• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wasichana wa Maolan wanaosuka mwanzi

    (GMT+08:00) 2012-02-18 18:02:28

    Hifadhi ya Msitu wa Kikarst iko katika tarafa ya Maolan, wilayani Libo, mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China. Mwaka 2007, hifadhi hiyo iliwekwa katika Orodha ya Urithi wa Dunia. Katika hifadhi hiyo, kuna shirika moja la utengenezaji wa sanaa ya mwanzi, ambapo wasichana wanaweza kutumia mwanzi wenye thamani ya yuan 10, na kuubadilisha kuwa kitu cha sanaa ambacho kinaweza kuuzwa kwa yuan elfu 4 hadi 5.

    Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa Hifadhi ya Maolan Bw. Ran Jingcheng anaeleza sababu ya kuendeleza shughuli za utengenezaji wa sanaa hiyo. Anasema, "Katika hifadhi hii, kuna aina nyingi sana za mianzi, kwani mianzi ina uhai mkubwa, hivyo inaweza kutumika kwa mambo mbalimbali. Tulipeleka baadhi ya wasichana wanaopenda kazi ya kusuka vyombo vya mianzi kutoka hifadhi yetu kwenda kujifunza ustadi wa kutengeneza sanaa hiyo mkoani Sichuan, tuliwalipia nauli na ada za shule."

    Yao Youfeng, msichana mmoja wa kabila la Wabuyi ni mmoja kati ya wasichana waliopelekwa kusomea fani hiyo na idara ya usimamizi wa hifadhi hiyo. Yeye pamoja na watu wengine wapatao 200 wanaishi katika sehemu ya katikati ya Hifadhi ya Maolan. Kwa mujibu wa kanuni husika, miti katika msitu huu inalindwa kisheria. Vijana wengi kutoka eneo hilo wanakwenda mijini kutafuta kazi, lakini kwa Yao Youfeng haikuwa hivyo. Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari, Yao Youfeng anayetoka familia yenye hali duni ya kiuchumi alitarajia kuanza kazi mara moja. Yao anasema 'Mwaka 2008 nilimaliza masomo ya sekondari. Baada ya kurudi nyumbani, nilisikia kuwa idara ya usimamizi wa hifadhi ya msitu ilikuwa inatarajia kupeleka baadhi ya watu kutoka tarafa yetu kwenda Sichuan kujifunza kufuma mwanzi, hivyo nilikwenda kujiandikisha.'

    Baada ya kumaliza mafunzo yaliyodumu kwa siku 45, wasichana hao walirudi nyumbani kwao Libo. Kama walivyoona viongozi wa idara ya usimamizi wa hifadhi hiyo, wasichana hao pia wana imani na mustakabali wa sanaa ya mwanzi, kwani biashara hii haihitaji mtaji.  Yao anasema 'Tulinunua mianzi kutoka kwa wakulima, mwanzi mmoja unauzwa yuan 10, lakini tunaweza kupata maelfu ya yuan baada ya kuutumia kwa kutengeneza sanaa ya picha moja."

    Hata hivyo, kufuma mwanzi sio kazi rahisi. Yao Youfeng anasema kuna utaratibu maalum wa kufuata wakati wa kutumia mwanzi kutengeneza vyombo au sanaa za picha, na pia kuna vigezo vya kiufundi. Yao anasema,"Mianzi tunayochagua inatoka eneo la mlima Maolan wa Kikarst, tunaikata, kupunguza rangi ya kijani iliyo nayo na kutia rangi nyingine, baadaye tunauwekea dawa ya kuukinga na vijidudu na kutooza. Huwa inachukua wiki moja kumaliza picha moja ya mwanzi, na picha moja inakamilishwa na mtu mmoja peke yake kuanzia mwanzo hadi mwisho."

    Yao Youfeng ni msichana mwenye usitadi zaidi miongoni mwa wasichana hao. Hata hivyo, Yeye na wenzake hawaridhiki na kipato kinachotokana na kusuka vyombo vya mwanzi, wanatarajia kuwa na biashara kubwa. Yao anasema, "kutokana na sera iliyowekwa na serikali ya kuwasaidia wakulima kuanzisha shughuli zao ili kujiendeleza, shirika la ushirikiano wa wakulima linaweza kusamehewa kodi, hivyo tulikwenda idara ya viwanda na biashara kusajili shirika letu"

    Wasichana sita wenye umri usiozidi miaka 20 walianzisha biashara ya sanaa ya vyombo vilivyosukwa kwa mianzi Waliona kama wakifanya biashara vijijini, hawatawalazimu kukimbilia mikoa mingine kutafuta kazi, lakini haikuwa rahisi kuanzisha biashara hiyo.

    Idara ya usimamizi wa hifadhi ya Maolan imekuwa ikitoa msaada mwingi kwa shirika hili. Ofisa wa mradi wa ofisi ya jamii na maendeleo ya idara hiyo Bw. Zhang Yanquan anasema, "Tunawafuatilia sana. Tuliwatafutia sehemu wanayoweza kuitumia kusuka vyombo vya mianzi bila gharama yoyote, hiyo inawasaidia kuchangia mitaji inayohitajika kuanzisha biashara yao. vilevile tuliwasiliana na idara husika wilayani kuomba msaada wa kifedha, na sasa biashara yao inaendelea vizuri."

    Yao Shefeng ni mkuu wa shirika hilo. Mbali na kufuma mwanzi, yeye na wasichana wengine pia wanaandaa mafunzo ili wasichana wengine waweze kupata ufundi huo. Akikumbuka hali ilivyokuwa wakati wanaanzisha biashara hiyo miaka mitatu iliyopita, Yao Youfeng anasema, "Mwaka 2009 hatukupata faida yoyote, na tuliwahi kufikiri kuacha, lakini tuliona sanaa hiyo ina mustakabali mzuri, hivyo tumefanya juhudi zaidi."

    Yao Youfeng anasema kwa sasa wanapata oda kutoka kwa kituo kimoja cha sanaa ya mwanzi mkoani Sichuan, na vitu vya sanaa ya mwanzi walivyotengeneza huwa vinauzwa nchi za nje. Yao anasema "Tunajua ufundi tu, soko na biashara hatuelewi sana. Katika siku za baadaye, tunatarajia kujenga kituo cha sanaa ya mwanzi katika hifadhi hiyo, na kuajiri nguvukazi ya ziada ili sote tujiendeleze na kupata manufaa. "

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako