Jumuiya ya kimataifa imelaani vikali mapinduzi ya serikali yaliyofanywa na jeshi la Mali jumatano wiki hii.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, jana ametoa taarifa akilaani mapinduzi hayo, pia ametoa mwito wa kurudisha utawala wa katiba nchini Mali.
Marekani jana imetangaza kumuunga mkono rais wa Mali aliyepinduliwa Amadou Toumany Toure.
Nayo Ufaransa imesitisha ushirikiano wote wa kiserikali na Mali, lakini itaendelea kutoa msaada kwa wananchi, hasa wa nafaka.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Hong Lei leo hapa Beijing amesema China inapinga kutwaa madaraka kwa nguvu na kukiuka katiba, na imezitaka pande husika nchini Mali zirudishe utaratibu wa kawaida, na kulinda mshikamano na utulivu wa nchi hiyo kwa ajili ya maslahi ya kimsingi ya nchi hiyo na wananchi wake.
Umoja wa Afrika umetoa taarifa ya kulaani vikali mapinduzi hayo, na kusema yameharibu utaratibu wa demokrasia nchini Mali na kurudisha nyuma maendeleo ya demokrasia katika bara la Afrika. Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Bw Jean Ping amewataka waasi wajisalimishe.
Mapinduzi hayo pia yamelaaniwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS. Jumuiya hiyo imesema inalaani kitendo cha kupindua serikali iliyochaguliwa kihalali, huku muda mchache ukiwa umebaki kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Mali, na kwamba waasi hao wamejitenga wenyewe kutoka ECOWAS.
Wakati huohuo, kamati ya ustawi wa demokrasia na ukarabati wa taifa iliyoundwa na waasi wa Mali jana imetoa taarifa ya kufunga mipaka na anga ya nchi hiyo.
Msemaji wa kamati hiyo Bw. Amadou Konare amesema, kazi za serikali zitarejea katika utaratibu wa kawaida tarehe 27 mwezi Machi, na watumishi ambao hawataripoti katika sehemu zao za kazi watakuwa wamejiachisha kazi wenyewe.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |