• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0619

    (GMT+08:00) 2012-07-18 16:23:00
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Ngaillo Patrick wa Chuo Kikuu Kishiriki cha SEBAS anasema nashukuru kwa maoni ya kukipa kiswahili umuhimu wake katika kuendeleza utamaduni. Ninachoomba ni kutengeneza sera ya lugha inayojitegemea yaani ile ambayo haitakuwa ndani ya sera ya Utamaduni. Hii itakifanya kiswahili kukua zaidi na kukifanya kiweze kutumika kufundishia hadi elimu ya juu badala ya kiingereza ambacho wanafunzi wetu wanateseka na kufeli kwa sababu ya ugumu wa lugha. Kumekuwa na matamko mbalimbali yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali kwa nyakati tofauti ya kusema mipango itafanywa kukifanya kiswahili kitumike kufundishia elimu ya juu lakini utekelezaji umekuwa hakuna. Mfano ni katika sera ya lugha ya 1997 inasema hivyo lakini utekelezaji wake haujafanyika mpaka sasa.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Ngaillo Patrick kwa barua yako, kwakweli Kiswahili hivi sasa kinashika kasi katika Afrika hata duniani, hivyo tunaona ni busara kuifanya lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu, kwani hiyo ni njia moja ya kukiendeleza, mfano hapa China lugha inayotumika kufundishia ni kichina na si lugha nyingine, pia kichina kinatumika kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali kwani pia ni lugha rasmi. Ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Yohana Magaigwa wa klabu ya Kemogemba S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania, anasema ni matumaini yangu kuwa wote ni wazima wa afya njema na mnaendelea kuchapa kazi kwa bidii ya kutuletea matangazo yenu ya Kiswahili siku hadi siku, nawaombea kwa Mungu awazidishie moyo wa upendo katika kazi yenu nzuri mnayoifanya.

    CRI ni redio ya uhakika isiyo na ubabaishaji, sifa hiyo iwafikie popote mlipo wafanyakazi wote wa CRI, nimevutiwa na kuamua kutamka waziwazi kuwa mnastahili pongezi zote kutokana na juhudi zenu za kuimarisha matangazo kwani siku hadi siku tunaendelea kunufaika na vipindi vyenu.. napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa kutimiza miaka 50 ya kuanzishwa kwa matangazo ya idhaa ya Kiswahili, na naweza kusema bila kusita kuwa CRI ni mzee kijana ambaye hataki kujiona anabaki nyuma bali kusonga mbele kwa kasi ya ajabu sana.

    Baada ya kusema hayo sasa nauomba uongozi kuboresha matangazo yale ya saa moja jioni yasikike kwa njia nzuri, kwani huwa na mwingiliano wa mawimbi ya stesheni nyingine, ili tuendelee kuyafurahia zaidi bila kuyumba yumba kama ilivyo sasa. Mwisho nawatakia heri ya mwaka mpya wa jadi wa China, uwe ni mwaka wenye mafanikio na baraka zake Mungu kwa watu wote wa China pamoja nasi wasikilizaji wenu, tuko pamoja.

    Shukran nyingi msikilizaji wetu Yohana Magaigwa kwa barua yako, kuhusu usikivu wa matangazo yetu ya saa moja jioni tutajitahidi ili kuhakikisha yanapatikana bila shida yoyote, pia tunapokea pongezi kwa moyo wa dhati kabisa, kwani CRI idha ya Kiswahili ina lengo moja tu, ambalo ni kuwaridhisha na kuwashirikisha wasikilizaji wake kwenye matangazo yetu, ahsante sana.

    Bw. Mogire Machuki wa S.L.P 646 Bogeka Village, Kisii Kenya anasema

    Salamu za kila la kheri kutoka hapa kisii Kenya nikiwa na matumaini kuwa hali shwari kabisa huko Beijing. Pili ni furaha kuwa hapa leo kwenye tovuti nimefanikiwa kuunganisha kipindi cha cheche zetu kutoka kwenye kompyuta na kuweza kusikika kwa sauti ya aina yake kote kwenye 'intaneti cafe'' hapa kila mtu anatabasamu. kweli DJ Moss anafanya kazi smati sana. hapa naona watu wanatikisha kichwa kwa kuendelea kusikiliza muziki wa aina yake. yavutia sana. niko hapa kutoka sasa na uongezee masaa matatu mbele

    Aidha nawaarifu CRI kuwa nimepokea zawadi yangu niliyoshinda kama zawadi ya kwanza kwenye shindano la ''xijiang through my Lens'' zawadi ni ya thamani sana na familia yangu yote na marafiki wameipenda sana. Asante sana kwa moyo wenu safi na Mungu aendelee kuiongezea CRI.. kwa sasa niko nyumbani kwa shughuli kama kawaida na matangazo naendelea kuyafurahia kwa njia ilio safi kabisa kupitia masafa mafupi ambapo siku hizi hali ya usikivu ni safi kabisa muda wote.

    Nawatakia kila lililo jema. Asante na udumu urafiki.

    Kwanza tunakushukuru sana msikilizaji wetu Mogire Machuki kwa barua yako, pia baada ya kumpa salamu DJ Moss, amefurahi na kuridhishwa na jinsi wasikilizaji wanavyomuunga mkono na kipindi cha cheche zetu, pia ameahidi kuleta mambo mzuri zaidi. Ahsante sana.

    Simba Suleiman Dunguzi wa S.L.P 452 Ukunda Mombasa Kenya naye anasema natumai barua hii imewapata mkiwa wazima. Jimbo la kwale matangazo ya CRI twayapata kwa njia mufti kabisa, kwanza ningependa kupongeza jopo zima la wakurugenzi, watangazaji, na wahudumu wote wa CRI kwa juhudi zao za kutuandalia wipindi vilivyo na mafunzo kedekede.

    Pili ningependa kuwajulisha kwamba bado naendelea kusikiza CRI licha ya kuwa kimya kwa miezi kadhaa. La mwisho ningependa kuanzisha klabu ya salamu ninachoomba toka kwenu mnitumie kadi za salamu na bahasha. Kando na kadi za salamu tafadhalini pia msikose kunitumia kitabu kilicho na picha na matukio mbalimbali ya CRI. Jarida la daraja la urafiki, kalenda na chochote ambacho mtakiona kina umuhimu kwangu.

    Nawatakia majukumu mema na Mungu awabariki na CRI idumu milele.

    Tungependa kukushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Simba Suleiman Dunguzi kwa barua yako, hongera sana kwa moyo wako wa kutaka kuanzisha klabu mpya ya salamu, nasi huku kwa kuonesha kukuunga mkono tutajitahidi kukutumia kadi za salamu na bahasha zilizolipwa ili kutoa urahisi zaidi kwa wanachama wa klabu hiyo, ahsante sana.

    Sasa tunawasomea ujumbe tuliotumiwa na wasikilizaji wetu kwanza ni Lydia msambweni anasema nafurahia kuhusu tamthilia ya doudou na ningependa iendelezwe.

    Epafra Stanley Deteba anuani yake ya babruapepe ni epst01@hotmail.com anasema matangazo yenu ni mazuri sana, ongezeni zaidi na zaidi kama kungekuwa na tuzo ya vyombo vya habari basi redio China kimataifa mngekuwa wa kwanza, ni dhahiri mko juu tena sana tu! safi sana CRI.

    Joseph Wangui wa Ruiru Kenya anasema napenda matangazo yenu yote hasa kipindi cha cheche zetu naye Dj Mos na pia salamu zenu. Pia mwatusaidia kujua mengi kuhusu nchi ya Uchina, watu wake na wanavyoishi na kuhusu lugha yao. Asante.

    Fadhili Kipene wa S.L.P 30 Nachingwea Hospital anasema wapenzi watangazaji na wasikilizaji wa radio China kimataifa mimi nimehama kituo changu cha kazi kwa sasa nafanya kazi Mtwara. Napenda sana kujua lugha ya kichina isipokua nna mambo mengi yanayonifanya nishindwe kujifunza.

    Tunawashukuru wasikilizaji wetu wote waliotutumia ujumbe kupitia tovuti yetu, ila tungependa kumjibu Lidya, kuwa tamthilia ya Mao Doudou na wakwe zake imeishia pale hivyo itakuwa vigumu kuindeleza, pia tunawaomba wasikilizaji wetu wote muendelee kusikiliza matangazo yetu na kututumia maoni na mapendekezo, Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako