• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1025

    (GMT+08:00) 2011-11-11 16:19:13
    Barua ya kwanza inatoka kwa Bwana Mogire machuki wa S.L.P. 646 Kisii Kenya anasema Salamu toka Kisii Kenya. Naamini kuwa mko salama salimini hapo Beijing China na jukumu ni kuchapa kazi kama mimi. Aidha nina furaha kwa mara nyingine kuchangia machache kuhusu matangazo yenu ya kimataifa mwaka 2011 kama nimekuwa nikiyapokea upande huu wa Kisii Kenya.

    Kwanza kama ilivyo kawaida nawafahamisha kuwa hali ya usikivu kwenye wiki hii ya kwanza mwezi Oktoba imekuwa nzuri sana hususani kwenye masafa mafupi kwangu sijakumbana na tatizo lolote kuwapata kwenye masafa mafupi na vilevile matangazo yenu bado twayapokea kwa njia mufti kabisa kupita shirika la Kenya KBC kila siku kupitia masafa ya kati na wimbi la FM hapa magharibi mwa Kenya.

    HIvi karibuni tumeshuhudia matukio mbali mbali kutoka kila pembe ya dunia, na kwa mtazamo wangu nimeona kuwa Redio China imejikakamua kwa kuripoti baadhi ya matukio haya kwa njia ya kuvutia.

    Hivi kumeshushudiwa kifo cha mwanamazingira kutoka Kenya Prof. Wangari Maathai, uwezekanao wa kuwa na jumuiya moja ya Afrika mashariki, sababu ambazo zimepelekea gharama ya maisha hapa Kenya kupanda , ni miongoni mwa ripoti ambazo CRI imeangazia kwa kina na kwa ufasaha kabisa. Pia CRI mmekuwa mkitangaza vipindi maalum yaani mfululizo wa makala kuhusu chimbuko la karatasi nchini China, kweli vipindi hivi vimekuwa vya kusisimua na mengi nimeyafahamu kuhusu historia ya matumizi ya karatasi nchini China. Mojawapo ya kipindi hicho ni kile kilichotangazwa mnamo tarehe 06-oktoba 2011 kilichoangazia historia ya karatasi kule mkoani Sichan-maskani ya Panda na maskani ya karatasi za kuchora na kuandika. Kipindi hiki japo kilikuwa kifupi kilinileta karibu sana na jinsi eneo hili lilivyonufaika na kuwa maarufu kutokana na karatasi zake za kupendeza.

    Aidha pia naendelea kusisitiza kuwa hiki kipindi cha 'jifunze Kichina kwa dakika tano tu' ni kizuri sana ila naomba muwe mnazungumza kwa upole kidogo maana mnaongea haraka mpaka maneno mengine yanatupita. Kipindi chenyewe ni kizuri na je kuna uwezekano wa kipindi hiki kuwa na chemsha bongo kidogo kwa ajili ya wasikilizaji mara moja kwa mwezi. hii itatusaidia sisi wasikilizaji polepole kukielewa Kichina kwa njia iliyo rahisi. Tafadhali tafakari hilo.

    Mtiririko wa vipindi na pia mada zinazoangaziwa na jinsi watangazaji wanavyowasilisha mada wakiwa hewani ni sawa kabisa. Chukulia kwa mfano hiki kipindi cha Cheche zetu na DJ Moses, kweli kipindi hiki cha dakika arobaini ni cha aina yake na kama nilivyowahi elezea kwenye ripoti zangu za awali naonelea ingekuwa jambo nzuri iwapo kipindi hiki kingetumika kwa kucheza mchanganyiko wa nyimbo za jadi za Kiafrika na pia za Kichina na sio tu za kizazi kipya kama nilisikia kwenye kipindi cha tarehe 09 Oktoba mwaka 2011 ambapo DJ alicheza rekodi za kisasa. Ni nadra sana kupata muziki kutoka China kwenye stoo za muziki hapa Afrika mashariki na sisi wasikilizaji wa CRI tunawategemea nyie kwa muziki wa Kichina. Kipindi chenyewe ni kizuri na DJ Moses anafanya kazi nzuri, muziki anauchanganya ipasavyo, ripoti kuhusu wasanii anazotufahamisha kwenye programu ni za aina yake. Kweli anafanya kazi nzuri sana na kipindi chake kina ladha ya kipekee nikilinganisha na vipindi vya muziki vya Redio nyingine za kimataifa.

    Bila shaka nawafahamisha pia kuwa kile kipindi cha 'salamu za wasikilizaji ' pia kina mvuto wa kipekee, jinsi watangazaji wanapokezana zile barua ni sawa kabisa na ule muziki unaochezwa kwenye kipindi hiki ni wa kuchangamsha pia.

    Upande huu wa Kisii kenya nawafahamisha wenzangu hapo CRI ni kuwa matangazo na vipindi vyenu kwa ujumla vinaendelea kupata mwamko mpya. kweli CRI imejipatia nafasi yake kwa kuwa kituo bora cha kimataifa tangu muanze kutangaza kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC. Hapa mna wasikilizaji wengi sana na takwimu zaonyesha kuwa mna wasikilizaji kadhaa kule magharibi mwa Kenya. Hili limetokana na kuwa na mpangilio mpya wa vipindi vyenu na kuongeza nguvu kazi kwenye jumba la CRI. Pia nawafahamisha kuwa CRI imepata umaarufu hapa AFrika mashariki na kati kwa jumla kwa sababu kila mtu anataka kufahamu China ni taifa la aina gani taifa ambalo bidhaa zake tunatumia kila siku? kweli nyingi za bidhaa tunazotumia kwenye maisha yetu ya kila siku hutokea China na hili limechangia pakumba kwa kuongezeka kwa idadi ya wasikilizaji wa CRI bila kusahau kuwepo kwa zile chemsha bongo za kila wakati ambazo kila msikilizaji ana nafasi ya kushiriki akiwa na nia ya kujishindia zawadi kitu ambacho ni nadra sana vituo vingine vya kimataifa kutekeleza. Hivyo matangazo yenu bado yanapendeza kipindi hiki ambapo kuna redio nyingi za kimataifa. Sasa redio tegemezi ni CRI maana ndio kwa sasa pekee inatangaza kwa saa nyingi na rahisi kupatikana hata ingawa kikwazo kikubwa ni chimbuko la vituo vya mawimbi ya FM ambavyo kazi yao ni kupiga tu muziki na kuwa na mijadala isiyofaa kwa jamii. Sisi wasikilizaji waaminifu wa CRI bado matangazo na vipindi tutavisikiliza na pia kuendelea na jukumu la kuhakikisha CRI inaendelea kupata umaarufu wa kipekee siku za mbele.

    Kutoka Kisii kenya nawatakia kila lililo jema mnapoendelea na kazi ya kuandaa vipindi hapo Beijing China.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Mogire machuki kwa barua yako ndefu kidogo ambayo imekusnya mambo mengi kuhusu vipindi na matangazo yetu kwa ujumla, kwa kweli ni jambo la faraja kuona kuna watu kama wewe ambao wanafuatilia kwa undani zaidi kila tunalotangaza. Tunakuomba uendelee kusikiliza zaidi na kutupa maoni yako ili tuweze kujirekebisha pale tunapokosea, ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Julius Alfred wa S.L.P 5019 Tanga Tanzania naye anasema napenda kusema kwa sasa CRI inavuma kwa kishindo kikubwa sana kwani inakubalika na wengi na hii ni kutokana na vipindi vya kukonga moyo pamoja na watangazaji mashuhuri ambapo ni faraja kila tuwasikiapo.

    Ni mara yangu ya pili sasa kuandika barua katika kituo chenu kwani barua ya kwanza ilieleza ju ya ugumu wa kupata matangazo yenu niwapo shuleni kwasababu mawasiliano ya redio kwa shule za bweni ni magumu, isitoshe mimi ni mfuatiliaji wa kipindi cha jifunze kichina. Hivyo kutokana na ugumu wa kupata kipindi hiki nimeomba kutumiwa jarida au kitabu chenye mfululizo wa mafundisho hayo, hii itanisaidia sana kukidhi kiu yangu ya kutaka kujua kuzungumza na kuandika kichina, nitashukuru sana kama ombi langu likipata kibali kwenu.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Julius Alfred kwa barua yako, kusema kweli tunakumbuka barua yako ya mwanzo ambayo ilikuwa imejaa masikitiko kuhusu upatakinaji wa redio China kimataifa huko ulipo masomoni, na ombi lako la vitabu vya kujifunza Kichina tumelipokea na kukutumia, labda itakuwa vimechelewa tu kukufika, ahsante sana.

    Mwisho ni barua kutoka kwa msikilizaji wetu Ras Frans Manko Ngogo

    wa Kemogemba Club S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania. Anasema maoni yangu ni kuhusu Kipindi maalumu cha utengenezaji wa karatasi nchini China. Ama hakika kipindi kilifana sana na kuvutia wasikilizaji kwa mada yake iliyokuwa ya kipekee. Ikumbukwe kuwa karatasi ni kitu kinachotumika kila leo kwa kila mtu. Hivyo ni kama kioja kuona kuwa wengi wetu hatukujua namna ilivyotengenezwa.

    Nilisisimka kusikia karatasi hupitia njia 72 hadi kukamilika kwake. Na ni jambo la kutumaini kusikia kuwa kuna karatasi zinazoweza kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika. Hayo na yale ya waendeshaji wa kipindi waliokuwa wanajitahidi kutangaza kwa lugha inayoeleweka vizuri, yaliwafanya wasikilizaji kutobanduka redioni.

    Hakika uandaaji wa vipindi vyenye maudhui kama hivi ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya radio hii. Ama kwa upande wa tovuti, bado inasomeka vizuri na kuvutia wasomaji. La muhimu katika kuboresha tovuti hii ni kutozidisha vipindi vya siku nyingi na kuviacha katika ukurasa kwa muda mrefu. Nashukuru kwa jitihada za uandaaji wa vipindi murua. Pongezi.

    Kwanza tunapenda kukushukuru msikilizaji wetu Ras Frans Manko Ngogo kwa maoni yako, tunatumai kuwa vipindi maalumu tulivyowaleteeni safari hii vitakuwa vimewapatia maarifa wengi zaidi na kujua hatua mbalimbali za utengenezaji karatasi, na hilo ndio lengo kuu hasa la Idhaa ya Kiswahili ya CRI kuwaelimisha wasikilizaji wake, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako