• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1218

    (GMT+08:00) 2012-12-19 15:38:29
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Wambura M Nyamhanga wa Kemogemba List Club S.L.P 71 Tarime Tanzania, anaanza kwa kusema ni matumaini yangu kuwa hamjambo wafanyakazi wote wa CRI, na mnaendelea vyema na shughuli zenu za kila siku. Mnamo tarehe 20 mwezi wa 9, nilifarijika sana mara baada ya kusikiliza kipindi cha China Machoni mwetu kinachoongozwa na manahodha Pili Mwinyi na Fadhili Mpunji, pia alikuwepo mgeni wa kipindi hicho Evance Mhando. Kipindi hicho kilizungumzia kwa upana zaidi kuhusu lugha ya kichina na namna inavyoenziwa kwa kufundishwa mashuleni kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.

    Hali hii ni tofauti kabisa na huku kwetu Tanzania ambapo masomo yanayofundishwa kuanzia darasa la kwanza hadi la saba yanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili na kingereza kama somo, lakini kuanzia kidato cha kwanza hadi chuo kikuu masomo yote yanafundishwa kwa lugha ya kingereza isipokuwa Kiswahili. Kwa mwenendo huu ndio maana wanafunzi wengi wanajikuta wakifanya vibaya katika masomo yao hasa pale wanapojiunga na masomo ya sekondari kwani lugha ni ngeni kwao.

    Ingekuwa ni vyema zaidi endapo serikali ya Tanzania ikapanga lugha kama vile, kichina, kingereza, kifaransa, pamoja na Kiswahili, zifundishwe kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu, kwani kufanya hivyo kungeleta mabadiliko makubwa zaidi, katika sekta ya elimu nchini Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla. Siikosoi sekta ya elimu wala serikali ya Tanzania bali huo ndio mtazamo wangu, ahsante sana,

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Wambura M Nyamhanga kwa barua yako yenye ushauri mzuri. Lakini kwa vile sisi huku sio serikali ya Tanzania hatutaweza kukujibu vizuri ila tunakushauri ingawa vyema kama ushauri wako huo ukauwasilisha mahali husika kwani ni mzuri sana. Ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Leornad Mwangu Macharia wa S.L.P 73-30301 Nandi hills Kenya, naye anasema mimi kama msikilizaji wenu wa dhati, nachukua fursa hii kuwapa heko na shukran nyingi mno kwa kazi nzuri na ya maana sana mnayowatendea wasikilizaji wenu, kwa kuwatumia zawadi mbalimbali mara kwa mara na pia hata kuwatumia kadi za salamu na bahasha zilizolipwa kama hizi zangu ahsanteni sana.

    Nikiongeza pia nawashukuru sana kwa kunitumia jarida la daraja la urafiki lisemalo maadhimisho ya miaka 70 ya CRI. Zaidi ya hayo kwasababu nyinyi CRI ni watu wenye ukarimu mwingi kwa wasikilizaji wenu, nawaomba mnitumie majarida zaidi yanayoelezea kwa kina kuhusu kituo chenu cha CRI na yanayohusu maendeleo ya utamaduni wa China kwa ujumla. Hii ni kwasababu kupitia hayo majarida nitaweza kufahamu na kuIelewa zaidi China na siku moja Mungu anijaalie niweze kuizuru nchi hiyo. Ahsanteni sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Leornad Mwangu Macharia kwa barua yako, kwa kweli kama ulivyosema CRI inajali sana wasikilizaji wake kwa kuwashirikisha kwenye mambo yetu mbalimbali ikiwemo chemsha bongo. Kuhusu majarida tutajitahidi kukutumia endapo tutoa mapya, ahsante sana.

    Barua nyingine ni ya msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi wa Eveready Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anasema ningependa kutoa tathmini yangu ya uhusiano na urafiki wangu na hii idhaa ya Kiswahili ya CRI hususan mwaka huu wa 2012 unaoelekea kumalizika, kwanza kabisa natoa pongezi na shukurani maradufu kwa CRI kutokana na juhudi zake za kuimarisha uhusiano mwema na vile vile kutambua wasikilizaji wake kwa kila hali.

    CRI kimekuwa chombo ambacho ni nguzo muhimu na tena thabiti katika ustawi wa mifumo mipya ya kutoa habari zilizo sahihi na ambazo zinakwenda na wakati. Ukweli ulio wazi ni kuwa CRI imetumia kila aina ya ngazi kuelimisha ulimwengu kuhusu China ni nchi yenye mfumo gani na wachina ni watu wa aina gani. Chombo hiki kimekuwa kielelezo bora kwa kuhakikisha wasikilizaji wake wanaelimika na maswala mbalimbali, kupitia majarida kama vile China Today na Daraja la Urafiki, ambayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa wa kuitambua China na maendeleo ya wachina.

    Chombo hiki cha CRI ni chombo cha pekee kinachowashirikisha wasikilizaji wake kwa mashindano mbalimbali ya chemsha bongo kisha kuwazawadia tuzo nyingi ikiwemo safari ya kuzuru China. Huu sio uvumi tu bali ni ukweli unaoshuhudiwa kila mara. Ninapofunga ukurasa huu ningependa kuwapongeza na kuwashukuru zaidi wasikilizaji wenzangu kote duniani, kwa kuendelea kuwa mabalozi wema wa CRI. Juhudi na bidii zenu zinatambuliwa sawasawa na CRI, endeleeni hivyohivyo, ahsanteni.

    Shukurani nyingi sana msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi kwa barua yako ya tathmini. Sisi tunafurahi sana tukiona wasikilizaji wetu wanashirikiana nasi kwa hali ya juu, na kuthamini juhudi zetu za kuwa pamoja nao na kuwashirikisha kwenye mambo mbalimbali. Tunakuombeni muendelee kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni yenu, ahsante sana.

    Mwisho ni ujumbe tuliotumiwa na msikilizaji wetu Ireneus Komba wa Dar es salaam, Tanzania kupitia kwenye tovuti yetu, anasema maoni yangu ni kuhusu makala kwenye tovuti "Wanafunzi wa lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China" kiukweli nimefuatilia kwenye Televisheni, nimependezwa na hiki chuo cha China, nawatakia mafanikio mema. Ahsante sana.

    Shukran sana msikilizaji wetu Ireneus Komba kwa ujumbe wako mfupi, ni kweli chuo hicho kinafundisha kozi mbalimbali ikiwemo Kiswahili, wachina wengi wanaopenda kujifunza lugha ya Kiswahili huenda chuoni hapo na viniginevyo vya hapa Beijing, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako