja na maua mengi ambavyo vinaleta uchangamfu nyumbani kwake.

    "vifaa vya bendi yetu ni vizuri sana, hata kuliko baadhi ya bendi zilizopo sehemu nyingine nchini China. Ingawa tuna maonyesho machache ya kibiashara, lakini tuna malipo mazuri na nyumba zinazotolewa na serikali. Mkoani Tibet, kuwa mmoja katika bendi yetu ni kazi inayoheshimiwa."

    Bw Bianba anasema anajivunia kuwa mwongozaji pekee wa Tibet nchini China. Lakini sasa, anatarajia kuwa vijana wataweza kupevuka haraka na kuchukua nafasi yake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako