• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 1211

    (GMT+08:00) 2012-12-19 15:36:39
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Shaha Pigigi S.L.P 701422 Shanghai China anasema inapata barua ya tatu sasa tokea nilipoanza kutuma lakini sijawahi kupokea majibu yoyote. Kwani mimi ni msikilizaji mzuri sana wa CRI.

    Ukweli ni kwamba nimevutiwa sana na mpangilio wa vipindi vyenu pamoja na matangazo yenu kwa ujumla, kwani redio pekee inayonipatia habari za kiuchumi za Afrika Mashariki, pia ninavutiwa sana ninaposikia mahojiano na viongozi mbalimbali wa Afrika mashariki. Na kubwa kati ya yote hayo ni darasa la Kichina, hivyo ningeomba mnitumie vitabu vya kujifunza kichina pamoja na CD zake. Mwisho nawatakia kila la heri watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa, ahsante sana.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Shaha Pigigi kwa barua yako kwanza tunakupa pole sana kwa kutopata majibu ya barua zako za awali, nasi tunafikiri kuwa labda njia uliyokuwa ukitumia ndio iliyosababisha kutotufika barua zako, tunakuomba safari nyingine utakapotuma barua tumia anuani yetu moja kwa moja. Na kuhusu vitabu tutajitahidi kukutumia ili uweze kujifunza zaidi kichina, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa Mutanda Ayub Sheriff wa Bungoma Kenya naye leo ametuandikia shairi zuri hapa la kuwaombea dua watu wa Tana River mola awape amani na anasema hili shairi lisomwe kwa minajili ya kuleta amani na utulivu katika eneo la Tana river nchini Kenya.

    Nimepata fadhaiko,wakenya wanachinjana,

    Mipaka yao kivuko, karibu na mto-Tana,

    Sasa wana sumbuko,kukicha wanawindana,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River

    Kwenye mji wa Riketa,eneo la River-Tana,

    Jamii zilipoteta,na watu wakauana ,

    Havitawafaa vita,ni bora kuridhiana,

    Mola wape amani, wenzetu wa Tana-River,

    Wapokomo na Oromo,haifai kupigana,

    Wagare na nyie mumo,ng'ombe munaibiana,

    Munadungana machumo,badala ya kupendana,

    Mola wape amani, wenzetu wa Tana-River,

    Mmechomeana nyumba,sasa makao hamuna,

    Wacheni hiyo kasumba,Nuhu nasema bayana,

    Hata mkitia ndumba,ni dhambi kwa maulana,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River,

    Naomba muwe wapole,muwache kumalizana,

    Wanawake wafilile,shingo mumechanachana,

    Na watoto vilevile,huruma hamukuona,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River,

    Fanyeni mtagusano,mueze kuelewana,

    Muitishe mkutano,muuweke muamana,

    Pasiwe na mivutano,mizozo ama hiyana,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River,

    Isiwe mmechochewa,kwa kujaliwa fitina,

    Na sasa mmepagawa,maisha hayana maana,

    Tubuni kwake moliwa,na wema mtauona,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River,

    Hapa nafunika kawa,nikimuomba Rabana,

    Muweze kunielewa ,na muwache kupigana,

    Maisha ndio ngekewa alotupa maulana,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River.

    Nahisi kizalizali mwenzenu nimesonana,

    Nawaomba tafadhali ,wacheni kumalizana,

    Bora mngataamali,watu wema hupendana,

    Mola wape amani,wenzetu wa Tana-River.

    Shukran nyingi sana msikilizaji wetu Mutanda Ayub Sheriff kwa barua yako yenye shairi zuri, nasi tunapenda kuungana nawe kuwatakia amani na utulivu wa watu wa Tana River, Kenya na dunia nzima, ahsante sana.

    Sasa tunawaletea ujumbe tuliotumiwa na wasikilizaji wetu kwanza ni Ras Franz Manko Ngogo wa klabu ya Kemogemba anasema ni matumaini yangu kuwa shughuli hapo CRI ni kemkemu kama ilivyo kwetu huku tuna pilikapilika za kuwategeeni masikio kwa kila mnachotuandalia. Kazeni buti msogeze mbele hili gurudumu la matangazo. Kila siku huizuru tovuti yenu. Naiona kama iko sawa na inahitaji vitu vichache vya kuiongezea tu. Msijali tuko pamoja daima.

    Mwisho ni Mary Msigwa barua pepe yake ni marymsigwa754@yahoo.com anasema kuhusu "Tamthiliya ya Kiswahili ya Doudou na Mama Wakwe zake" kazi yenu nzuri ila naomba mnitumie jina la mtunzi wa kitabu, muhariri, dhamira kuu na mwaka wa kuchapwa. asante sana.

    Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu Ras Franz Manko Ngogo na Mary Msigwa kwa barua zenu ila kwa kumjibu Bibi Mary Msigwa kuhusu mtunzi wa tamthilia ya Mao Doudou na wakwe zake anaitwa Wang Linping, mwisho tunawasihi wasikilizaji wetu muendelee kusikiliza matangazo na kututumia maoni na mapendekezo yenu, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako