Katika sehemu za milimani za magharibi mwa mkoa wa Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, kuna tarishi mmoja ambaye ni kiziwi na bubu. Kila siku anapanda pikipiki kupeleka barua, magazeti na mizigo kwa familia zipatazo elfu 5, na kwa wastani kila mwaka anasafiri kwa kilomita elfu 25 kupeleka maelfu ya barua, lakini hajawahi kufanya makosa yoyote, na anachukuliwa kuwa ni ndugu wa wanakijiji hao. .
Familia zipatazo 5000 katika vijiji vidogo zaidi ya 120 ambavyo vimesambaa katika tarafa ya Longtan mjini Beipiao, katika mlima wa Nuluerhu wenye kilomita 300 za mraba, na wenye umbali wa mita 800 kutoka usawa wa bahari . Kutokana na vijia vyenye taabu mlimani, katika miaka 10 iliyopita ni tarishi mmoja tu ambaye anatoa huduma ya kupeleka barua katika tarafa hiyo, na ndiye tuliyetaja hapo kabla, yule mlemavu anayeitwa Huang Wei, mwenye umri wa miaka 37.
Vijia vya mlimani siyo vya tambarare, ni taabu kupita, na kila mara inambidi Huang Wei apande pikipiki kusafiri umbali wa kilomita 20 na ili afike kijijini. Mara baada ya kusikia sauti ya filimbi aliyopiga Huang Wei, mama Wang Xianrong wa familia iliyopo mashariki mwa kijiji, anatoka nyumbani kwake na kumkaribisha. Mume wa mama huyo anapenda kuchora na anajulikana kuwa mtu mwenye elimu katika kijiji hicho ambaye kila mwaka anaagiza magazeti na majarida, hivyo tarishi Huang Wei anafika nyumbani kwao mara kwa mara. Mama Wang anasema,
"Kila mara Wang Wei anatuletea barua na magazeti bila kukawia, tunamtegemea sana."
Njia anazotumia kupeleka barua ni mbili, moja ni kuelekea upande wa kaskazini mwa posta ya tarafa ya Longtan, ambapo asilimia 60 ya vijiji vya tarafa hiyo viko katika sehemu za upande huo, na vyote viko katika sehemu za mlimani, na njia nyingine inaelekea upande wa magharibi na kusini mwa posta ya tarafa. Ingawa vijiji vilivyopo katika sehemu hiyo viko karibu na barabara, lakini kuingia kijijini ni lazima kupita vijia vingi ambavyo ni taabu kupita, ambapo migodi mingi vinatapakaa pale, hivyo kila anapeleka barua moja, anapaswa kusafiri kwa kilomita 10 kwenye vijia mlimani.
Mwezi Januari Mwaka 2000, Huang Wei anayependa kukusanya stempu, alipata nafasi ya pili katika shindano la kukusanya stempu mkoani Liaoning, hali iliyomfanya Huang Wei ajulikane miongoni mwa viongozi wa posta za mji wa Beipiao. Kwa bahati, wakati ule Kata ya Longtan ilikuwa inahitaji tarishi mmoja, na Huang Wei alijitokeza. Tokea mwezi Mei mwaka huo, Huang Wei aliyekuwa na umri wa miaka 25 wakati huo, akawa tarishi wa posta ya tarafa ya Longtan. Kijana huyo anathamini sana kazi hiyo, na kila siku anapeleka barua kwa wanavijiji hao. Mkurugenzi wa posta hiyo Bw. Ma Xiaobo anasema,
"Kabla ya Huang Wei kuja, matarishi walipeleka barua kwa vijiji mbalimbali, ambavyo navyo vilipeleka barua hizo kwa wanavijiji, lakini sasa Huang Wei anapeleka barua moja kwa moja mikononi mwa watu."
Tarishi katika sehemu za milimani si kama tu anapeleka barua, magazeti na hati ya kupokea pesa, bali pia anapeleka vifaa vya maisha na pembejeo. Kila alfajiri, Huang Wei anafika posta mapema kuchukua vitu hivyo na kuviweka katika mifuko yake miwili, kisha anapanda pikipiki yake na kusafiri zaidi ya kilomita mia moja. Mama yake anasema,
"Hujaona mifuko anayobeba, ni mikubwa mno. Mifuko imejaa vitu mbalimbali, ikiwemo sabuni na sabuni ya unga, mvinyo, shangpo, hata dawa za kuua vijidudu."
Vijia vigumu mlimani na mzigo mzito, taabu hizo zote Huang Wei anaweza kuzishinda, lakini yeye ni mtu mwenye ulemavu wa kusikia na kuongea, inambidi akabiliane na changamoto zinazosababishwa na ulemavu wake. Mama Wang anasema,
"Hawezi kuongea wala kusikia, hivyo anashindwa kumwita mtu aje achukue barua. Nilimwambia achukue filimbi iliyokuwepo nyumbani kwetu, akipuliza basi mtu atatoka."
Tangu hapo, filimbi ya Huang Wei inasikika kote katika tarafa ya Longtan.
Ili kupeleka barua kwa watu bila kukawia, Huang Wei anachora ramani ya kila kijiji, ambayo ina majina ya familia, namba za nyumba, upande wa nyumba na njia ya kufika nyumbani hapo.
Barua ni njia kuu wanayotumia wanakijiji hao kuwasiliana na nje, hivyo watu wanaoishi milimani wanategemea sana posta. Wakati wa sikukuu, watu wanaofanya kazi mijini au wanaosoma wanaandikia barua au kuwatumia pesa jamaa zao, na wakati huo Huang anakuwa na kazi nyingi, lakini anaendelea kufanya kazi kwa makini. Mtu anayeshughulikia kupokea barua katika kijiji cha Qianjingzi Xu Xiangcai anasema,
"Kijiji chetu kina watu watano wenye majina sawa, na kabla ya kuwapatia barua, kwanza Haung anathibitisha vitambulisho vyao, halafu anaangalia ramani ya eneo la makazi yao."
Mwaka mmoja wakati wa majira ya joto, Huang alipeleka barua kwenye kampuni moja, kwa bahati mbaya, mtu aliyestahili kupokea barua hakuwepo, ili kuhakikisha barua inamfikia, Haung alimsubiri mtu huyo arudi ili apokee barua wakati hali ya hewa ilikuwa nyuzi joto juu ya 30."
Mbali na kupeleka barua na mizigo, vilevile Huang Wei anawasaidia wanakijiji kupeleka ujumbe. Baadhi ya wakati, wanakijiji wanamwomba kupeleka ujumbe au vitu kwa jamaa zao wanaoishi katika kijiji kingine, na kwa sababu Huang Wei anapenda kuwasaidia wengine, haoni tatizo kufanya hivyo.
Miaka kumi imepita, njia ya Huang Wei ya kupeleka barua imefikia urefu wa kilomita laki 2.5 na amepeleka barua elfu 60, lakini hajawahi kufanya makosa yoyote, na wanavijiji wote wanamwamini na kumsifu sana.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |