• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0703

    (GMT+08:00) 2012-07-18 16:23:38
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Yaaqub Saidi wa S.L.P 792-50100 Kakamega Kenya anaanza kwa kusema nawapa mkono wa heri na fanaka watangazaji, viongozi na wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya CRI nikitaraji kuwa nyote mu wazima huku mkiendeleza shughuli za kutuhudumia kwa vipindi na matangazo.

    Zifuatazo ni sababu zinazonifanya niseme taifa la China ni bora kati ya mataifa mengi hapa ulimwenguni, sisi tunaishi katika nchi ambayo utamaduni wa kichina umeacha athari zake, nasi tunajivunia jambo hilo. China inastahiki kuungwa mkono na kushirikiana nayo kutokana na ushujaa wake wa kusimama kidete mbele ya siasa za magharibi katika wakati huu ambapo dunia inashuhudia ongezeko la joto. Katika kipindi cha muda mrefu China imeweza kupiga hatua kubwa na kuwa na nafasi muhimu katika nyanja zote na hilo wananchi wa China, Kenya na ulimwenguni kwa ujumla wanalijua vyema.

    Kwa mfano katika kipindi cha muda mrefu sasa China imefanikiwa kutuma satalait katika anga za juu jambo ambalo linaweza kufanywa na nchi chache tu duniani, aidha baada ya kupita miaka 30 imeweza kulitilia kasi sana suala la nyuklia ambayo nchi za magharibi zinageuza kuwa suala la kisiasa na kufanya kisingizio cha kutishia mataifa mengine, wakati ambapo Shirika la kimataifa la nishati ya Atomiki limeunga mkono mara nyingi shughuli za nyuklia za China likisema ni za amani na hazijaenda kinyume na sheria za kimataifa.

    Katika upande wa maendeleo ya viwanda China pia imewathibitishia walimwengu kuwa inaweza kujiletea maendeleo. Kwa kweli katika kipindi kirefu taifa la China limefungua miradi mbalimbali na kupata maendeleo makubwa katika mambo ya teknolojia ya kijeshi na sayansi. China pia imefanikiwa kuandaa mazingira ya kunawirisha maadili bora na hivi sasa vijana wanayajua vyema masuala ya kitaifa na kimataifa na wanajivunia kwa utamaduni wao wenye utajiri mkubwa. Mwisho nawaombea kila la heri watangazaji wafanyakazi na uongozi wote wa CRI. Ahsante sana.

    Kwanza tunapenda kukushukuru sana msikilizaji wetu Yaaqub Saidi kwa barua yako yenye maoni murua kabisa. Kwa kweli China hivi sasa imepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, na hivi majuzi tu imerusha chombo cha anga ya juu cha Shenzhou no 9 ambacho kimebeba wanaanga watatu akiwemo mwanamke mmoja, hayo ni mafanikio makubwa kwa China, isitoshe imejaribu kuandika historia kuwa China nayo imekuwa miongoni mwa nchi zenye wanaanga wanawake, Ahsante sana.

    Na sasa ni barua ya Claude Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania anasema natumai mu wazima wafanyakazi wote wa CRI Idhaa ya Kiswahili, na mimi ni mzima na naendelea na ujenzi wa taifa langu la Tanzania pamoja na kufuatilia kila siku matangazo ya CRI na kuwaandikia barua mara kwa mara redio hii niipendayo ya CRI.

    Kabla ya yote natumia fursa hii kuwapongeza wafanyakazi na wananchi wote wa China kwa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China ambapo katika mwaka huu wa 2012 unawakilishwa na mnyama Dragoni. Baada ya hayo nachukua fursa hii kuipongeza CRI kwa kutuletea habari nyingi na nzuri katika kipindi kizima cha mwaka uliopita wa 2011 ambapo na katika mwaka huu pia tunaiomba CRI iendelee kufanya hivyohivyo.

    Mwisho naishukuru CRI kwa kunitumia bahasha, kadi za salamu pamoja na jarida la CRI la Daraja la Urafiki ambapo limerejea tena baada ya kulikosa kipindi cha muda wa miaka sita iliyopita. Ahsanteni sana uongozi mzima wa CRI kweli sisi wasikilizaji wenu mnatujali na kutupenda sana.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Claude Magoye Kumalija kwa barua yako, kama lilivyo lengo la CRI hususan idhaa ya Kiswahili kwamba ni kuwaletea habari motomoto za dunia ambazo tunataraji kuwa zitawaridhisha na kuwaelimisha wasikilizaji wetu wote, hivyo usiwe na wasiwasi kwani mwaka huu tutajitahidi kufanya vizuri zaidi kuliko mwaka jana asante sana.

    Naye Yohana Marwa wa klabu ya Kemogemba. baruapepe yake ni marwa.yohana@yahoo.com anasema ni siku nyingi zimepita bila kuwaandikia barua lakini tuko pamoja kila matangazo ya CRI yanapokuwa hewani. moja ya vipindi vilivyonivutia sana ni kile cha China Machoni mwetu ambacho kilizungumuzia maisha ya waafrika waishio katika mji wa Guangzhou nilifurahia kipindi hicho sana. Naomba mwendelee na moyo huohuo ahsanteni sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Yohana Marwa kwa barua yako fupi, na tunapenda kukuahidi kuwa vipindi kuhusu mji wa Guanghzhou vitasikika zaidi katika miezi ya mbele, kwani tunapenda waafrika waufahamu mji wa Guangzhou ambao unaonekana kama ni Afrika ndogo ahsante sana.

    Choma wa Choma S.L.P 108 Mwamkulu Mpanda Tanzania naye anasema Asante sana CRI kwa kunitumia vitabu vya jifunze kichina kwa watoto wagu, sasa hawana tabu, natoa shukurani, na nitaendelea kuchangia CRI nataka mnitumie chemsha bongo na maswali, ili nami nishiriki kama wegine Asante radio China Kimataifa, watoto wamefurahi, kupata vitabu, hususan Magiled Choma, nataka nitowe shukurani. natamani kuiona Beijing China, karibuni Tanzania Mwamkulu Mpanda.

    Shukran za dhati Bwana Choma wa Choma kwa barua yako, nasi tumefurahi sana kuona vitabu hivyo unatumia pamoja na watoto, kwani kama tunavyofahamu kuwa mtoto ni rahisi zaidi kujifunza lugha kuliko mtu mzima, kuhusu maswali ya chemsha bongo tutakutumia pale tutakapotoa chemsha bongo mpya ahsate sana.

    Sasa tunawaletea ujumbe tuliotumiwa na wasikilizaji wetu kupitiakwenye mtandao wetu

    Msikilizaji wetu John mwenye baruapepe n3jajmc@yahoo.com anasema napenda kupata habari zenu nzuri, zina vutia.

    Naye Elias Msafiri baruapepe yake ni elias_msafiri@yahoo.co.uk anasema ni jambo zuri sana kwa serikali ya China kuendelea kudhamini wanafunzi wanaotaka kuja huko kusoma. Mimi ni miongoni mwa wanafunzi wanaopenda sana kusoma China lakini sijajua nifuate hatua gani ili niweze kufanikisha lengo langu. Naombeni msaada wenu.

    Msikilizaji wetu Daniel Khaoya Ngoya S.L.P 1674 Bungoma anasema ningependa kuwashukuru kwa zawadi mliyonitumia kwa njia ya posta. Namwomba Bi Han Mei siku moja anialike nije China kuitembelea CRI.

    Alhaj Ntungwabona wa baruapepe hntungwabona@yahoo.com naye anasema hongereni kwa kazi nzuri. Ninataka kutuma Swali langu, ingwawaje ni refu zaidi ya maneno 1000, nifanyeje?

    Naye Simba Suleiman Danguzi wa Ukunda, Mombasa Kenya. Anasema natumai hamna neno mjini Beijing. Nchini Kenya hatuna neno, naendelea kuyapata matangazo ya CRI kwa njia Mufti, Tafadhali nitumieni Kadi za salam, jarida la daraja, kitabu kidogo kilicho na picha za matukio mbalimbali ya CRI na kalenda

    Mwisho ni maoni kutoka kwa Masoud Khamis Hamed masoudkhamis07@gmail.com anaanza kwa kusema Ni hao, ni hao ma?

    Naitwa Masoud Khamis Hamed wa Zanzibar Tanzania, kiukweli radio ina matangazo mazuri lakini katika masafa ya short wave inakua tabu kupatikana hivyo tunaomba muungane na radio washirika wa hapa nchini ili iweze kuenea na kutoa faida kwa wote, pia katika blog yangu hii htt://zenjibarza.wordpress.com nimeweka anuani ya tovuti yenu ya CRI mtu akitembelea blog anaweza kuingia katika mtandao wa idhaa, tunaomba anuani ya barua pepe ya idhaa.

    Tunawashukuru wasikilizaji wetu wote mliotutumia maoni kupitia kwenye mtandao wetu, kwanza tunapenda kumjibu Elias Msafiri kwamba unachotakiwa kufanya ni kutafuta fomu ya chuo unachotaka kusoma ambacho kinatoa udhamini halafu unajaza na kutuma kwenye chuo hicho, kwani hapa China kuna vyuo vingi tu vinavyotoa udhamini wa masomo. Na kwa upande wako Daniel unachotakiwa kufanya ni kuambatanisha faili lenye hilo suali kwenye baruapepe yako, halafu ututumie kupitia anuani yetu ya baruapepe, Ahsanteni sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako