• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mahesabu ya gharama ya talaka nchini China yawazuia baadhi ya wanandoa kuachana

    (GMT+08:00) 2012-01-07 18:21:15

    Kila siku ndoa elfu 5 zinavunjika nchini China. Lakini mahesabu ya gharama ya talaka kwenye mtandao imewafanya wafikiri mara mbili kuhusu kutalikiana. Wanandoa wameanza kutembelea tovuti za "My Divorce Calculator" au "Bailixia Forest Divorce Calculator" ili kufahamu watapoteza kiasi gani kama watapeana talaka.

    Mwanasheria mjini Beijing Si Pengfei anasema kwa uzoefu wake, ongezeko kubwa la talaka nchini China kati ya wanandoa wenye umri kati ya miaka 20 na 30 linatokana na sababu mbalimbali.

    "Kuna mambo mengi ya kutatanisha yanayosababisha kuvunjika kwa ndoa nchini China, kubwa zaidi ikiwa ni kukosa uaminifu katika ndoa, yaani uzinifu, mawasiliano mabaya, kuishi kwenye miji tofauti na shinikizo la maisha. Hususan kwa watu wenye umri wa miaka 30 hivi, mara nyingi wanaachana kutokana na matatizo ya kifedha, uzinifu na kuishi sehemu tofauti kwa muda mrefu. Vilevile watu wenye umri huo wana maamuzi ya haraka linapokuja suala la talaka."

    Inawezekana kuwa wanafanya kazi sana, hivyo inakuwa rahisi kwao kukata tamaa na ndoa zao, lakini kuna sababu nyingine pia. Dokta Rick Ruiter kutoka Canada amekuwa mshauri wa ndoa kwa miaka 25, na ameishi China kwa miaka 7. Anaona watoto wa kizazi hiki wanakabiliwa na tatizo la kuwa tegemezi kupita kiasi.

    "Watoto hawa wanalelewa na babu na bibi zao, kila mara wanaishi katika hali ya upweke sana, na hawapati mafunzo yoyote, wanafanyiwa kila kitu. Hivyo unapofika umri wa kufunga ndoa, na huwa kuna shinikizo kubwa kutoka wazazi, serikali na wengine, kuwataka wafunge ndoa, wanafanya hivyo bila kuwa na maandalizi yoyote"

    Shinikizo la kufunga ndoa ni tatizo moja, lakini Dk. Ruiter anasema mawasiliano baada ya kipindi cha fungate kumalizika ni tatizo kubwa zaidi. Kwani wanandoa wengi hawana muda wa kutatua tofauti zao katika maisha yao ya kila siku, hivyo kama mambo hayaendi vizuri, ni rahisi zaidi kwao kuachana.

    Wanapoanza kutafuta taarifa kwenye mitandao, ndipo wanakuta mitandao ya China kama mtandao wa Wulumqi Online. Huo Yanwen, mhariri wa tovuti hiyo, anaeleza ni kwa nini wanatoa taarifa, mabaraza, gharama za talaka na mambo mengine.

    "Kuna msemo wa zamani wa Wachina unaosema 'ni vigumu kukutana na watu asiye na kasoro maishani, hivyo mthamini huyo uliye naye'. Hata hivyo, siku hizi watu wana haraka na wenzi wao, hawavumilii ndoa zao kutokana na mambo madogo tu. Natarajia kuwa tovuti hii itawakumbusha watulie na kufikiri kuhusu ndoa zao, japo katika upande wa fedha."

    Tovuti ya Forest Divorce Calculator ilianzishwa na Dang Yongzhong. Alianzisha tovuti hii kwa sababu tovuti ya kiingereza ilikuwa ni ngumu sana kwa wanandoa wachina kuielewa. Hivyo alianzisha tovuti hii kwa lengo la kuwakumbusha Wachina wakitalikiana si kama tu watapoteza mapenzi, bali pia watapoteza fedha kila upande.

    Talaka haina gharama kubwa, bali ni mgawanyo wa mali. Tovuti ya hesabu ya talaka inatoa taarifa za wanandoa, ikiwa ni pamoja na nyumba, mali, magari, na kadhalika. Lakini Si Pengfei anatahadharisha kuwa gharama hiyo ni makadirio tu.

    "Mjini Beijing, kama wanandoa wana nyumba yenye thamani ya yuan milioni 1.5 (sawa na tsh milioni 375), gharama ya kuiandikisha mahakamani ni yuan 3,000, kuweka wakili yuan 10,000, kukadiria thamani ya mali yuan elfu 15, jumla ya vyote hivyo ni yuan elfu 20. Wanandoa wengi wana mali yenye thamani ya kati ya yuan milioni 1.5 hadi milioni 3, ada za kuweka wakili ni kati yuan elfu kati ya 10 na 20, ukijumlisha vyote hivyo, utaona kuwa inabidi utoe yuan elfu 20 kabla ya kupata talaka."

    Lakini bado Dk. Ruiter anasema, hesabu kama hizi zinazowatisha wanandoa na kuwafanya wasitishe uamuzi wao wa kuachana kwa hofu ya vurugu katika mgawanyo wa mali pia si jambo zuri. Ndoa inahitaji vitu vingi zaidi ya nia ya kuwa na ndoa.

    "Ni jambo zuri kwa wanandoa kuishi pamoja kwani inawabidi washighulikie ndoa yao. Kama wakiachana, nadhani hii inatakiwa kuwa hatua ya mwisho, lakini baadaye wataingia kwenye mzunguko anaojirudia. Kama hawatakuwa na jitihada binafsi za kukua na kujiendeleza, basi watakuwa wanarudia jambo hilo. Hivyo naona ni bora kuishi pamoja na kila mmoja kujituma ili kujipatia maendeleo na kuboresha uhusiano kati yao."

    Kwa bahati mbaya, ni rahisi zaidi kusema suluhu ya matatizo kuliko kutatua tatizo lenyewe. Huenda fedha haiwezi kununua mapenzi na furaha, lakini kutokana na kuogopa kupoteza fedha, baadhi ya wanandoa wanaendelea na ndoa zao."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako