• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1101

    (GMT+08:00) 2011-11-11 16:19:49
    Barua ya kwanza inatoka kwa Bw. Xavier Lincolyn Telly-Wambwa wa S.L.P 1993, Bungoma, Kenya ametuletea barua akisema Pokea salamu kutoka hapa Embu, Kenya. Mimi ni mzima na natumai nanyi wote mu wazima pia. Ninataka kuwashukuru sana kwa vipindi murua na ni vipindi muhima sana kwa wasikilizaji mimi nikiwa mmoja wao.

    Siku ya Alhamisi usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kwa hakika nilifurahishwa na Bw. Fadhili Mpunji kwa yale yote aliyokumbana nayo katika safari yake ya huko Tibet. Yeye na wanahabari wengine walipokuwa katika mkahawa mmoja, wakijiburudisha na nyama ya kondoo, nilipata fursa ya kusikiliza tumbuizo la nyimbo za kitibeti wakiimba kwa fujo ambapo mimi mwenyewe sikuweza kuvumilia na kuamua kucheza mpaka ulipokwisha.

    Ungedhani ni kama Kihindi lakini la si hivyo. Sauti za warembo hao ni nyororo kweli na za mvuto wa kupendezasa sana. Wanahabari hawa shujaa natumai walijihisi kuwa siku zao za kurudi Beijing zikawie. Je mimi ninauliza iwapo kanda za nyimbo hizo za Kitibet zinaweza kupatikana na mkaweza kunitumia. Pongezi CRI na pongezi kwa wote wahusika wa CRI.

    Shukrani za dhati msikilizaji wetu Xavier Telly-Wambwa kwa barua yako ambayo inaonesha ni jinsi gani unayofuatilia kipindi cha China Mchoni mwetu na kuhusu ombi lako la kutaka kanda za nyimbo za kitibet tutaangalia kama itawezekana tutakutumia, lakini hatuwezi kukuahidi moja kwa moja, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Exaud John Makyao mwenye baruapepe makyaoexaud@yahoo.com naye ametuletea barua yenye kichwa cha habari MSHUMAA UMEZIMIKIA GIZANI, anasema kufariki kwa Mwanaharakati mtetea mazingira na haki za binadamu raia wa Kenya; Profesa Wangari Maathai ni sawa na mshumaa kuzimikia ndani ya GIZA NENE.

    Mshindi wa tunzo ya Amani ya Nobel marehemu Wangari Maathai alikuwa shujaa shupavu katika kutetea haki za kijami, mazingira, demokrasia na kupambana na rushwa. Katika nyakati hizi ambapo Dunia nzima inahitaji sana viongozi wenye maono ya kuitoa dunia kwenye GIZA NENE la athari za uharibifu wa mazingira, kukosekana kwa demokrasia ya kweli na kukithiri kwa rushwa, mtu kama marehemu Profesa Wangari Maathai alihitajika sana.

    Sasa shujaa Profesa Wangari Maathai ameshapumzika; sisi tuliobaki tuzienzi kazi na maono yake kwa kutekeleza kwa bidii na uaminifu wajibu wetu kwa mazingira, jamii na dunia kwa ujumla. Marehemu Profesa Wangari Maathai hakuyafanya hayo yote kwakuwa alikuwa msomi maarufu bali harakati zake hizo ndizo zilizomfanya atambulike kuwa ni msomi maarufu mwenye manufaa kwa jamii yake na dunia kwa ujumla.

    Marehemu Profesa Wangari Maathai hakuwa mtu wa kutafuta faida kutoka kwa jamii iliyomzunguka, bali yeye siku zote alifanya bidii kuipatia jamii iliyomzunguka faida kutoka kwake. Mungu tusaidie sisi viongozi na wakaazi wote wa dunia kuwa na maono ya maendeleo, haki na kutunza rasilimali tulizopewa nawe mwenyezi Mungu ili Duniani pawe mahali salama pa kuishi wakati tukisubiri kuiendea njia ya haki kwa wote. KWELI MSHUMAA UMEZIMIKIA GIZANI.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Exaud John Makyao kwa barua yako, ambapo hata sisi pia tuna huzuni na masikitiko makubwa kwa kumpoteza mwanaharakati Profesa Wangari Maathai mpigania haki za binaadamu na mazingira. Ni pigo kubwa kwa Kenya na Afrika, sisi watu wa duniani tulimpenda lakini tunaamini kuwa Mungu alimpenda zaidi na ndio maana hivi leo hatunaye tena, cha muhimu ni kwa viongozi wa Afrika kuendeleza pale alipofikia na hapo ndio itakuwa kumuenzi kikweli, Mungu ailaze roho yake mahali pema, amin.

    Naye Mutanda Ayub ambaye ametuletea baruapepe kwa anuani ayub06@yahoo.com anasema ningependa kuwatumia salamu kutoka kwa jamii yangu pamoja na wasikilizaji wengine kutoka hapa Bungoma Kenya. Hapa ninaendelea kuwapata hewani bila shida yoyote hivi sasa sinabudi kuwafahamisha kuwa muda wa sanduku la barua kweli umekuwa mchache.

    Na hapo nyuma kidogo barua pamoja na mashairi ambayo nimeyatuma hayajasomwa. Vilevile nimepokea barua pepe kutoka kwa Bw. Ras Manko akisema ni muda sasa tangu aandike barua kwa CRI haijasomwa kwa siku kadhaa. Kwa hivyo tatizo laweza kuwa sisi wasikilizaji labda hatutumi barua nzuri au wasomi na wachapishaji upande mwingine wamepunguza au vipi? JAMBO linalo nikera sasa hivi ni kuwa nimejaribu niwezavyo kusoma makala ya chemsha Bongo katika tovuti ya CRI mwaka huu bila kufanikiwa, haipatikani kabisa na siku ya mwisho ya kutuma majibu yakaribia. Hebu tuelezee tufanye nini?

    Hata hivyo ninafurahia jambo moja kutoka kwa Bw. Ras kuwa kwa sasa anauwezo wa kutuma barua pepe hata kama ni mara moja kwa mwezi au wiki. Bila kusahau jambo hili wakati nilipotembelea mji mkuu wa Kenya niliweza kufuatilia vipindi vizuri na kupata kujua yote ni shwari kabisa. Lakini kama kuna uwezekano tuwe na kipindi kama vile SAUTI ya wasikilizaji.

    Nitajaribu kuwaeleza hili. Kama ni vigumu kujieleza hapa lakini hivi ndivyo mawazo yangu pamoja na washiriki tunaonelea; Ili vipindi viweze kuboreshwa zaidi tuwe na kipindi cha majadiliano na mahojiano kati ya watangazaji na wasikilizaji wa CRI kwa njia ya ujumbe mfupi (sms), Barua pepe, na hata kupiga simu moja kwa moja ambapo wasikilizaji wataweza kupata fursa ya kutoa maoni yao bila kukawia. Ndipo hiki kipindi chaweza kujulikakana kama SAUTI YA WASIKILIZAJI.

    Vilevile katika kuwepo kwa kipindi hiki wasikilizaji waweza kupewa nafasi ya kutuma salamu au kutoa anwani zao kwa wale waohitaji mawasiliano haswa kwa marafiki, Jamaa zao kujuliana hali na fursa hii Itawezesha Vilabu vya wasikilizaji kutoka pande zote za dunia kubadilishana maoni jinsi wanavyoendelea. Jambo jingine ni kwamba tuwe na angalau uwezekano wa wahariri /waandishi wa CRI kutembelea wasikilizaji hata ni kama mara moja kwa mwaka. Hii itakuwa njia moja ya kuleta ushirikiano na maelewano zaidi na ya kipekee. Kati ya wasikilizaji kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo DRC, na Afrika kwa jumla.

    Shukran Bwana Mutanda Ayub kwa barua yako ambayo ina maoni mazuri tu, kila siku tunajitahidi kusoma barua za wasikilizaji wetu, ni kweli barua ni nyingi, lakini tunajitihidi. Vilevile kuhusu kufanya kipindi cha sauti ya wasikilizaji au kufanya majadiliano na mahojiano kati ya watangazaji na wasikilizaji wa CRI kwa njia ya ujumbe mfupi (sms), Barua pepe, na hata kupiga simu moja kwa moja tuliwahi kujibu kuwa itakuwa vigumu kwa kiasi Fulani, labda hapo baadae tukiweza kurusha matangazo moja kwa moja hewani tunaweza kufanya hivyo. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako