• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0828

    (GMT+08:00) 2012-08-29 15:35:36
    Barua ya kwanza inatoka kwa Geofrey Wandera wa EVEREADY SECURTY GUARD S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anasema hii ni furaha ambayo siwezi kuificha kamwe, ilikuwa kwangu siku njema nilipopokea jarida zuri na maridadi la China Today, jarida hili limepambwa kisawasawa, limebeba mengi mazuri ambayo yana uzito wake, ingawa nimechelewa kulipata, lakini jawabu ni kuwa nimeshalipata sasa.

    Kwangu mimi nimeshaanza kulipekuwapekuwa kwa kulisoma kurasa baada ya kurasa. Ingawa jarida hili limekusanya na kuonesha baadhi ya miundo mbinu ya China kama vile majengo marefu yenye ghorofa nyingi, barabara mpya ambayo imewekwa pembeni mwa jarida hilo. Mbali na hayo ndani mwa jarida hili hasa katika ukurasa wa 60 na 61, kuna elimu ya mapishi, jinsi ya kuandaa jiaozi na vilevile maandalizi ya kupika chakula cha Kung Paa Chicken.

    Pembeni pia kuna wanamuziki ambao wamesimama na kila mmoja ameshika ala yake ya muziki. Biashara nayo haijaachwa nyuma ambapo kuna picha nzuri za mahoteli kama vile hoteli ya Beijing, hoteli ya Jianguo ya Beijing na nyinginezo, kwa kweli kuna mengi ya kusoma na kujifunza ndani ya jarida hili. Hii ni taarifa fupi tu ambayo nimekusanya lakini mengi nitajifunza na wenzangu tunaposoma kwa pamoja, kwani kwa pamoja tunaweza kusonga mbele hatua kwa hatua. Hongera CRI asanteni sana.

    Shukran za dhati Bwana Geofrey Wandera kwa barua yako, nasi tunashukuru kwa kututaarifu kuwa umepokea jarida hilo na kubwa ni kwamba umelifurahia, tunatumai kuwa utakapolisoma pamoja na wenzako, nao watalifurahia na kujifunza mambo mengi kuhusu China, mwisho tunakuomba wewe na wasikilizaji wengine muendelee kusikiliza redio China kimtaifa na kutoa maoni na mapendekezo yenu, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa Yohana Marwa Magaigwa wa klabu ya wanakemogemba baruapepe yake ni marwa.yohana@yahoo.com, anasema ni matumaini yangu kuwa hamjambo timu nzima ya CRI hapo Beijing China Idhaa ya Kiswahili. Kwa mara nyingine tena ni siku njema kwangu kuungana na wasikilizaji wenzangu wa Idhaa hii kusema machache kuhusiana na matangazo ya Radio China kimataifa kwa ubora wake wa kuhakikisha kuwa tunaendelea kunufaika na kile kinachotolewa na radio hii ya Ulimwengu mzima kwa nyanja mbalimbali katika kupasha habari mpya mara zinapotokea katika kona mbalimbali bila kikomo kwa hili ndo maana nasema CRI ni radio ya ulimwengu wote.

    Nikiwa na wingi wa furaha na kutokana na kusoma kwenye mtandao napenda kuungana na wananchi wa China kulipongeza Bunge la umma la China kwa uamuzi wa busara sana waliochukuwa kwa kuwaondolea wananchi wa China kodi ya kilimo kutokana na kile kinachoonekana kama kutaka kuleta mapinduzi ya uzalishaji wa chakula cha kutosha na kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kuweza kufikia lengo la kuwa na chakula cha kutosha.

    Hii ni hatua kubwa sana kwa serikali ya China kutambua umuhimu wa raia wake hadi kufikia uamuzi kama huu ambao unastahili kuigwa na nchi nyingine katika bara la Asia na kwingineko duniani kote kwani katika kila nchi sio kweli kwamba wote wana uwezo wa kulipia kila kitu kwa serikali yao, kweli ni jambo la kupendeza sana kwa uamuzi uliochukuliwa na serikali ya China.

    Japokuwa mara nyingi idhaa hii haisomi hewani barua pepe zinazotumwa na wasikilizaji nina matumaini kuwa hii barua pepe yangu itawafikia na pongezi zangu zitaifikia sekta husika na wananchi kwa ujumla. mara nyingi ninafurahia matangazo ya CRI mara yanapokuwa hewani kutoka Beijing China kwani huwa yameandaliwa kwa kiwango cha hali ya juu sana na kutokana na hili siku zote CRI idhaa ya kiswahili itaendelea kuvuna wasikilizaji wengi zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati bila kusahau kokote duniani ambako kiswahili kinasikika.

    Kutokana na hili, mimi nipo pamoja na CRI japokuwa kwa sasa muda wa kuwasiliana nanyi kwa njia ya barua ni ngumu kidogo hivyo basi ninaomba niwasiliane nanyi kwa njia hii ya barua pepe kwani kwa sasa hii ndio njia ya rahisi kwangu ya kuwasiliana nanyi CRI idhaa ya kiswahili kwani kutosikiliza matangazo ya Radio China kimataifa kwangu ni hasara kubwa sana waswahili wanasema kizuri chajiuza kibaya chajitembeza kwa maana kuwa CRI iko mahali pake kwa kile inachokitangaza kwa hadhira yake. Mwisho nawatakia kila la kheri CRI.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Yohana Marwa Magaigwa kwa barua yako ndefu yenye pongezi kuhusu matangazo yetu kwa ujumla, pia kuhusu malalamiko ya kutosoma baruapepe za wasikilizaji, sio sahihi kwani kila kipindi tunajaribu kuchanganya barua tunazotumiwa na wasikilizaji wetu kwa njia ya posta na baruapepe, labda husikilizi kipindi kwa makini, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako