• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0925

    (GMT+08:00) 2012-09-25 16:00:53
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Wilson Julius Akhusama wa S.L.P 2191-50100 Kakamega Kenya, anaanza kwa kusema mimi kama shabiki sugu wa CRI ningependa kuwashukuru watangazaji wote wa CRI pamoja na wafanyakazi wote kwa ujumla, mimi mwenyewe naona pia mwaka umeanza vizuri. Kulingana na maoni yangu ni kwamba ningependa kipindi chetu cha salamu kiongezwe muda kutoka saa nne za usiku hadi saa tano kasorobo usiku, kwasababu mashabiki ni wengi na muda ni mfupi na pia naomba mniletee maswali ya chemsha bongo na kalenda ya mwaka 2012.

    Pia napenda kupongeza hasa kwa mwaka jana mliponitumia fulana pamoja na cheti na mimi pia niliwatumia picha yangu. Mungu aibariki Kenya yetu, aibariki China na mashabiki wa CRI na watangazaji wote wa CRI.

    Kwanza tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Wilson Julius Akhusama kwa barua yako fupi ya pongezi, na pia tumepokea kwa mikono miwili pongezi hizo. Ila kukujibu kuhusu kuongezwa muda wa kipindi cha salamu zenu, inabidi tuwe wa kweli ni jambo ambalo litakuwa gumu kulitekeleza kwa sababu tuna vipindi vingi vya kutangazwa na matangazo yetu kawaida huwa ni kwa saa moja tu, hivyo tunaomba mkubali muda huo na mtuwie radhi, ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Ramadhan Hamisi wa S.L.P 14-40602 Ndori Kenya, anaanza kwa kutusalimia asalam aleikum, natumai kuwa bado mmesimama kidete mithili ya chuma cha pua, hata baada ya kudidimia kwa uchumi wa dumia mwaka uliopita, kwani bado mnaweza kujiboresha na kujiimarisha zaidi. Huku niliko sote tuko salama na tunazidi kukuombeeni kwa rabuka awajaalie makubwa na kuimarisha maisha yenu. Nawashukuru kwa jarida la daraja la urafiki, mlilonitumia kwani limenijuza mengi kuhusu China.

    Nimepokea salamu za mkuu wa CRI kwa furaha na ninawapa heko kwa matangazo yenu, mmeweza kuelewa jinsi ya kuimarisha uchumi wenu, na tunaomba uchumi wenu usididimie. Ningependa kuwasalimu Bwana Salim Agili wa Jordan na Bwana Mbarouk Msabah. Na nigependa tu kuuliza kama kalenda za mwaka 2012 zipo, kwani sijapata hata moja, kwasababu kalenda zenu huvutia machoni mwetu, natumai mtanitumia moja, na nitawashukuru sana, nawaombea maisha marefu, ahsante sana.

    Shukurani nyingi sana msikilizaji wetu Ramadhan Hamisi kwa barua yako, kwanza tumefurahi kwa kututaarifu kuwa umepata jarida la daraja la urafiki tulilokutumia. Lakini kuhusu kalenda za mwaka 2012 kwa sasa itakuwa vigumu kukutumia kwani mwaka ndio unaelekea kumalizika, na hata tukikutumia itachukua muda mferu kukufikia, hivyo tungeomba ustahamili hadi tutakapotoa kalenda za mwaka 2013. ahsante sana.

    Na sasa tunawasomea ujumbe kutoka kwa wasikilizaji wetu wanaotembelea tovuti yetu, msikilizaji wetu Xavier L. Telly-Wambwa wa S.L.P 1993-50200, Bungoma, Kenya anasema ni vyema sana kumjua huyu mwandishi na hebu Mola azidi kumbariki kwa usikivu wake wa CRI. Asante.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Xavier L. Telly-Wambwa kwa maoni yako mafupi, na kukujibu ni kwamba ungemtaja huyo mwandishi uliyemkusudia kwani kwa kufanya hivyo tungeweza kufikisha ujumbe huu kwake, hata hivyo tunapokea dua zako, ahsante sana.

    Na mwisho tunawaletea maoni kutoka kwa Madjid Sage baruapepe yake ni birashmadj@yahoo.fr anasema mimi husikiliza kwa kiwango kikubwa idhaa ya kiswahili ya redio China kimataifa, kwa kuwa mimi ni mtangazaji wa habari kwa kiswahili muda mrefu toka mwaka 1997, wakati huu nimestaafu sina kazi lakini nilikuwa napendekeza kujiunga nanyi katika kuripoti habari muhimu zilizojiri hapa nchini Burundi-Bujumbura au kama kuna uwezekano wa mimi kuja kujinoa bongo katika upashaji wa habari huko nchini china nipo radhi kuja pasina hofu yeyote ile. Nakutakieni kila la heri na fanaka katika utendaji wenu kazi.

    Tunakushukuru sana msikilizaji Madjid Sage kwa maoni yako ila kwa sasa bado hatujahitaji mtu wa kuripoti ama kuja huku, lakini endapo tutahitaji mfanyakazi, tutakupasha habari, na tutazingatia ombi lako, mwisho tunakuomba uendelee kusikiliza matangazo yetu na kutuma maoni yako.

    1 2
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako