• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ya 16 na ya mwisho ya michezo ya olimpiki jijini London Uingereza.

    (GMT+08:00) 2012-08-12 20:12:12

    Jumla ya michezo 287 kati ya 302 tayari washindi wamejulikana……...imesalia michezo 25……...Mieleka kwa wanaume,Uendeshaji Baiskeli,Masumbwi vitengo kadha,Mpira wa kikapu kwa wanaume,Gymnastics vitengo kadha.

    Tuanze na riadha mbio za mita 5000 kwa wanaume, Mo Farah wa Uingereza alidhihirisha ubabe wake na kutia mkobani medali ya dhahabu, Gebremeskel Dejen wa Ethiopia akakumbatia medali ya fedha nae Longosiwa Thomas Pkemei wa Kenya akajiliwaza na medali ya shaba.Mbio za mita 800 kwa kina dada zilivunja moyo wakenya wengi baada ya mwanariadha Pamela Jelimo kushindwa kutamba.Aidha Savinova Mariya na Poistogova Ekaterina wa Russia walibeba nishani za dhahabu na shaba mtawalia na kumwacha Caster Semenya wa Afrika Kusini kuchukua medali ya fedha.Timu ya kina dada ya mbio za mita 400 kupokezana kijiti ya Marekani ilijinyakulia nishani ya dhahabu,Russia ikachukua nishani ya Fedha nayo ile ya Jamaica ikalitilia mkobani medali ya shaba.Mbio za mita 400 kupokezana kijiti kwa wanaume zilishuhudia Jamaica chini ya Uongozi wa Usain Bolt ikikumbatia medali ya dhahabu na kuandikisha rekodi mpya ya dunia,Marekani ikaridhika na medali ya fedha nayo Trinidad and Tobago ikatosheka na nishani ya shaba.

    Kirdyapkin Sergey wa Russia alijinyakulia nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa kutembea kwa kasi kwa wanaume kilomita 50, Tallent Jared wa Australia akajitwika medali ya fedha nae Si Tianfeng wa China akachukua nishani ya shaba.kwa upande wa kina dada kitengo cha kilomita 20, Lashmanova Elena na Olga Kaniskina walichukua medali za dhahabu na fedha na kumlazimisha Qieyang Shenjie wa China kujiliwaza na nishani ya shaba.

    Kwenye mchezo wa Kayaki kwa wanaume kwa mtu mmoja kitengo cha K-2 mita 200, McKeever Ed wa Uingereza alivikwa nishani ya dhahabu, Craviotto Rivero Saul wa Hispania akakumbatia medali ya fedha nae de Jonge Mark wa Canada akaridhika na medali ya shaba.kwenye kitengo cha C-1 mita 200 kwa wanaume, Cheban Yuri wa Ukraine aliibuka na medali ya dhahabu, Shuklin Jevgenij wa Lithuania akabeba medali ya fedha nae Shtyl Ivan wa Russia akajivunia medali ya shaba.Bado kwenye mchezo huo kwa kina dada kitengo cha K-1 mita 200,Carrington Lisa wa New Zealand alibeba medali ya dhahabu,Osypenko-Radomska Inna wa Ukraine akajizolea nishani ya fedha nae Douchev-Janics Natasa wa Hungary akakumbatia medali ya shaba.Kitengo cha K-2 mita 200 kwa timu ya watu wawili kwa wanaume,Postrigay Yury na Dyachenko Alexander wa Russia walivuna nishani ya dhahabu, Piatrushenka Raman na Makhneu Vadzim wa Belarus wakakumbatia media ya fedha nao Heath Liam na Schofield Jon wa Uingereza wakajaza mkoba wan chi hiyo na medali ya shaba.

    Mchezo wa mpira wavu kwa kina dada uliona Brazil ikichukua medali ya dhahabu,Marekani ikavikwa medali ya fedha nayo Japan ikakumbatia nishani ya shaba.

    Mwanadada Bresset Julie wa Ufaransa alichukua medali ya dhahabu na kuwalazimisha Spitz Sabine wa Ujerumani na Georgia Gould wa Marekani kujiliwaza na medali za fedha na shaba mtawalia kwenye mchezo wa uendeshaji baiskeli aina ya "mountain bike" kwa kina dada.

    Mechi ya soka kwa wanaume ilitoa matokeo ya kushangaza huku Brazil ambayo ilikuwa imepigiwa upato kushinda ikilazimishwa kuchukua nishani ya fedha.Mexico ilibeba medali ya dhahabu baada ya kupata ushindi finyu wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Brazil.

    Mchezo wa Rhythmic Gymnastics kwa kina dada ulishuhudia Yevgenia Kanayeva na Dmitrieva Daria wa Russia wakibeba nishani za dhahabu na fedha mtawalia na kumwacha Lyubov Cherkashina wa Belarus kujiliwaza na medali ya shaba.

    Timu ya Ujerumani ilinyanyua medali ya dhahabu kwenye mchezo wa mpira wa magongo kwa wanaume,Uholanzi ikachuka medali ya fedha nayo Australia ikaridika na medali ya shaba.

    Timu ya Australia ilivikwa nishani ya shaba baada ya kuifunga Russia vikapu 83 kwa 74 kwenye mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanaume.

    Kwenye mchezo wa mpira wa mkono kwa kina dada,timu ya Norway ilivikwa nishani ya dhahabu,Montenegro ikabeba medali ya fedha nayo Hispania ikatia mkobani nishani ya shaba.

    Asgarov Toghrul wa Azerbaijani alitia mkobani medali ya dhahabu kwenye mchezo wa mieleka kwa wanaume kitengo cha kilo 60 freestyle,Besik Kudukhov wa Russia akaridhika na medali ya fedha nao Coleman Scott wa Marekani na Dutt Yogeshwar wa India wakangangania medali ya shaba.Kitengo cha kilo 84 freestyle kwa wanaume, Sharifov Sharif wa Azerbaijani alivikwa medali ya dhahabu,Espinal Jaime Yusept wa Puerto Rico akaridhika na medali ya fedha nae Marsagishvili Dato wa Georgia akakumbatia medali ya shaba.Bado kwenye mieleka kitengo cha kilo 120 kwa wanaume, Artur Taymazov wa Uzbekistan alibeba nishani ya dhahabu, Modzmanashvili Davit wa Georgia akavikwa medali ya fedha nao Ghasemi Komeil wa Iran na Makhov Bilyal wa Russia wakagombani nishani ya shaba.

    Walcott Keshorn wa Trinidad and Tobago alivikwa nishani ya dhahabu kwenye mchezo wa kutupa mkuki(Javelin) kwa wanaume, Pyatnytsya Oleksandr wa Ukraine akakumbatia nishani ya fedha nae Ruuskanen Antti wa Finland akaridhika na medali ya shaba.

    Mchezo wa kupiga mbizi kwa wanaume mita 10 ulishuhudia David Boudia wa Marekani akijitilia mkobani nishani ya dhahabu, Qiu Bo wa China akabeba medali ya fedha nae Tom Daley wa Uingereza akachukua medali ya shaba.

    Tujirushe ulingoni kwenye mchezo wa masumbwi kwa wanaume kitengo cha Light Flyweight, kilo 49, Zou Shiming wa China alinyanyua medali ya dhahabu baada ya kumshinda Pongprayoon Kaeo wa Thailand ambae alijitwalia nishani ya fedha.kitengo cha Bantamweight, Luke Campbell waUingereza alijizolea nishani ya dhahabu baada ya kumchubua sura Nevin John Joe wa Ireland aliyelazimika kuchukua nishani ya fedha.

    Tuangalie meza ya medali kufikia sasa…..

    JUMLA Dhahabu Fedha Shaba

    1. Marekani 102 44 29 29

    2. China 87 387 27 22

    3. Uingereza 62 28 15 19

    4. Russia 78 21 25 32

    5. Korea Kusini 27 13 7 7

    24. Afrika Kusini 6 3 2 1

    25. Ethiopia 7 3 1 3

    28. Kenya 9 2 3 4

    44. Tunisia 3 1 1 1

    50. Algeria 1 1 0 0

    55. Misri 2 0 2 0

    68. Botswana 1 0 1 0

    68. Gabon 1 0 1 0

    78. Morocco 1 0 0 1

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako