• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tamthiliya ya Kiswahili ya Doudou na Mama Wakwe zake

    (GMT+08:00) 2011-11-22 16:41:57

    Leo kwanza tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu habari moja ya kufurahisha, kwamba tamthiliya ya China inayoitwa Doudou na mama wakwe zake ambayo imetafsiriwa na kutiwa sauti ya Kiswahili itazinduliwa kesho tarehe 23 huko Dar es salaamu, Tanzania, na sherehe ya uzinduzi wa tamthiliya hii utafanyika kwenye TBC1 saa 12 jioni siku hiyo, baadaye tamthiliya hiyo itaoneshwa kwenye kituo cha televisheni cha TBC1.

    Kweli ni habari nzuri. Tamthiliya hii tumeisubiri kwa muda mrefu. nadhani kwanza tungewafahamisha wasikilizaji wetu kuhusu tamthiliya hii. Kutokana na makubaliano kati ya serikali za China na Tanzania, tamthiliya hii ya Kichina ilichaguliwa kutafsiriwa kuwa ya Kiswahili na kutiwa sauti ya Kiswahili, halafu kuonyeshwa katika televisheni ya TBC1. Idhaa yetu ya kiswahili ya CRI, ilibahatika kupata fursa ya kufanya kazi hii mwishoni mwa mwaka jana, na kazi ya kutafsiri na kutia sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthiliya ya Kiswahili imefanyika kwa zaidi ya miezi 10, kweli si rahisi. Na waigizaji kutoka Kenya na watangazaji wote wa Idhaa yetu ya Kiswahili tumeshiriki katika kazi ya kutia sauti ya Kiswahili kwa tamthiliya hiyo kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na nchi za Afrika ya mashariki.

    Karibu watu wote wa idhaa yetu tulijiunga na kazi ya kutafsiri kwa Kiswahili tamthiliya hiyo ya Kichina.

    Msichana Doudou aliolewa na kijana Yu Wei, ambaye ndoa ya wazazi wake ilivunjika, na kila mmoja akafunga ndoa tena, kwa hiyo kijana Yu Wei ana baba wawili na mama wawili, basi mkewe Doudou anapaswa kuishi na mama wakwe zake wawili, ambao wanazozana kila mara kutokana na uhusiano kati yao kama paka na chui. Kwa hiyo ni vigumu kwake Doudou kushughulikia vizuri uhusiano kati yake na mama wakwe hao wawili ambao hawapendani. Na pia ni kazi ngumu kwa mume wake Yu Wei kuishi pamoja na mama yake na mke wake bila kukumbwa na matatizo.

    Kila mwaka China inatengeneza tamthiliya nyingi za aina mbalimbali, tamthiliya hiyo ya Doudou na mama wakwe zake imechaguliwa kuwa tamthiliya ya kwanza kuonesha katika nchi za Afrika ya Mashariki, kwa sababu inapendwa na watu wengi hapa China, kwani imeonesha maisha ya kawaida ya wachina ya kila siku, watu wakiitazama, wanaweza kujionea mvuto wa maisha ya kawaida ambayo yanajaa furaha na mabishano kila mara kutokana na mambo madogomadogo yanayotokea kila siku katika maisha ya watu.

    Hapa China kuna tamthiliya za aina mbalimbali zinaohusu maisha ya kawaida ya watu, matukio ya kuwavutia watu, mapenzi kati ya watu na kadhalika, ingawa watu wengi wanapenda kutazama tamthiliya zinazoeleza matukio mbalimbali kama vile ya kufanya uchunguzi kuhusu majasusi, mauaji na kadhalika. Lakini tamthiliya zinazoeleza maisha ya kawaida ya watu ambayo yanaweza kugusa hisia za watu huwavutia watu zaidi.

    Watu wengi wanapenda kutazama tamthiliya ya Doudou na mama wakwe zake kwa sababu tamthiliya hii imeonesha maisha ya kawaida ya watu ya kila siku, ambayo inawawezesha watu waone mvuto wa maisha ya kawaida. Tamthiliya hiyo iliyoonesha maisha ya watu katika pande za familia, uchumi na ndoa inahusiana na maisha ya kawaida ya watu, takriban kila mtu anaweza kuona kivuli chake katika tamthiliya hiyo, watu wengi wanaweza kusema, mimi ni kama mhusika fulani, au mimi naishi kama mhusika fulani, tamthiliya hiyo ni kama kioo kwa kila mtu, hivyo inaweza kugusa hisia za kila mtu. Tunaona maisha ya binadamu karibu ni sawasawa, ingawa China iko mbali na nchi za Afrika, lakini baada ya kutazama tamthiliya hiyo, watazamaji wa Tanzania mtaona wachina na waafrika wanafanana katika maisha. Ni matumaini yetu kwamba, wasikilizaji wetu mkipata habari kuhusu tamthiliya hiyo mtapata fursa ya kutazama tamthiliya hiyo, na mtafurahi mwishowe.

    Barua za wasikilizaji

    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi wa EVEREADY Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anasema baada ya kuwapa majina na anuani wasikiliazaji saba ambao walitamani sana kusajiliwa na kuorodhoshwa kuwa miongoni mwa wasikilizaji kwa hakika hilo limetimia. Mara tu waliposikia barua hiyo ikisomwa hewani wote saba walinipigia simu wakiniarifu kuwa lengo lao limetimia, nami niliwauliza maswali kadhaa.

    Kwanza lilikuwa je barua hiyo ilisomwa kwenye kipindi kipi na imesomwa na nani na nani? Kwa kweli walinijibu wakisema kuwa kituo ni CRI na imesomwa kwenye kipindi cha sanduku la barua na imesomwa na watangazaji wenye tajriba kubwa ya utangazaji na waliobobea kimataifa mama Chen na Bibie Pili Mwinyi. Mazungumzo yangu na wao kwa njia ya simu yalikuwa ya kufana kabisa ambapo niliwaahidi kuwa nitaendelea kuwataarifu na kuwajuza mengi yanapotokea kila mara.

    Hata hivyo niliwakumbusha kwamba nitaendelea kuwasiliana nao kila siku kwa kuwaarifu yaliyomo kwenye matangazo kwani sisi hapa Nairobi hupokea matangazo haya kwenye muda wa saa mbili asubuhi ambapo wao wanasikiliza saa nne usiku kupitia KBC Idhaa ya taifa, na baada ya siku chache tu walinifahamisha kuwa wameshapokea barua zao kutoka CRI, ambapo walieleza furaha yao kubwa pia walinifahamisha kwa simu kuwa wao pamoja na jamaa na marafiki zao walipokea barua hizo kwa shamrashamra.

    Mwisho nikiwanukuu kwa pamoja walisema CRI sasa imewafikia vijijini yaani ni kama umeme uliowashwa kwenye giza totoro, walionesha msimamo wao kuwa wataendelea kusikiliza na kufuatilia matangazo na vipindi vya CRI kila siku hatimaye watakuwa mabalozi wema wa CRI. Kwa kauli yao ya pamoja walinishukuru sana kwa kuwafikisha mahali walipofika.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Geofrey Wandera kwa barua na kwa moyo wako wa kuwasaidia wasikilizaji wetu wengine hadi wakaweza kutambulika na kuwa wanachama wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa, tunakuomba uendeleee zaidi kuwa balozi wetu kwa huko Kenya. Ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Chacha Samuel Ngogo wa Tanzania, naye anasema kwanza napenda kuwapongeza jamii nzima inayohusika na maendeleo ya Redio China Kimataifa kwa kuhakikisha kwamba wasikilizaji wote wanaendelea kupata matangazo yenu kwa uhakika zaidi bila ya tatizo lolote. Pia kwa kuonesha kuwa mnajali sana wasikilizaji wenu na kuona kuwa kuna umuhimu wa kuwepo kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka sabini na kuweza kujumuika nanyi ni suala la busara sana.

    Katika suala zima la maendeleo ya redio China kimataifa napenda kama mdau mkubwa wa redio kuona kuwa inaendelea kutoka sehemu moja kwenda nyingine yaani kuongeza studio za FM katika sehemu mbalimbali bila kusahau nchini kwangu Tanzania ili kuongeza mashabiki na wasikilizaji pia na kufanikisha malengo ya redio China kimataifa ifikiapo maadhimisho yake ya miaka sabini na moja, pia napenda kuona uhusiano wa waandishi wa nchi yetu na China unakuwa mkubwa zaidi.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Chacha Samuel Ngogo kwa barua yako, kuhusu kuanza kurusha matangazo huko Tanzania mpaka sasa hatua moja imeshapigwa kwani Zanziba wanatupata safi sana kupitia FM na huko Tanzania bara juhudi bado zinaendelea ili kufanikisha hilo, tunakuomba wewe na wasikilizaji wetu wengine kuwa wastahamilivu. Ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Deborah Bhoke wa S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania naye anasema nikiwa kama mwanamke mwenye umri wa miaka 37 sasa, ninayeishi kijijini, fundi wa kushona nguo, napata moyo sana niwapo kando ya redio yenu ya CRI, Idhaa ya Kiswahili ambayo ina mambo ya kuelimisha na kufurahisha.

    Chemsha bongo hii ya sasa ya kutimiza miaka 70 tangu CRI ianzishwe inanifanya niiamini mno kwa kile kilichotajwa kwenye makala zote nne za chemsha bongo, zinatambua vizuri kazi za akina mama wazifanyazo katika kila kona ya dunia. Mfano mzuri ni huyo Bi Hara Kiyoshi mama wa kijapani aliyeanzia kutangaza kwenye pango ili kupunguza uhasama wa vita kati ya Japana na China miaka 70 iliyopita.

    Naomba kila mmoja wetu akubaliane na hali halisi ya usemi usemao "kila mwanamme aliyefanikiwa basi nyuma yake yupo mwanamke" hebu angalieni Fangbingbing alivyoifanya ile ziara ya waandishi wa Russia na China hadi ikafanikiwa vizuri. Naomba msichoke kuwajali wanawake kwa busara, bidii na nia yao njema ya kuendeleza kila sekta, vilevile mama Chen wa CRI idhaa ya Kiswahili alivyoweka sawa wasikilizaji wote wa idhaa hiyo kuwa kitu kimoja, na sasa muone vizuri Bi Han Mei anayefanya haya yote yawe katika mstari ulionyooka.

    Naona nisijisahau kwa sifa kemkem ni Deborah Bhoke aliyekuwa bega kwa bega katika juhudi za kuimarisha klabu ya wasikilizaji ya Kemogemba, ninao wajibu mmoja wa kustawisha na kuimarisha maendeleo yake kwa kusudi la kutoa urithi kwa vizazi vijavyo, kama mwanamke najua hilo kuwa ni dhima na muhimu kwa maana sisi wanawake ni vichwa vya jamii yote.

    Ni wajibu wetu pia kuwa mbele katika kuwafunza lugha ya kichina wanachama na watoto wetu kwa njia ya kuimarisha urafiki kwa China na Afrika. Namalizia nikiwa na ujumbe wa kuwataka radhi kama nimekosea ama kuwaomba kuungana nami katika hili suala la kuimarisha mahusiano na kuboresha vipindi vya redio China Kimataifa. Ahsante.

    Kwanza tunapenda kutoa shukurani zetu za dhati kwako msikilizaji wetu Deborah Bhoke kwa barua yako na ujumbe na maoni yako murua kabisa, kwa kweli kama ulivyosema mwanamke ni mtu muhimu katika jamii, na ndio maana wanasema ukimuelimisha mwanamke mmoja ni sawa na kuielimisha jamii nzima, wanawake wanamchamgo mkubwa katika jamii yoyote ile duniani, muhimu tuongeze bidiii wanawake sote duniani katika kutetetea haki zetu na tunapozipata tuzitumie ipasavyo.

    Naye msikilizaji wetu Hilal Nassor Alkindy wa S.L.P22 P.C Oman anasema nashukuru sana kwa barua zenu na picha nzuri za maendeleo ya China kwa hiyo naomba msinisahau kila mara mnitumie na nisome yenye manufaa. Ahsante sana.

    Tunakamilisha kwa barua ya Eric Makori Aoga wa S.L.P 1805 Kisii Kenya anasema ningependa kuchukua fursa hii kuwapa pongezi na shukurani nyingi kwa kazi mnayoifanya kama watangazaji kwasababu mnatupa fursa ya kujuliana hali na ndugu, jamaa na marafiki zetu popote pale walipo na hasa kutufahamisha hali na jinsi China inavyoendelea na matukio yake.

    Ninawaombea Mola azidi kuwapa afya, neema na baraka zake kwa kazi mnayoifanya na hata mimi naomba nijazie hekima na busara ninapoendelea na masomo yangu ili niweze kujiunga nanyi.

    Shukurani za dhati wasikilizaji wetu Hilal Nassor Alkindy na Eric Makori Aoga kwa barua zenu fupi, tunawaomba muendelee kusikiliza matangazo yetu na kututumia maoni na mapendekezo yenu. Ahsanteni sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako