• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ni ya 13 kwenye mashindano ya olimpiki jijini London,Uingereza.Siku tatu zimesalia kabla kukamilika kwa mashindano hayo.

    (GMT+08:00) 2012-08-09 18:33:59

    Kamati ya kimataifa ya olimpiki(IOC) imesema haitachunguza ushindi wa mwanariadha Taoufik Makhloufi wa Algeria kwenye mbio za mita 1500 licha ya shaka ya kupata kwake nafuu kwa usiku mmoja. Makhloufi mwenye umri wa miaka 24 alishinda mbio hizo saa 24 baada ya kujiondoa chini ya mita 150 kwenye mbio za mchujo za mita 800.Mwanariadha huyo aidha aliondolewa kwenye olimpiki na shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha(IAAF) kwa madai ya kutojituma kwenye mbio hizo.Aidha uamuzi huo ulibatilishwa baada ya Makhloufi kuonyesha cheti cha daktari kuonyesha alikuwa na jeraha la goti.Alipoulizwa kuhusu goti lake punde baada ya kushinda mbio hizo za mita 1500,mwanariadha huyo alisema ni kwa uwezo wa Mungu ameweza kushinda mbio hizo na kusisitiza kuwa goti lake bado lina jeraha na linahitaji upasuaji.

    Mwanariadha Caster Semenya wa Afrika Kusini amerudi kwa kishindo kwenye mbio za mita 800 miaka mitatu baada ya kulazimishwa kufanyiwa uchunguzi wa kijinsia.Semenya ambaye alimaliza wa pili kwenye kundi lake la mchujo la mbio za mita 800 kwa kina dada alitengwa kwa muda wa mwaka mmoja huku bodi ya michezo ya riadha ikitafakari kama imruhusu kushiriki mchezo huo.Semenya mwenye umri wa miaka 21 alishinda taji la dunia la mbio za mita 800 kwa kina dada mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 18.Aidha mwanariadha huyo alipimwa na kuruhusiwa kushiriki riadha mwaka 2010 ambapo aliibuka wa pili kwenye mashindano ya dunia mwaka jana.Semenya aliibeba bendera ya Afrika Kuisni wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya olimpiki jijini London.

    Ikiwa zimesalia saa chache kabla ya mechi ya kusaka medali ya dhahabu kwenye soka ya kina dada kati ya Marekani na Japan,ligi mpya ya soka ya kina dada imetangazwa kuundwa nchi Marekani na itaanza mwakani.Taarifa hii inajiri siku kadha baada ya mwenyekiti wa soka nchini Marekani,Sunil Gulati kuzungumzia njia tofauti zitakazowawezesha wanasoka wa kike wa nchi hiyo kusakata kabumbu nje ya nchi.Ligi mbili zilizoko nchini humo ambazo hazijafikia kiwango cha juu cha soka ya wanawake ni Ligi ya kina dada ya soka(WPS) ambayo ilidumu kwa misimu mitatu kufikia mwaka 2011 na Muungano wa vyama vya soka vya kina dada (WUSA) pia iliyodumu kwa misimu mitatu hadi kufikia mwaka 2003.

    Mwanariadha Usain Bolt wa Jamaica atajaribu kuandika ukurasa mpya kwenye historia yake ya riadha atakapojitupa kiwanjani leo kusaka medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 200.Iwapo mwanariadha huyo atafaulu kushinda mbio hizo,atakuwa mtu wa kwanza kushinda nishani ya dhahabu kwenye mbio za mita 100 na 200 kwa pamoja.Mapema wiki hii Bolt alisema amemuonya mpinzani na raia mwenza,Yohan Blake kuwa mbio za mita 200 ni kipenzi kwake.

    Mwanariadha Sarah Attar wa Saudi Arabia amemaliza katika nafasi ya mwisho kwenye mbio za mchujo za mita 800 kwa kina dada. Licha ya Attar kushika mkia mashabiki waliokuwa kiwanjani walisimama na kumpigia makofi kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoa nchini mwake kushiriki riadha.Huku akiwa amejifunika kutoka kichwani hadi kwenye vidole vya mguu,Attar mwenye umri wa miaka 19 aliandikisha historia siku tano baada ya mwanadada Wojdan Ali Seraj Abdulrahim Shahrkhani pia wa nchi hiyo kushiriki mchezo wa judo kwa kina dada.Aidha viongozi wa dini ya kiislamu nchini humo wamesemekana kuelezea dharau zao kwa Wojdan kwa kudai alishiriki pambano hilo mbele ya wanaume wakiwa ni pamoja na majaji na refarii.Saudi Arabia ni mojawapo ya nchi tatu pamoja na Qatar na Brunei zenye kuamini dini ya kiislamu ambazo zimetuma wanamichezo kwenye olimpiki huku kwa mara ya kwanza ikijumuisha wanamichezo wa kike.

    Sakafu ambayo waandishi wa habari wa kimataifa walikuwa wakiwafanyia mahojiano mabingwa wa mchezo wa voliboli ya ufukweni(Beach Volleyball) imeporomoka na kuwaacha waandishi wakikimbilia usalama.Hakuna aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo huku kina dada washindi wa medali ya dhahabu ya mchezo huo, Misty May-Treanor na Kerri Walsh Jennings wa Marekani wakiondolewa kwa haraka.

    Tuangalie meza ya medali kufikia sasa…..

    JUMLA Dhahabu Fedha Shaba

    1. China 77 36 22 19

    2. Marekani 81 34 22 25

    3. Uingereza 48 22 13 13

    4. Korea Kusini 25 12 7 6

    5. Russia 52 11 19 22

    19. Afrika Kusini 4 3 1 0

    29. Ethiopia 4 2 0 2

    33. Kenya 5 1 2 2

    39. Algeria 1 1 0 0

    45. Misri 2 0 2 0

    51. Tunisia 2 0 1 1

    66. Morocco 1 0 0 1

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako