• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uteuzi wa kikosi cha Kenya kwenye Olimpiki

    (GMT+08:00) 2012-07-26 18:44:49

    Shangwe vifijo na nderemo vilitanda katika uwanja wa kimataifa wa nyayo jijini Nairobi wakati wa mashindano ya riadha ya kuteuliwa kwa kikosi kamili cha wanariadha watakaoiwakilisha Kenya kwenye mapambano ya Olimpiki yatakayoandaliwa London Uingereza kuanzia tarehe 27 Mwezi Juai Mwaka huu.

    Uteuzi huu uliwalazimu wanariadha wanaotaka kushiriki katika mbio za vitengo tofauti kukabiliana kufa kupona na wenzao kutoka hapa Kenya kabla ya kupata tiketi ya kuelekea Uingereza kwenye olimpiki ambayo ni ndoto ya kila mwanariadha kushiriki.

    Kabla ya siku hii, chama cha riadha nchini kilikuwa tayari kimewachagua wanariadha watakaiwakilisha Kenya kwenye mbio za masafa marefu yaani Marathon mita elfu 10.

    Kwa hivyo mashindano haya ya siku hii tarehe 23 Mwezi Juni yalikuwa ni ya mwisho ya kusaka tiketi ya olimpiki na ni wanariadha watatu pekee waliochukua katika kila kitengo cha mbio walizoshiriki.

    Kocha wa kikosi cha riadha nchini Kenya Julius Kirwa ameelezea kuwa kikosi chake kiko tayari kuandikisha matokeo mazuri kwenye olimpiki baada ya mazoezi na maandilizi ya kutosha.

    Ilikuwa ni siku ya wanariadha hawa kusaka nafasi ya mbio za mita 5000 wanaume na wanawake,mita 1500 ,mita elfu 3 na hatimae tiketi ya mita mia 8 kitengo ambacho kwa sasa ,Kenya imekitawala sana.

    Kinyanganyiro cha kwanza siku hii kilikuwa ni uteuzi wa wanariadha wa mita elfu tano.

    Baada ya kivumbi kikali kutoka kwa wanariadha hao bingwa wa dunia Vivian Cheruiyot ,Sally Jepkosgei na Viola Kibiwot walijikatia tiketi za kuiwakilisha Kenya upande wa wanawake baada ya kunyakuwa nafasi ya kanza ya pili na ya tatu mtawalia.

    Vivian Cheruiyot ambae ni bingwa dunia alieleza furaha yake ya kupata nafasi hiyo na kuahidi kushindia Kenya dhahabu kweye olimpiki.

    Yeye atawakilisha Kenya mara mbili kwenye mbio za mita Elfu tano na mita elfu 10.

     

    Kwa upande wa wanaume mbio za mita elfu tano, Kenya itawakilishwa na Isaih Kiplagat,Edwin Soy Cheruiyot pamoja na Thomas Longosiwa walioshinda kwenye mbio za majaribio.

    Kitengo kingine kilichokuwa na upinzani mkali sana nchini Kenya ni mbio za kitengo cha mita 1500.

    Upande wa wanaume baada ya raundi tatu na nusu za mapambano mazito, Silas Kiplagat alishinda na kufuzu akifuatwa na wenzake Asbel Kiprop na Nixon Chepseba ambao pia walipata tiketi kwa kumaliza katika nafasi tatu bora.

    Licha ya kuonekana kulemewa na wenzake Asbel Kiprop anaeshikilia rekodi ya dunia kwenye kitengo hicho alipata tiketi baada ya kuchukuwa nafasi ya tatu.

    Alitueleza mbinu aliyoitumia na kusisitiza kunyakuwa nafasi ya kwanza kwenye olimpiki.

    Silas Kiplagat alieshinda nafasi ya kwanza na kujipatia tiketi katika kitengo hichi anasema kabla ya mashindano ya olimpiki angependa kufanya mazoezi yake hapa nchini Kenya badala ya kufanya mazoezi nchi za nje.

    Upande wa wanawake mbio za mita elfu 1500 hazikuwa na upinzani mkali kwani Helen Obiri,Nancy ,Chebet na Eunice Jepkoech walipata tiketi kama walivyotrajiwa.

    Kenya ina sifa kubwa sana duniani ya kuzitawala na kutia fora sana kwenye mbio za mita elfu tatu na kuruka viunzi kwenye mashindano ya kimatiafa,na katika kindumbwedumbwe cha kutafuta tiketi mambo yalikuwa magumu sana kwani kila mmoja alitaka kudhihirisha weledi wake.

    Hatimae Brimin Kipruto,Ezekiel Kemboi na Abel Kiprop Mutai walipata tiketi za kuiwakilisha Kenya baada ya kupata nafasi tatu za kwanza.

    Brimin Kipruto ni chipukizi kwenye mbio hizi baada ya kupata tiketi hii atakuwa anatetea taji lake baada ya kushinda olimpiki ya Beijing mwaka 2008.

    Ezekiel Kemboi al maarufu POLICE alipata tiketi baada ya kuchukua nafasi ya pili kwenye mbio za mita elfu tatu kuruka viunzi, na kutokana na umaarufu wake na tajriba ya hali ya juu alishabikiwa kwa shangwe nyingi kutoka kwa mashabiki.

     

    Kina dada nao upande wa mita elfu tatu hawakuacha nyuma pia, kwani walitoana nyute na hatimae Milcah Chemos Cheywa,Merscy Wanjiku na Lydia Chebet Rotich wakapata nafasi tatu za kwanza.

    Mashabiki waliojaa katika uwanja wa Nyayo wakati wa mashindano haya walisubiri kwa raghba ya mkanja kujionea mbio za mita mia nane upande wa wanaume na kinada, mbio hizi ziliwajumuisha wanariadha wawili maarufu zaidi katika riadha nchini Kenya kwa sasa.Wao ni mabingwa wa dunia Daivid Rudisha na bingwa wa olimpiki mwaka 2008 Pamela Jelimo.

    Kipenga kilipopulizwa upande wa kinadada Pamela Jelimo alitimka kama swara na kuwashinda wenzake akijikatia tiketi ya moja kwa moja.

    Wenzake walimfuata kwa karibu ni Janeth Jepkosgei aliekuwa wa pili na Sylvia Cheseve wa tatu.

    Wote hawa walipata nafasi ya kuenda olimpiki.

    Jelimo aliekuwa akitokwa na machozi ya furaha alielezea jinsi alivyofurahi haswa baada ya kukosa mashindabi yoyote ya kimatiafa kwa miaka mitatu kutokana na jeraha. Aliapa kutetea dhahabu yake kwenye olimpiki.

    Upande wa wanaume bingwa wa dunia wa mita mia nane David Rudisha alitimka kama radi na kushinda mbio hizo huku akijigamba kuwa anasubiri olimpiki kwa hamu na ghamu ili ajipatie dhahabu yake ya kwanza kwenye mashindano hayo ya kihistoria.

      

    Timothy Kitum na Anthony Chemut walichukua nafasi ya pili na ya tatu na kupata tiketi.

    Kwa ujumla kikosi chote cha Kenya kilichoteuliwa kuiwakilisha kwenye Olimpiki siku hii ni

    Mita elfu 5 kinadada, ni Vivian Cheruiyot, Sally Jepkosgei na Viola Kibiwot na wanaume

    ni Isaih Kiplagat, Edwin Soy Cheruiyot pamoja na Thomas Longosiwa

    Mita elfu 3 wanaume ni Brimin Kipruto, Ezekiel Kemboi na Abel Kiprop Mutai na wanawake ni

    Milcah Chemos Cheywa, Merscy Wanjiku na Lydia Chebet Rotich

    Mita elfu 1500 wanaume ni Silas Kiplagat Nixon Chepseba na Asbel Kiprop na wanawake

    Ni Helen Obiri, Nancy Chebet na Eunice Jepkoech

    Na hatimae kitengo cha mita mia nane wanaume David Rudisha ,Timothy Kitum na Anthony Chemut na wanawake ni Pamlel Jelimo,Janet Jepkosgei na Sylvia Chesebe.

    Katika mashindano ya Olimiki ya London Uingereza Kenya itashiriki kwenye riadha, ndondi pamoja na kuogelea lakini kudura kuu za medali zinatarajiwa kupatikana kupitia riadha.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako