• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0814

    (GMT+08:00) 2012-08-29 15:33:21
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Christopher P. Masanja wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania, anasema kwanza kabisa napenda kuipongeza sana redio China Kimataifa kwa vipindi vyake murua. Sisi wadau wa kituo hiki, kila ifikapo wakati wa matangazo hujiweka kando ya redio zetu ili tufaidi uhondo wa vipindi vyenu vinavyoburudisha. Kwa hakika napenda kuwapongeza wafanyakazi wote wa kituo hiki kwa vipindi vyenu hakika vinatupanua mawazo kijografia, kihistoria na kimaendeleo.

    Kipindi kikubwa kinachonivutia ni China machoni mwetu, na hususan kipindi kuhusu Mogoa alipotembelea mkoa wa Harbin mpakani mwa China na Russia. Kipindi hiki kiliniacha mdomo wazi na hasa niliposikia habari za kampuni ya kilimo iitwayo Deidodang. Ni ajabu kubwa sana kwa kampuni kulima mazao kwaajili ya chakula cha kutosha watu bilioni moja nukta tatu, kwa hahika hii ni ajabu sana hususan kwa nchi zetu za kiafrika ambazo kilio chake kikubwa ni njaa kila kukicha.

    Swali langu ni kuwa kwanini viongozi wetu wasipokee wataaalamu wa kilimo kutoka kwenye kampuni kama hiyo ya Deidodang wakajifunza mbinu mbalimbali za kilimo ili nasi tuondokane na njaa iliyozidisha umasikini? Kumbuka ni rahisi sana kwa mtu aliyeshiba kutembea uchi, kuliko kuvaa suti yenye gharama kubwa na kisha ulale na njaa kwa muda wa siku tatu. Ombi langu kwa watayarishaji wa vipindi vya redio ni kuwa watuandalie kipindi kimoja tu kinachohusu kampuni hiyo ya Deidodang kitakachofafanua habari za kampuni hiyo. Naomba ieleweke kipindi hiki kirushwe mara moja tu kwenye kipindi mama cha China Machoni mwetu. Mwisho nawasalimu watangazaji wote wa CRI, wasikiliazaji wote wa CRI, waafrika wote waishio nchini China na raia wote wa China, ahsante sana.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Christopher P. Masanja kwa barua yako, kuhusu ombi lako la kutayarisha kipindi kuhusu kampuni ya Deidodang na shughuli zake kwa ujumla tutajaribu kufuatilia na kuandaa kipindi hicho, lakini tungependa kuweka wazi suala moja, kampuni hiyo sio kama ni pekee kwa China, inayoshughulika na kilimo cha mazao ya chakula cha kulisha China nzima, isipokuwa kuna kampuni nyingine nyingi tu ambazo nazo pia zinajishughulisha na kilimo, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa Bi Halima Ijeiza wa S.L.P 14-40602 Ndori Kenya anasema pokeeni salamu nyingi kutoka kwangu, kwani namshukuru Rabuka kwa yote mliyotutendea tangu tulipoanza mwaka huu. Pia tumshukuru kwa kutupa uzima kwani tu buheri wa afya.

    Ningependa kuwashukuru kwa maswali ya chemsha bongo mliyonitumia kwani majibu yalikuwa kwenye makala mlizosoma napenda kuwajulisha kuwa siku hizi sipati kadi za salamu mlizokuwa mnanitumia, kwani imekuwaje?

    Tukiwa tunamshukuru Mungu kwa mema aliyotutendea tunafaa kumuomba awakumbuke wale wanaokumbwa na janga la njaa katika pembe ya Afrika na sote tunafaa kujitolea na kuchanga pesa ili kuwasaidia. Tukumbuke kuwa kutoa ni moyo usambe ni utajiri. Pia tunafaa kuwaombea amani ndugu zetu na dada zetu walio Somalia kwa vita vinavyoendelea vikome kwani maisha ya watu wengi yanapotea. Ahsante sana.

    Kwanza tunapenda kukushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Halima Ijeiza kwa barua yako, pia tunasikitishwa sana kuona vita bado vinaendelea nchini Somalia, na hivi majuzi tu nchi hiyo imepitisha katiba mpya, hivyo tunatumai kuwa hatua hiyo itasaida kuingiza nchi hiyo kwenye hali ya utulivu, na kuhusu suala la njaa katika pembe ya Afrika tunapenda kuzipongeza nchi mbalimbali ikiwemo China kwa kutoa msaada wa chakula katika sehemu hiyo, ila kwa sasa tunatumai kuwa hali kidogo imekuwa nzuri, ahsante sana.

    Msikilizaji wetu Truphosa Aluoch Akhusama wa S.L.P 2191 Kakamega Kenya anasema, kwanza napenda kuipongeza redio China kimataifa kwa kazi nzuri inayofanya kwa kutuletea matangazo na vipindi na kurusha kupitia Kenya, Afrika na nchi nyingine katika dunia, nina uhakika kwa habari tunazopata hapa Kenya katika idhaa ya Kiswahili kutoka saa nne hadi tano usiku katika wiki, zinawasaidia wakenya wengi na nchi nyingine duniani kwa kuelewa ukweli wa maisha. Kwani habari hizo zina muelekeo mwema kwa kuwafunza wakenya wengi jinsi ya kuishi maisha bora, tunawaomba muendeleee hivyohivyo na muongeze utangazaji mwingi, mwisho naomba mnitumie kadi za salamu. Ahsante sana.

    Shukrani nyingi sana msikilizaji wetu Truphosa Aluoch Akhusama kwa barua yako fupi, ni kweli vipindi vyetu vingi huwa tunajaribu kuangalia zaidi maisha ya kila siku ya watu, tunatumai kuwa kupitia vipindi hivyo tunatoa mafunzo makubwa, ahsante sana.

    Na barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Philip Mokaya Machuki wa Nyakware CRI List Club S.L.P 646 Kisii Kenya anasema kwanza kabisa pokeeni salamu zangu kutoka hapa Kisii nikiwa namatarajio kwamba nyote huko ni wazima, ni muda sasa tangu mpokee barua kutoka kwangu na hii ni kwasababu ya masomo chuoni, lakini hii leo ninafuraha ya kuwaeleza kwamba nimemaliza masomo yangu na nitakuwa na muda wa kutosha kabisa kuitegea na kuiandikia CRI barua mara kwa mara.

    Pia ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza marafiki zangu wote kutoka hapa Kenya, Tanzania na sehemu nyingine mbalimbali za Afrika Mashariki na kati ambao mnanikumbuka mara kwa mara kupitia kipindi cha salamu zenu. Kwetu sisi redio China ni kama daraja ambalo linatuunganisha kati ya China na Afrika. Vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya CRI vinaendana na wakati, kwasababu vinaelimisha, kufundisha na hata kuburudisha.

    Lile ambalo siwezi kusahau ni ushirikiano mzuri kati ya CRI na wasikilizaji kwani mara kwa mara huwa napokea barua kutoka kwenu, kuna barua ambayo nilipokea kitambo kidogo ambayo ndani yake ilikuwa na CD na vitabu vya jifunze kichina bado naendelea kufuatilia masomo hayo na kusema ukweli ni magumu lakini tunajitahidi. Usikivu wa matangazo kupitia idhaa ya Kiswahili ya KBC ni mzuri sana, CRI ndio kituo cha habari pekee ambacho kimeanzisha uhusiano na KBC na tunashukuru kwa hilo kwasababu kupitia KBC tunapata matangazo bila usumbufu wowote ule. Ahsante sana.

    Nasi tunakushukuru sana msikilizaji wetu Philip Mokaya Machuki kwa barua yako, ni kweli muda mrefu umepita bila kupokea barua yako, tunatumai kuwa utakuwa umefanya vizuri kwenye masomo yako, na kuhusu vitabu ulivyopokea, unaweza kusikiliza huku ukifuatilia kwenye vitabu hivyo masomo ya kichina, tunakiri kuwa kweli lugha ya kichina ni ngumu, na ndio maana tumetia CD ili ziweze kuwaongoza wasikilizaji wetu wanaopenda kujifunza, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako