• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1108

    (GMT+08:00) 2011-11-11 16:20:22
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Exaud Mkyao ambaye ametuletelea baruapepe yenye anuani makyaoexaud@yahoo.com na ameanza kwa kuuliza "BADO KILIMO NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI WA TANZANIA?

    Marehemu baba wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema; "KILIMO NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI WA TAIFA LA TANZANIA". Dhana hii bado ipo mioyoni na vinywani mwa watanzania wengi ila sioni vitendo vinavyoambatana na dhana hii ya kilimo kuwa uti wa mgongo Tanzania. Kwa mujibu wa marehemu mwalimu Nyerere, usemi huu ulimaanisha kwamba hali ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania utategemea maendeleo ya sekta ya kilimo.

    Kilimo kikiwa katika hali nzuri katika taifa la Tanzania ambalo inasadikiwa kuwa asilimia 95 ya raia wake wanaishi vijijini, basi uchumi wa nchi ya Tanzania utakuwa katika hali nzuri pia. Je dhana hii ya kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania ilikufa na Mwalimu Nyerere? Sijui kama viongozi wetu wa sasa wanamaanisha nini wanapoendelea kuimbisha wimbo wa kilimo ni uti wa mgongo huku wakicheza ngoma ya kilimo ni adhabu.

    Viongozi wetu wanapaswa kuanza kusoma alama za nyakati na kugundua kuwa kwanini kumekuwa na mfumuko mkubwa wa watu kuhama vijijini na kufurikia mijini. Kama kweli Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, basi serikali ya Tanzania kwa uchache ifanye yafuatayo:-

    *Wizara ya kilimo isiendelee kupewa bajeti finyu mwaka hadi mwaka kama ilivyo kasumba.

    *Kuzidi kupanda kwa bei za pembejeo kudhibitiwe, kwa serikali kuweka ruzuku ya kutosha katika pembejeo hizo ili kumpa nafuu mkulima.

    *Serikali itafute masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo ili kupunguza uharibifu unaofanyika wakati wa mavuno.

    *Harakati za uanzishwaji viwanda kwa ajili ya mazao ya kilimo zianzishwe ili usindikaji ufanywe hapa nchini.

    *Wawekezaji wakubwa toka nje na ndani ya nchi, washawishiwe kuwekeza katika sekta ya kilimo sambamba na maendeleo ya viwanda.

    *Barabara vijijini ziimarishwe ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na wakulima majira yote ya mwaka.

    *Juhudi za makusudi zifanywe ili kumkomboa mkulima kutoka katika kifungo cha Jembe la mkono na zana duni za uvunaji na uhifadhi wa mazao ya kilimo.

    *Wataalamu wa kilimo kutoka serikalini wawepo vijijini kwa wingi ili kutoa ushauri sahihi kwa wakulima kila unapohitajika.

    *Huduma za umeme, maji, vituo vya utafiti na mawasiliano ya kiteknolojia vipewe umuhimu vijijini pia.

    Kama mambo hayo yatafanyika itakuwa na maana ya kweli kuhubiri kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi wa taifa la Tanzania.

    Vinginevyo tutaendelea kuwa wasanii wa wimbo wa kilimo ni uti wa mgongo, huku tukicheza ngoma ya kilimo ni adhabu.

    Shukrani za dhati msikilizaji wetu Exaud Mkyao kwa barua yako, na vile vile kwa maoni yako uliyotoa, tunatumai kuwa kama kuna wahusika ambao wamesikia watajaribu kuyafanyia kazi kwani ni maoni mazuri tu, hasa ukizingatia kuwa Tanzania ni nchi yenye ardhi nzuri kwa kilimo.na kama dhana hiyo itaendelezwa kufuatiliwa na kutekelezwa basi itasaidia sana kupatikana kwa mazao mengi nchini Tanzania badala ya kuagiza kutoka nchi za nje. Ahsante sana

    Na msikilizaji wetu mwingine aliyetuletea barua ni Bw. Xavier Lincolyn Telly-Wambwa naye anasema ninashukuru sana kwa kunijulia hali na kunitia mori kuhusu usikivu wangu katika vipindi vizuri, vizuri kutoka Redio China Kimataifa huko Beijing kupitia kwa salamu. Ninatumai kuwa mambo ni kukuru kakara katika shughuli ya kutusaidia wasikilizaji wa Idhaa Ya Swahili hili kudumisha urafiki wa usikilizaji.

    Mimi ninapenda kuwajulisha eti ninaposikiliza Redio China Kimataifa ninakuwa na maringo tele ya kufaidi mafunzo mema katika matangazo yenu yanayohusika na vipindi vya sekta tofauti tofauti. Basi ninawapongeza kwa kujitolea kwa ajili yetu. Ninatamani kufanya kazi pamoja nanyi siku moja. Asante tu sana kwa kujisikia vyema baada ya kusoma barua pepe hii kutoka kwangu.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Xavier Lincolyn Telly-Wambwa kwa barua yako tunakuomba uendelee kusikiliza matangazo yetu na kututumia maoni na mapendekezo yako ili kuyaboresha zaidi. Ahsante sana

    Barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania naye anasema moja ya masuala muhimu ambayp mimi hupenda mimi hupenda kuona yanapewa kipaumbele katika dunia nzima ni uhifadhi wa mazingira. Redio China Kimataifa na vyombo vingine vya habari vimekuwa vikiripoti juhudi na mikakati ya China ya kukabiliana na kuongezeka kwa joto duniani linalosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za kila siku binaadamu.

    Kwa mujibu wa ripoti za utafiti wa sayansi ya mazingira, ukame, mafuriko, joto kuongezeka, theluji kuanza kuyeyuka milimani, kutabiriwa kuwa baadhi ya visiwa humu duniani vitatoweka kabisa katika uso wa dunia kwa kuzama katika miaka ijayo ni matokeo mabaya uharibifu wa mazingira. Ikiwa ni viashiria vibaya na hatari vinavyotishia maisha na usalama wa binaadamu wote.

    Nchi zilizoemdelea za viwanda na zile zinazoinukia zimekuwa walengwa namba moja wa lawama hizo.wanaharakati wa mazingira na viumbe hai wamekwenda mbali zaidi na kusema kwamba mgogoro wa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa ni kibepari zaidi kwa kuwa nguvu ya soko ndiyo iliyotufikisha katika hali hii mbaya. Katika mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uliofanyika jiji Cancun, Mexico wanaharakati na viongizi mbalimbali duniani walitoa maoni yao, hisia zao, wasiwasi wao mapendekezo yao na mikakati ya mipango yao ili kuzuia kuongezeka kwa joto duniani.

    Mkutano huo ulionesha kupata mafanikio kwa kufikiwa kwa makubaliano maalumu hivyo mimi nikiwa msikilizaji wa redio China kimataifa naunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na China na nchi nyingine katika kupunguza hatua kwa hatua kuongezeka kwa joto duniani, tuyatunze mazingira ili yaweze kututunza.

    Kwanza tunakushukuru sana msikilizaji wetu Kilulu Kulwa kwa maoni yako murua kuhusu mabadiliko ya hewa duniani. Pia nasi tunaungana nawe kwa kuzipongeza nchi zote zinazojitahidi kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa ya kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa, wengi tunafahamu kuwa Afrika ndio waathirika wakubwa, hivyo viongozi wahusika tunaomba waendelee kuzisaidia nchi hizo ili kuondokana na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako