• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0724

    (GMT+08:00) 2012-07-27 17:55:05
    Barua ya kwanza inatoka kwa Daniel Khaoya Ngoya wa S.L.P 172-50200 Bungoma Kenya, anasema natumai kuwa mu buheri wa afya, huku Bungoma tunapokea vizuri matangazo yenu kwa njia iliyo safi kabisa, ingawa kadi hutumiwa kwa kiwango kidogo sasa inasababisha mawasiliano kupitia kwenye salamu kuwa machache mno. Ningependa mnitumie kadi za salamu kwa wingi ili niweze kuwajulia hali ya wasikilizaji wenzangu wa CRI.

    Mimi binafsi nimewahi kushiriki kwenye mashindano yenu na kufuatilia kwa karibu sana vipindi vyenu kuanzia mwaka 2000 lakini sijawahi kupokea zawadi yoyote, sasa nawaomba mnitumie majarida ya CRI na pia vitabu vya kujifunza kichina. Ndoto yangu kuu ni kualikwa na CRI ili nishuhudie mwenyewe namna ninavyoipenda CRI ambayo huongoza na nyingine zikifuata, natumai siku moja ndoto yangu itatimia.

    Hongera zangu ziwafikie Mama Chen Lianying, Pili Mwinyi, Josephine Moeni Waweru, Khamis Darwesh, Asha Nzunga Kitembe, Jackob Mogoa, Johari Mayoka, Fadhili Mpunji, Caroline Nassoro, Moses Onasaa na Fundi Bengo kwa tamthilia nzuri ya Doudou na mama wakwe zake na nawaomba kama kuna nakala ya kitabu cha tamthiliya hiyo naomba mnitumie. Mwisho nawaombea muwe na mwaka wa mafanikio huku nikitumai mtanitimizia maombi yangu.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Daniel Khaoya Ngoya kwa barua yako, na kwa kukujibu kuhusu kutopata zawadi ya chemsha bongo, tunaendelea kusisitiza kuwa, zawadi hazitolewi kwa kuangalia mtu fulani bali tunajali zaidi wale waliojibu vizuri maswali tuliyotoa, na tunashukuru pongezi lako kuhusu kutia sauti tamthilia ya Doudou na mama wakwe zake. Ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa mtoto wa Afrika, Happynes Julius wa Arusha Tanzania anasema mapema mwaka 2006 nilikutumieni mchoro wa picha ya ramani ya dunia, ramani ikiwa imebeba ujumbe wa amani itendeke kote duniani. Ni kipindi kirefu sasa kimepita amani ambayo haijasimama kote duniani. Badala yake vita vinavyosababishwa na uchu wa mali na madaraka ya uongozi vinaendelea kushika kasi. Hali hii imesababisha utulivu wa jamii katika maeneo husika kutoweka na watu wengi kuwa wakimbizi.

    Migogoro ya kisiasa na misuguano ya kikanda katika umiliki wa maeneo inaendelea kutawala siku hadi siku, mfano umiliki wa eneo la (SKARIBIRO) kati ya China na Vietnam ndani ya bahari ya China kusini. Nako Syria, Korea Kaskazini, Iran, Misuguano inaendelea. Bila kusahau barani Afrika, kwa upande wa vita vya njaa na magonjwa pia Sudan, Ethiopia, Eritrea na Mali eneo la Azawati kutaka kujitenga, Somalia nako ambako umaskini umekithiri hadi unahesabika kwa kipimo cha kilometa badala ya hatua.

    Kupitia kipindi hiki cha sanduku la barua ninaomba maoni na ushauri kutoka kwa wasikilizaji wa CRI, ni nini kifanyike ili dunia iweze kuwa na amani na haki sawa bila kusahau kushuka kwa uchumi wa Afrika na ongezeko la watu masikini duniani.

    Tunakushukuru sana mtoto wa Afrika, Happynes Julius kwa barua yako, kwakweli hadi leo hatujapokea mchoro wa ramani uliyotuma, labda ilikuwa imekwama njiani, kuhusu suala la vita na umasikini, ni kweli lilikithiri katika bara la Afrika na katika nchi za kiarabu, ingawa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Kimataifa na nchi nyingi zinajitahidi kuzuia na kuondoa hali hiyo, ili kuhakikisha dunia inakuwa eneo lenye amani na usalama, lakini bado mizozo na migogoro inaendelea, sisi redio China Kimataifa tunazisihi pande zote zinazohusika zijizue na kutumia njia ya amani katika kutatua migogoro hiyo. Ahsante sana.

    Sasa ni barua ya Yohana Marwa baruapepe yake ni marwa.yohana@yahoo.com Kemogemba Club S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania, anasema siku ya leo ningependa kupanda kwenye kipindi cha sanduku la barua kwa kuwapongeza kwa matangazo mazuri na ya uhakika kwani yanaendana na hali halisi. Kwasababu mnatupatia sisi wasikilizaji wenu kile tunachokihitaji kutoka CRI. Sina mengi zaidi isipokua kuwatakia kila la heri.ni wenu yohana marwa magaigwa.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Yohana Marwa, kwa vile CRI inawajali wasikilizaji ndio maana tunajaribu kukuleteeni vipindi na matangazo ambayo tunajua yatawaridhisha, na kama una maoni au mapendekezo unaweza kututumia ili tuboreshe zaidi matangazo yetu, ahsante sana.

    Sasa tunawasomea maoni tuliyotumiwa na wasikilizaji wetu kwenye mtandao maoni ya kwanza yanatoka kwa Pius Mwita wa New Jersey USA anasema ninatoa salaamu kwa watangazaji wote wa kiswahili Beijing idhaa ya kiswahili. Mimi ninawaomba mturudishie idhaa ya kiswahili. Tunapenda kusikiliza matangazo ya kiswahili kupitia kwenye channel hiyo ya kiswahili. Tafadhali sana mrudishe matangazo upesi iwezekanavyo mkipenda. Tutashukuru sana. Mimi ni msikilizaji mkubwa wa idhaa ya kiswahili ya redio China Kimataifa.

    Naye Ras Franz Manko Ngogo wa S.L.P 71, Tarime Tanzania anasema nimeizuru hii tovuti ya CRI na kuiona kuwa imepangiliwa vizuri kiasi cha kuvutia. Ni upeo mkubwa unaotumika kuifanya ipendeze hivyo. Hongera sana wataalamu wa tovuti ya CRI. Tupo nanyi pamoja.

    Msikilizaji wetu Epafra Stanley Deteba baruapepe yake ni epst01@hotmail.com naye anasema habari marafiki zangu wapendwa idhaa ya kiswahili Redio China Kimataifa, mimi msikilizaji wenu ninaendelea kuyategea sikio matangazo yenu kama kawaida na kufuatilia kwa njia ya mtandao pia, hongereni sana cri kwa mpangilio mzuri wa vipindi mlionao. Hakika CRI ni mfano wa kuigwa na idhaa nyinginezo ulimwenguni.

    Naye Suna baruapepe yake ni omarisuna@yahoo.com kwa upande wake anasema naipenda radio CRI kwa matangazo yake ninasikia habari za kila nchi

    Na Sikabwe Emmanuel mwenye baruapepe emmanuelsika@yahoo.fr anasema wapendwa watangazaji wa idhaa ya redio China ni siku nyingi hatujawasiliana kwa barua pepe napenda kuwajulisha kama habari nyingi zenye kutokea hapa kwetu BUKAVU mashariki mwa DRC CONGO hatuzisikii mnazitangaza kwenye idhaa ya redio China. Sasa kwa hiyo ninahitaji kufanya kazi hiyo pamoja nanyi niwe nawapasha habari zenye kutokea hapa kwetu BUKAVU hata KONGO nzima. nina hitaji kujuwa ikiwa mtapendezwa na hilo na muniunge mkono. Asante.

    Tunawashukuru wasikilizaji wetu wote wanaosikiliza matangazo yetu kwenye mtandao na kututumia maoni, tunawaomba muendelee kusikiliza na kutuma mapendekezo yenu, na kwa kumjibu Sikabwe Emmanuel, ni kwamba tunajaribu kutoa habari mbalimbali za DRC labda hujabahatika kusikia, ila tutakapohitaji mtu wa kututumia habari za huko DRC tutakutafuta kwani anuani yako tumeihifadhi, ahsanteni.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako