• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sauti ya Radio yasikika daima

    (GMT+08:00) 2012-03-05 17:57:05

    Katiku siku za zamani, huenda redio ilikuwa ndio njia muhimu ya mawasiliano. Redio iligusia nyanja mbalimbali za maisha, kutoka usafiri wa baharini na angani, pamoja na kutoa habari, burudani na elimu. Mfumo huo wa mawasiliano kati ya mtu na mtu ulifungua dunia ya mawasiliano kati ya mtangazaji na msikilizaji.

    Tarehe 13, Februari mwaka huu ilikuwa "Siku ya Redio Duniani", siku ambayo ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ili kusherehekea matangazo ya redio, kuongeza ushirikiano wa kimataifa kati ya vituo vya redio, na kuwahamasisha watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi kutoa maoni na mapendekezo kwa kupitia redio, ikiwemo redio za kijamii. Kwa mujibu wa Andrea Cairola, mshauri wa UNESCO kwenye sekta ya upashanaji habari na mawasiliano, redio bado ni chombo kinachoweza kuwafikia watu wengi zaidi.

    "Katika miaka 100 ya zama za hivi sasa, redio bado ni moja kati ya vyombo vya habari vya umma kinachoweza kuwafikia watu wengi, hasa katika sehemu nyingi za mbali. Kwa mujibu wa takwimu, redio inaweza kuwafikia kwa uchache asilimia 95 ya watu duniani, na barani Afrika, karibu asilimia 80 ya familia zina redio moja inayofanya kazi."

    Redio imechukua nafasi muhimu katika historia ya hivi karibuni ya binadamu, na iliwahi kutumika kwa ajili ya kutangaza hali ya dharura na kuokoa maafa, hata viongozi wa nchi mbalimbali wanaitumia kutoa habari. Wakati uchumi wa Marekani ulipodidimia na nchi yake kukumbwa na Vita vya Pili vya Dunia, rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt atoa mlolongo wa vipindi 30 ya redio kuwahutubia wananchi wake na kuwahakikishia kuwa nchi hiyo itarudi katika hali yake ya awali, na pia aliwapa moyo kwa kuwataarifu mipango ya nchi hiyo, baadaye hotuba hizo alizotoa Roosevelt ziliitwa "fireside chats".

    Kwa miongo kadhaa iliyopita, matangazo ya redio yamekuwa yanathaminiwa nchini China. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, familia moja ilitarajia kupata vitu vinne, yaani baiskeli, saa ya mikononi, mashine ya kushona nguo pamoja na redio, hivyo watu wa kizazi kimoja walikuwa wakisikiliza redio. Wang Hui mwenye umri wa miaka 40 hivi ni mmoja wao, na anakumbuka wakati watu walipokuwa wakisikiliza redio, anasema,

    "Nakumbuka wakati vipindi vya muziki vilipoanza kusikika, tuliweza kusikia nyimbo nyingi nzuri kwenye redio. Kuomba wimbo kwa mtu unayempenda kupitia redio kweli ilikuwa ni jambo la kisasa wakati ule. Nakumbuka nilipokuwa chuoni, msimamizi wa idara yetu alikuwa anapendwa na watu wengi, na tuliwahi kutumia pesa kumwombea wimbo mmoja kwenye redio."

    Hata hivyo, kutokana na kugunduliwa kwa televisheni na baadaye internet, athari ya redio imepungua, ambapo si rahisi kuona redio katika familia za mijini kwa hivi sasa, je, bado kuna watu walio na tabia ya kusikiliza redio?

    "Hivi sasa? Hapana kabisa."

    "Ndiyo, inategemea mahali nilipo. Nikiwa Nyumbani, sisikilizi redio, ninapoendesha gari nasikiliza, ninapokuwa shuleni, nasikiliza redio kwenye mtandao wa internet."

    "nasikiliza redio, tunapotoa mafunzo kupitia elimu ya mbali, tunahitaji redio hasa kwa sehemu za vijijini na zile za mbali."

    Qu Zhi ni shabiki mkubwa wa redio. Anatumia "walkie-talkie" kusikiliza redio kila anapopata nafasi.

    "Kitu kinachonivutia zaidi ni kuwa chombo kinachotumika kusikiliza redio ni rahisi, vilevile redio inasikika kwa utulivu hasa katika hali ya dharura. Kwa mfano, tetemeko la ardhi lilipoikumba Wenchuan, China mwaka 2008, karibu nyaya zote za simu, kebo zilizotumika kwa mawasiliano na minara ya simu viliharibika, hivyo redio ni chombo pekee kilichoweza kutumika kutoa habari zinazohusu sehemu zilizokumbwa na maafa.

    Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa njia zinazotumika kusikiliza vipindi vya redio, baadhi ya njia za kufikisha matangazo ya radio ziko hatarini kutoweka. Kwa mfano, baadhi ya vituo vya redio vimeacha kurusha matangazao yake kupitia masafa mafupi na kuchagua mtandao wa internet kutokana na gharama. Kwa mujibu wa daktari Javad Mottaghi, katibu mkuu wa Umoja wa redio wa Asia-Pasifiki, anasema pamoja na mazingira hayo, huduma za redio bado ni maarufu duniani. Akisema,

    "Mkondo wa sasa ni baadhi ya radio kupunguza matangazo yake ya masafa mafupi, mimi naona baadhi ya vituo vilivyofanya hivyo vimeanza kujipanga upya kutoa matangazo yake kupitia masafa mafupi. Bila shaka, baadhi yao viliacha kabisa matangazo ya masafa mafupi na sasa vinajaribu kurusha matangazo yao kwenye mtandao wa internet."

    Huduma za matangazo ya redio zinapaswa kulingana na teknolojia mpya na zana, ambazo zinatumia vyombo vya habari vya aina mpya, kama vile mtandao wa intener, simu za mkononi na tablet. Lakini bila kujali njia gani inayotumika kurusha matangazo, redio inazidi kupata maendeleo, na kuhifadhi kumbukumbu za hatua zilizopigwa kupitia mawimbi yake na mikondo yake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako