• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kupeana upendo

    (GMT+08:00) 2012-02-13 15:19:44

    Siku chache zilizopita, kijana Jia Xiaodong kutoka mji wa Shenyang, mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China na Li Yao kutoka mji wa Benxi mkoani humo walifunga ndoa. Vijana hao wawili walikutana na kupendana kupitia mtoto mmoja kutoka Mianyang, Sichuan, mkoa uliopo mbali na Liaoning. ..

    Jia Xiaodong mwenye umri wa miaka 32 ni afisa wa Jeshi la Ukombozi wa umma la China mjini Benxi. Mara baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea mkoani Sichuan tarehe 12, Mei mwaka 2008, Jia Xiaodong alituma Yuan elfu 2 kwa watu walioathiriwa na tetemeko hili. Baadaye Jia alipata habari kuwa Benki ya Akiba ya Posta ya China ilizindua kampeni ya kuchanga pesa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo, na Jia aliitikia wito wa kampeni hiyo.

    Baada ya kampeni hiyo, Jia alikumbuka anwani na jina la mtoto mmoja aliyeathiriwa na tetemeko hilo, na hadi leo anaendelea kumtumia yuan 100 kila mwezi kwa njia ya posta.

    "Wakati ule, sikutaka ajue ni nani anayemtumia pesa, nilimsaidia kwa dhati, huenda nguvu yangu ni dhaifu, lakini ni lazima nifanye vitendo halisi vya kuwasaidia wengine."

    Kila ifikapo mwishoni mwa mwezi, Xiaodong alionekana katika Benki ya Akiba ya Posta ya China huko Benxi akituma pesa.

    Siku hadi siku wafanyakazi wa benki hiyo wakamfahamu kijana huyo. Li Yao mwenye umri wa miaka 25 ni mfanyakazi katika benki hiyo, na alikuwa akimsaidia mara nyingi kutuma pesa hizo. Bw. Jia anasema.

    "Li Yao aliniuliza natuma pesa kwa jamaa yangu au la, na nilipomwambia namtumia mtoto aliyeathiriwa na tetemeko la ardhi, alishangaa sana, na aliona mimi ni mtu mwenye moyo safi na huruma."

    Jia Xiaodong anasema baadhi ya wakati akiwa anatekeleza jukumu katika mji mwingine, huwa anashindwa kutuma pesa hizo. Lakini anakumbuka aliposhindwa kutuma pesa mara mbili alipokuwa nje ya mji, aliporudi alitambua kuna mtu ambaye alikuwa amemsaidia kumtumia pesa mtoto huyo.

    "Huwa natuma pesa kati ya tarehe 28 hadi 30 kila mwezi, nikichelewa kutuma na nikifika benki, ataniambia ameshatuma. Baada ya mara hizo mbili, nikaona yeye ni mtu mzuri na mwenye moyo mweupe."

    Mtu aliyemsaidia kutuma pesa ni Li Yao. Li Yao anasema: "Naona kitendo chake hicho kinastahili kusifiwa, nilivutiwa sana. Baadaye nilijua yeye ni mwanajeshi, anaweza kuja kutuma pesa, isipokuwa wakati anapotekeleza jukumu nje au anapokuwa na kazi ya dharura. Asipokuja hakika ana shughuli, hivyo namsaidia kumtumia, pesa mtoto huyo, sipendi upendo wake ukwamishwe na kazi yake, hivyo namsaidia kuendelea kutoa upendo wake huo kwa mtoto huyo aliyeathirika na maafa ya tetemeko la ardhi."

    Kitendo cha Li Yao pia kiligusa hisia za Xiaodong, na akaona huu ni mwanzo wa mapenzi kati yake na Li, lakini Li Yao anasema wakati ule kitu alichotarajia ni kuiendeleza shughuli hiyo muhimu, kwani kitendo cha Xiaodong pia kiligusa hisia za watu wengine.

    Mwezik Novemba Mwaka 2011, Xiaodong alisafiri kikazi Chengdu, Sichuan, na baada ya kumaliza kazi, alitaka kujua hali ya mtoto Yuwei ambaye amekuwa akimfadhili kwa miaka miwili, ikoje.

    Hivyo alikwenda Mianyang, mji uliopo kilomita 200 kutoka Chengdu. Yuwei alikuwa shuleni, hivyo Xiaodong alimsubiri nje.

    Baada ya kutoka darasani, Xiaodong alikutana na Yuwei, lakini alidhani labda kumtembelea Yuwei kutasumbua maisha yake. Na hakutaka jambo hili litokee. Anatarajia kamwe Yuwei hatajua ni nani anayemsaidia.

    "Nikiwa katika treni nikirudi Benxi, nilishindwa kulala, kwani nilisisimka nilipofikiri kuwa nitaonana na Li Yao na kumwambia hali ya msichana Yu Wei tunayemfadhili."

    Baada ya kuwasili Benxi, Xiaodong hakuchelewa kuonana na Li Yao, na Li pia alivutiwa na hisia yake ya kusisimua, na alijivunia sana kutokana na kumsaidia msichana Yu Wei na kuendeleza upendo wa Xiaodong.

    Uhusiano kati ya vijana hao wawili wenye fikra zinazofanana unazidi siku hadi siku kutokana na kuelewana zaidi. Xiaodong anaona Li Yao ndiye msichana anayemfaa, hivyo Xiaodong aliamua kuonyesha mapenzi yake kwa Li Yao.

    Li Yao alimchukulia Xiaodong kama kaka yake mkubwa na hakutarajia iko siku watafunga ndoa. Lakini tatizo halisi lililowakabili vijana hao ni kuwa wanaishi katika miji tofauti. Akiwa mtoto pekee kwa wazazi wake, Xiaodong anatakiwa kurudi Shenyang baada ya kumaliza muda wake jeshini, na wazazi wake walimkutanisha Xiaodong na wasichana wengi wa Shenyang. Vilevile Li Yao akiwa binti pekee, wazazi wake wanatarajia aishi pamoja nao. Wazazi wa Li Yao walipojua kuwa atahamia Shenyang hawakusema kitu, lakini walisikitika kidogo. Hata hivyo wazazi hao waliposikia hadithi kuhusu jinsi vijana hao walivyofahamiana na kupendana walionyesha kidole gumba.

    "Uungwana wake na moyo wake wenye huruma vimenivutia sana. Wakati ule wazazi wangu walikuwa na wasiwasi kuhusu kazi yangu na tatozo la kuishi katika miji tofauti, lakini baada ya kuambiwa kuwa Xiaodong alimtumia pesa mtoto aliyeathiriwa na maafa ya tetemeko, na kuona kuwa yeye ni mtu mwenye moyo mweupe, mama yangu alituunga mkono."

    Katika majira ya mpukutiko ambapo mavuno yanapatikana, mapenzi yao yamezaa matunda. Xiaodong na Li Yao waliandaa harusi isiyo ya kawaida, kwamba hawakutumia magari yoyote, bibi harusi alivaa veli na bwana harusi alivaa sare ya kijeshi, wakiongozana na marafiki na ndugu zao kwenda sehemu iliyofanyika harusi yao kwa kutumia subway, huku Xiaodong na marafiki zake kutoka jeshini waliimba wimbo uitwao: "Tazama, sisi askari wa jeshini!".

    Baada ya kusikia hadithi ya jinsi wanandoa hao walivyokutana na kumsaidia msichana aliyeathiriwa na maafa ya tetemeko la ardhi, baadaye wakapendana na kuoana, watu walioshiriki katika harusi yao walitiwa moyo na wengi wakatoa pesa kwenye sanduku la michango kwa ajili ya kumsaidia mtoto Yu Wei.

    Harusi ilimalizika, lakini hadithi yao ya upendo itaendelea. Xiaodong anasema watamtumia mtoto Yuwei pesa walizochanga marafiki zao na baadhi ya pesa walizozawadiwa kwenye harusi.

    Xiaodong anasema Yuwei anasoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari na wanatarajia kuendelea kumsaidia hadi ahitimu masomo katika chuo kikuu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako