• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0612

    (GMT+08:00) 2012-07-18 16:22:23
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Dushime Dominique wa S.L.P 105 Makamba Burundi, anaaanza kwa kusema ndungu watangazaji, Salaam nyingi kutoka kwangu. Nataka nawajulishe kama selikali ya China inasaidia sana nchi yetu ya Burundi katika miradi mbalimbali: kama vile Kujenga barabara, hospitali, mabwawa ya maji na ya umeme, chuo kikuu cha walimu na vingine vingi. Tena China ilitowa msada wa ndenge kubwa sana katika shirika la ndege la Burundi Air Burundi, tena wakatowa nyingine kwa mkopo; wafanya biashara kutoka China ni wengi sana hapa Burundi. Tena wanafundisha watoto mchezo wa sarakasi na matayarisho tafauti ambayo yataoneshwa wakati Burundi itakapotizimisha miaka 50 ya uhuru kutoka kwa wa Ubelgiji (Belgium), tarehe 1/ 7 / 2012.

    Naomba Radio China idhaa ya Kiswahili itume watangazaji wake katika sikukuu hiyo, tena itakuwa ni furaha kwetu wasikirizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio China. Nataka niwajulishe kama hivi karibuni nina niya ya kuanzisha Club ya Kiswahili Radio China hapa Burundi japo tunaipata kwa taabu saana. Tena nataka niwakumbushe kama mliniahadi kunitumiya kalender na programa za Radio China hadi sasa hazijanifikiya. Nataka kuwaahidi kama nitakuwa nawatumiya habari mbalimbali kuhusu China na Burundi. Asanteni sana. Radio China idumu milele.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Dushime Dominique kwa barua yako, kwa kweli tunafurahishwa sana na moyo wako wa kujitolea wa kutaka kuanzisha klabu ya wasikilizaji huko Burundi, na kuhusu kalenda tutajitahidi kukutumia ila hatuwezi kukuahidi moja kwa moja khusu kuleta watangazi kwenye sherehe hizo za tarehe mosi july, kwani shughuli kama hiyo inahitaji matayarisho ya muda mrefu. Ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Yohana Marwa mwenye baruapepe marwa.yohana@yahoo.com, anasema napenda kutumia nafasi hii kwa mara nyingine kuwapa pongezi kwa umahiri mkubwa wa kutoa habari zenye msimamo ambao hautetereki hata bila uoga wa kutamka, kwa sababu daima mpo kwenye mstari. Naandika maoni haya kutokana na kusikiliza kipindi cha Sanduku la Barua kilichoenda hewani tarehe 22/05/2021 ambapo msikilizaji alitoa maoni ya kurudishwa nyuma matangazo kutoka saa 19:00 pm hadi saa 16:00 jioni.

    Kama yeye mwenyewe alivyo sema kwamba na sisi tutoe maoni natumia nafasi hii kusema kuwa, kama alivyosema mama Chen kuwa hana uhakika kama itawezekana kwa kweli huo muda haitakuwa vizuri kwani bado huwa ni muda wa kazi hivyo basi napenda kuungana na mama chen kuwa muda ubakie pelepale kama ilivyo sasa. Mwisho nawatakia kazi njema na yenye mafanikio zaidi ili mwendelee kutuletea habari za uhakika ambayo yananifanya niendelee kujivunia idhaa hii ya kiswahili ya CRI kama idhaa yangu mama.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Yohana Marwa kwa barua yako, pia tunapokea pongezi kwa mikono miwili na tunakuomba uendelee kusikiliza zaidi matangazo yetu na kututumia maoni na mapendekezo yako kuhusu matangazo yetu kwa ujumla. Ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya, anasema kwanza salamu zangu ziwafikie wasimamizi wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa. Pia naomba kuwajulisha ya kwamba sikosi kusikiliza vipindi na matamgazo ya idhaa ya Kiswahili ya CRI kila siku, licha ya matangazo na vipindi vingi, kipindi cha kuwa nasi jifunze kichina kimenipa moyo sana katika hali ya kujifunza kuongea na kutamka maneno ya kichina.

    Ingawa nimekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kuzidiwa na shughuli za ujenzi wa taifa sikosi kusikiliza matangazo na vipindi vya CRI, shukran za dhati ziwafikie watangazaji na wasimamizi wa idhaa ya kiswahili ya redio China kimataifa sisi wasikilizaji tunazidi kufurahishwa na jinsi mlivyoboresha vipindi na matangazo. Mbali na hayo kipindi kipya cha studio ya jifunze kichina. Mwisho pongezi zangu ziwaendee wasimamizi na watangazaji wa shirika la utangazaji la Kenya KBC kwa kuwa na mwamko mpya ambapo shirika hilo hivi sasa linajulikana kama "KBC redio taifa, sauti ya mkenya"

    Nasi tunakushukuru sana msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie kwa barua yako, pia tumenafurahi kuona wasikilizaji wetu wanaridhishwa na mbadiliko na uboreshaji wa vipindi vyetu, kwani hilo ndio lengo hasa kuwafurahisha wote. Tunakuomba tu uendele kusikiliza matangazo na kutoa maoni zaidi, ahsante sana.

    Barua ya mwisho inatoka kwa Msikilizaji wetu Mwita Mwita Omahe wa S.L.P 376 Tarime Mara Tanzania anasema ninapenda kutanguliza salamu zangu za dhati kwenu watangazaji wote wa redio China kimataifa, na kama nyote ni wazima kiafya na kikazi ni bora kwani ni furaha kubwa kwetu wasikilizaji kwa upande wangu ni mzima wa afya njema.

    Lengo kubwa la kuandika barua hii ni kutaka kujiunga na kuwa mmoja wa wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya redio China. Mimi binafsi nimeshawishika kujiunga na idhaa hii kutokana na rafiki yangu Emma Mseti ambaye yeye vilevile ni msikilizaji na mfuatiliaji wa vipindi vya redio China, hivyo najisikia mpweke pale mwenzangu anapokuwa anafanya jambo na mimi nikiwa pembeni bila ya kujishughulisha.

    Hivyo leo hii nimeamua kuichagua CRI kuwa msikilizaji wake. Na kikubwa kinachonifanya niipende redio hii ni kile kipindi chake cha salamu zenu, na mimi napenda kuwa mmoja wa watuma salamu, hivyo naomba mnitumie kadi kwa wingi, ili niweze kuwakumbuka ndugu na marafiki kupitia idhaa ya Kiswahili ya CRI na bila kusahau chemsha bongo.

    Shukran nyingi msikilizaji wetu Mwita Mwita Omahe kwa barua yako. Ombi lako tumelipokea na tayari tumeshakuorodhesha kwenye majina ya wanachama wetu, kuhusu kadi pia tutakutumia, ila tunakuomba usikilize zaidi matangazo yetu ili uweze kutoa maoni yako. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako