• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1018

    (GMT+08:00) 2011-11-11 16:18:47
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania, anasema wahusika wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa na idara nyingine za CRI na CIBN kwa ujumla pokeeni salamu nyingi kutoka Tanzania huku barani Afrika, natumai kwamba wote hamjambo na mnaendelea vyema na majukumu ya kazi za kila siku ili kuhakikisha kuwa sisi wasikilizaji wenu mnatuandalia matangazo na vipindi murua na vya kuvutia sana.

    Nikiwa msikilizaji wenu hai wa CRI na rafiki wa China ninafurahia sana kupata habari za taifa tukufu la China, watu wake na dunia nzima kwa njia ya redio China kimataifa, kwa sababu hii na kwa mantiki hiyo basi maadhimisho maridhawa ya miaka 70 ya redio China kimataifa ni nuru na mwanga kwa wasikilizaji wa CRI popote walipo humu duniani na pia ni changamoto kwa wasikilizaji wenu wapya na watu wote wapendao amani na maendeleo duniani .

    Ndugu marafiki pamoja na barua hii fupi naambatanisha majibu ya chemsha bongo kuhusu miaka 50 ya idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa nikiamini kuwa itafika kwa wakati, baadaye nitatuma maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhusu maadhimisho hayo na pia kuhusu studio ya jifunze kichina na vipindi vingine, hakika CRI inafanya kazi kubwa na nzuri sana hivyo naipongeza sana.

    Shukran za dhati msikilizaji Kilulu Kulwa kwa barua yako, na kuhusu majibu yako ya chemsha bongo yamefika kwa wakati, jambo lililobaki ni kusubiri kutangazwa kwa washindi, na tunakuomba uendelee kusikiliza matangazo yetu na kutuandikia barua za maoni, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Martin Y. Nyatundo wa S.L.P 2282 Kisii Kenya' anasema nina matumaini makubwa kwamba Rabana amewahifadhi na muwazima wa afya, mimi pia mzima mithili ya kigongo cha mpingo nikiendelea kusukuma mbele gurudumu la maisha lililo zito. Ninashukuru sana kwa juhudi zenu za kuendelea kuiboresha idhaa ya CRI katika kuleta vipindi vipya na kuzidi kuwasiliana nasi ama kwa kweli ni furaha iliyoje kutegea sikio idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa ole wao kwa wale wasioifahamu.

    Hali ya usikivu na matangazo ni nzuri kabisa sauti za watangazaji ni za kuvutia, lugha ni sanifu na ubunifu wa vipindi ni wa hali ya juu, zaidi ni kuitunza kuiboresha na ninawaombea dua njema katika uboreshaji zaidi wa matangazo hayo. Kwa kumalizia nawaomba watangazaji kama ingewezekana mtutembelee hapa Afrika kama mlivyofanya mwaka 2005 na mfanye juhudi ya kuchapisha jarida la daraja la urafiki kati ya China na Afrika kwa hayo machache nawaombea kila la kheri.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Martin Y. Nyatundo kwa barua yako ya maoni, ingawa hilo ombi ulilotuletea ni gumu kidogo kulikubali kwani hivi sasa watangazaji wana shughuli nyingi sana, hata hivyo watangazaji wanaokuja likizo huko huwa wanajitahidi kuwasiliana na wasikilizaji mfano mzuri ni Fadhili Mpunji mara nyingi akija Tanzania anajaribu kuwatafuta wasikilizaji ingawa sio wote jambo ambalo si rahisi. Ahsante sana.

    Ni zamu ya msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Shinyanga Tanzania anasema ni matumaini yangu kuwa hamjambo wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa kutoka mjini Beijing China. Mimi huku ni mzima wa afya njema nikiwa pamoja na klabu ya wasikilizaji wa CRI wa Kahama, na tunaendelea kusikiliza matangazo yenu kama kawaida.

    Pamoja na hayo ni dhahiri kuwa ninapenda kuipongeza sana redio China Kimataifa kwa kuanzisha tena mashindano ya chemsha bongo kuhusu miaka sabini tangu kuasisiwa kwa CRI, Ambapo pia mashindano hayo yanazihusu klabu za wasikilizaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. Ambapo mpaka sasa CRI inatangaza kwa lugha zipatazo 61 na kutangaza kwa saa 12 kila siku pamoja na kuwa na klabu 3165 duniani kote.

    Hivyo basi kwa mantiki hii sina budi kuwafahamisha kuwa klabu yetu ya kahama listeners inawapongezeni sana kwa kuanzisha mashindano hayo ya chemsha bongo kwa kila klabu ya CRI. Na ikiwafahamisha kuwa iko tayari kushiriki katika mashindani hayo. Mimi Stephen Magoye Kumalija nikiwa kama mwenyekiti na mwanzilishi wa klabu yetu, sina budi kuishukuru na kuipongeza kwa dhati CRI na klabu yangu ya Kahama ipo tayari kushiriki kwasababu naielewa sana China na CRI, ambapo mwaka jana nilipata fursa ya kuitembelea China nikiwa pamoja na wenzangu wa nne kutoka Tanzania pamoja na falme za kiarabu. Mwisho nazitakia kila la kheri klabu zote katika kushiriki mashindano hayo.

    Kwanza tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako, pia tunakupongeza kwa kujitahidi kuwashiwishi wanakahama kuanzisha klabu yenu, ni jambo la kutia moyo sana, na tunakuomba uwe na moyo huohuo na tunawapongeza wanachama wote wa kahama listeners club. Ahsante sana.

    Barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi wa Everready Security Guard S.LP 57333 Nairobi Kenya anasema ingawa hapo awali nilikuwa nimekamilisha shindano la chemsha bongo kwa njia ya maandishi pamoja na kutoa mchango wangu wa maoni. Hata hivyo nimefanikiwa kupata nakala ya maswali ya mashindano ya miaka 70 tangu CRI ianzishwe, ingawa nimelipata kwa kuchelewa lakini naamini kuwa litafika kwa wakati uliowekwa.

    Maoni yangu kuhusu haya maswali kuna kasoro kadha wa kadha amabazo zimejitokeza, halikadhalika kwenye majibu, kwa mfano swali la kwanza limekaririwa vizuri lakini kwa upande wa majibu ya kuchagua hakuna jibu linalofaa, swali la saba pia limesanifiwa vizuri lakini kwenye majibu alama ya koma imekosekana yaani kutawanyisha nambari, kwa kuielewa vizuri, nalo swali la mwisho yaani la 8 halina jibu lifaalo.

    Tunapolimulikia swali la nane ambalo jibu lake ni klabu ya Japani hamna jawabu kama hili kwenye makala, kumbukeni kuwa mliyotangaza ndiyo tuliyoyafanya, kwangu mimi nimeshuhudia matatizo kama hayo. Jambo jingine mngetueleza kama mazungumzo yenu yamelenga lugha au nchi kwa ujumla, chunguzeni vizuri hilo shindano mtaona dosari.

    Kwanza tunapenda kukuomba radhi wewe msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi pamoja na wasikilizaji wengine wote, ni kweli tumeona kasoro hizo zimejitokeza kwenye maswali yetu, hata hivyo maswali ambayo tulitangaza redioni na majibu yake ya kuchagua yalikuwa hayana kasoro kama hizo, hivyo tunatumai kuwa wasikilizaji wetu wamejibu kwa mujibu wa makala na maswali tuliyotangaza redioni. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako