• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0807

    (GMT+08:00) 2012-08-29 15:32:49
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Wambura M. Nyamhanga wa Kemogemba Salam Club S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania, anaanza kwa kusema mimi ni mwanafunzi wa kidato cha nne nasoma katika shule ya sekondari ya Mwema iliyoko katika wilaya ya Tarime mkoani Mara. Nilianza kusikiliza idhaa hii ya Kiswahili kuanzia mwaka 2008 nikiwa darasa la 7, ambapo idhaa hii ilivutia sana siku baada ya nyingine kutokana na matangazo yake mazuri, vipindi vya kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha, pamoja na watangazaji bora waliobobea katika nyanja hii ya utangazaji na sauti zao nzuri zenye mvuto wa kipekee.

    Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwani kwa mapenzi yake nilituma barua yangu ya kwanza hapo studio za radio China kimataifa, mwaka 2011 nanyi mkaipokea kwa moyo mmoja na kwa mikono miwili na kunitumia barua ya ujulisho ikiwa pamoja na bahasha zilizolipwa kwaajili ya kuwatumia maoni, pamoja na kadi za salamu. Kitu ambacho kilinivutia sana na kunitia moyo na kunifanya niipende CRI, siku baada ya siku, shukrani nyingi sana CRI nami nawaahidi nitakuwa msikilizaji wenu daima, ahsante sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Wambura M. Nyamhanga kwa barua yako ya shukurani na maoni, kweli hata sisi tuna furahi sana kupata barua zako Pia tunawashukuru wasikilizaji wetu wote kwa kututumia barua mbalimbali zenye maoni, masuali, mapendekezo na salamu. Mwisho tunakutakia masomo mema ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya, anasema kwanza salamu zangu ziwaendee watangazaji na wasimamizi wa Idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa. Naomba kuchukua fursa hii ili kutoa pongezi zangu kwa CRI. Bila shaka huu ni mwaka wa 2012 ni furaha yangu kuwa Mwenyezi Mungu ametufanikisha kuuona, hata hivyo sisi wasikilizaji tunazidi kufurahia vipindi na matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa.

    Ni wazi kuwa mwaka jana idhaa ya Kiswahili ya CRI ilipiga juhudi kubwa katika kutuandalia vipindi na matangazo bora zaidi. Pongezi zangu za dhati zifike kwa kuwatumia wasikilizaji kalenda maridadi za mwaka 2011, kutupasha habari motomoto kuhusiana na maonesho ya kimataifa ya Shanghai ya mwaka 2010 na hata kutuandalia shindano la chemsha bongo kuhusiana na maonesho hayo.

    Vilevile kuzidisha juhudi ya kusoma barua za wasikilizaji kwenye kipindi chetu cha sanduku la barua, kuwatumia wasikilizaji kadi za salamu ambazo zina picha za watu wa makabila mbalimbali ya China. kutupasha habari za michezo ikiwemo michuano ya kombe la dunia, ambayo kwa mara ya kwanza imeandaliwa na bara la Afrika, nchini Afrika Kusini. Kutuburidha vilivyo kwa muziki na pia kutufahamisha habari kuhusiana na maisha ya kimuziki ya wanamuziki mbalimbali.

    Pia kuwatumia wasikilizaji vitabu vya kuwa nasi jifunze kichina na kuzidi kutuandalia kipindi chetu cha studio ya kichina na kuwa nasi jifunze kichina. Kualikwa kwa wasikilizaji watano kutoka Tanzania kutembelea China kwa siku 10, kutuandalia shindano la chemsha bongo kuhusu miaka 45 tangu China na Tanzania zianzishe uhusiano wa kibalozi, shindano ambalo lilikuwa wazi kwa wasikilizaji kutoka Kenya na Tanzania, na mwisho kutupatia matumaini kuwa mtaboresha vipindi na matangazo ya mwaka 2012, ahsante sana.

    Shukurani za dhati wasikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie, kweli tunafuraha kubwa sana kwa kupokea maoni mbalimbali kuhusu chemsha bongo ya maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania na vipindi vyetu vingine, hili ni jambo la faraja sana kuona kweli mnafuatilia vipindi vyetu, chemsha bongo, uhusiano na maendeleo ya nchi hizi mbili, na kuhusu michezo kwa vile sasa michezo ya Olimpiki inaendelea kule London Uingereza, basi pia tunajaribu kukuleteeni habari hizo ili mjue nini kinaendelea kwenye michezo hiyo, ahsante sana.

    Na Barua ya mwisho iantoka kwa msikilizaji wetu Julius M Mafuriko wa Club ya wasikilizaji ya Kemogemba S.L.P 71 Tarime Mara Tanzania, anasema napenda kutoa pongezi zangu kwa redio China kimataifa kwa kutimiza miaka 70, matangazo ya CRI yakianzishwa kutoka kwenye pango la Yan'an hadi kufikia kurushwa kwenye mitabend ya FM katika miji ya nchi mbalimbali duniani. Baada ya CRI kuanzishwa iliandaa muziki maalumu kama alama ya CRI kila inaporusha matangazo yake hewani.

    Pia napenda kuipongeza CRI kwa kuamua kutumia lugha ya Kijapani kwa mara yake ya kwanza mwaka 1941. Lugha hiyo iliwafanya wanajeshi wa jeshi la Japani kusikiliza matangazo. Pia natoa shukurani kwa Bibi Hara Kiyoshi ambaye ni mtangazaji wa kwanza mjapani wa CRI aliyepinga vita na kuishi nchini China. CRI sasa ni redio inayosikilizwa na mamilioni ya watu tofauti, ambapo awali ilikuwa ikisikilizwa na watu 300 tu wakati ilipokuwa ikirusha matangazo yake kwenye pango.

    Pia napenda kuipongeza CRI kwa kurusha matangazo kwa lugha ya kingereza baada ya kupata ushindi dhidi ya uvamizi wa Japani mwaka 1947, na baada ya ushindi huo CRI iliamua kurusha matangazo yake kwa lugha ya kichina mnamo mwaka 1949, baada ya hapo CRI iliamua kuhamia Beijing na kurusha matangazo yake kusini mwa China na sehemu mbalimbali za Asia kusini Mashariki.

    Na pia naipongeza CRI kwa kufungua kituo cha FM mjini Nairobi kikiwa ni cha kwanza kwa Afrika Mashariki, na kuendelea kufungua vituo vingine vya FM katika nchi mbalimbali ambapo hadi kufikia mwaka 2011 vituo hivyo vimefikia 60. Mwisho naipongeza CRI kwa kuanzisha tovuti ya Internet ya CRI na hatimaye kuwapongeza wasikilizaji wenzangu wote kwa kundelea kuiunga mkono redio China Kimataifa, ahsante sana.

    Kwanza kabisa tunamshukuru sana msikilizaji wetu Julius M Mafuriko kwa barua yako ndefu kidogo. Tunavutiwa sana na moyo wako wa kufuatilia maendeleo ya redio China kimataifa na matangazo yake, na hata una kumbukumbu ya matokeo yote tangu kuanzishwa kwa redio hii. Tunakuomba uendelee kufuatilia zaidi matangazo na vipindi na mwisho kutoa maoni na mapendekezo, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako