• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0522

    (GMT+08:00) 2012-06-06 16:19:50
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi wa Eveready Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anaanza kwa kusema sioni sababu inayoweza kunizuia kuzimimina pongezi nyingi na vilevile shukrani zangu za dhati kwa CRI. Hii ni kutokana na kupokea kitabu kidogo kilicho na picha murua zenye maelezo mafupi. Kwenye kitabu hiki ukurasa wa kwanza kuna maelezo kuhusu kuanzishwa kwa CRI ambacho ni chombo pekee kinachotangaza kwa lugha nyingi kote duniani.

    Ukurasa wa pili nao umewekwa picha maridadi yenye mvuto wa kupendeza ambapo wafanyakazi wa CRI wamesimama mbele ya jengo la CRI na pembeni yao mama Chen, mama mwenye kipaji kikubwa cha utangazaji na kawaida yake hupenda kutabasamu kwa furaha. Nikipekuwa ukurasa wa tatu namuona mkurugenzi mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI Bibi Han Mei akiwa amesimama karibu sana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na kushoto kwake kuna kijana ambaye amesheheni na kunawiri katika anga za utangazaji Bw. Fadhili Mpunji ambaye kwa miaka na miaka sauti yake imekuwa ikivutia wasikilizaji wengi.

    Ninapomulika jicho langu kwenye ukurasa wa nne nawaona mama Chen akitabasamu na Bw. Fadhili Mpunji akisoma habari studio na ninapofungua ukurasa wa nane na tisa denda linanitoka huku nukitamani ningelikuwa mimi nimeketi na mama Chen kwani namuona msikilizaji mwenzangu Bwana Mutanda Ayubu na Ras Manko Ngogo, pembeni au mbele yao meza imepangwa na kupambwa huku vifuani mwao yakipachikwa mashada ya maua, naye Bwana Stephen Magoye Kumalija akiwa kwenye mnara akiutazama mji wa Shanghai, ambapo Bibi Jane Shirima akiwa kwenye uwanja wa Tianamen Square wa Beijing, Bwana Mbarouk Msabaha anaonekana kwenye picha akitembelea jumba la maonesho la Afrika. Natamani siku moja mguu wangu utue kwenye ardhi ya China.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi kwa barua yako ya shukurani kuhusu kitabu ulichopokea, tunajua kwamba unatamani kuja China kutembelea siku moja na hilo sio wewe tu bali wasikilizaji wetu wote, ndio maana huwa tunatumia njia mbalimbali kuhakikisha wasikilizaji nao wanakuja China ikiwemo chemsha bongo, hivyo kama kweli una nia, jitahidi maradufu zaidi tutakapotoa maswali ya Chemshabongo, ahsante sana.

    Naye Bw. Gulamu Haji Karim wa S.L.P 504 Lindi Tanzania anasema natumai hamjambo, mimi kwa upande wangu kazi moja tu ni jioni saa moja redio mkononi nasikiliza CRI. Tarehe 3 mwezi wa nne mwaka huu nilisikia barua yangu ikisomwa, msikilizaji akisikia barua yake ikisomwa anahamasika kuandika nyingine zisomwe barua nyingi kwa kadiri ya muda wote.

    Pendekezo langu ni kubadilisha muda wa matangazo badala ya kuanza saa 1-2 jioni yaanze saa 10 mpaka 11 jioni kwani muda huo wengi wetu tunakuwa nyumbani, tusharudi kazini naomba wasikilizaji wenzangu pia watoe maoni yao juu ya muda huu. Ahsante.

    Shukrani nyingi sana Bw. Gulamu Haji Karim kwa barua yako fupi, lakini kukujibu pendekezo lako kuhusu kubadilisha muda, kwakweli tumeshafanya mabadiliko kwani awali ilikuwa saa 4-5 usiku na sasa tumerudisha kati ya saa 3-4 usiku kwani muda huo ni mzuri kwa kila mtu, kwasababu wengi wanakuwa wamerudi nyumbani na kupumzika lakini saa 10 jioni watu wengi sana wanakuwa hawajarudi kwenye shughuli zao za kila siku, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako