• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 1225

    (GMT+08:00) 2013-01-04 17:03:25
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Wilson Akhusama wa S.L.P 2191 Kakamega Kenya, anaanza kwa kusema mimi kama shabiki wenu sugu wa CRI, ningependa kumshukuru mkurugenzi wa CRI na watangazaji pamoja na wafanyakazi wote wa redio China kimataifa katika idara tofauti. Shukurani nyingine ni kwa kurudisha matangazo yenu muda wa saa nne usiku na pia kunitumia fulana kama zawadi ya kushinda chemsha bongo.

    Sasa ninaloomba kwenu ni kwamba mniletee maswali mengine, jarida la daraja la urafiki, CD za kujifunza kichina na kunialika China kuja kutembelea. Kadi zenu za salamu sasa ni nzuri kuliko za zamani nahitaji nyingine nyingi. Mwisho naombea kwa Mungu aibariki Kenya, CRI na wafanyakazi wake wote, ahsanteni sana.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Wilson Akhusama kwa barua yako, nasi tunakwambia usiwe na wasiwasi kwani tukitoa maswali mapya ya chemsha bongo tutakutumia, pia tumeshatoa taarifa kwa wahusika ili uweze kutumiwa CD na jarida la daraja la urafiki, mwisho tunakuomba uendelee kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo, ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Omari Athumani wa S.L.P 4608 Dar es salaam Tanzania, anasema natumai kuwa mnaendelea na shughuli mbalimbali hapo studio ili kuhakikisha mnatupatia wasikilizaji wenu habari kemkem na za kusisimua.

    Pia napenda kutumia nafasi hii kujipongeza mimi mwenyewe kwa kupata nafasi ya tatu kwenye chemsha bongo kuhusu maadhimisho ya miaka 70 ya CRI mwaka 2011, pia pongezi hizi ziende kwa wasikilizaji wote waliopata nafasi ya kwanza, pili, tatu na nafasi maalumu ya kutembelea China.

    Zaidi naishukuru CRI kwa kunipatia zawadi ya CD ya jifunze kichina na vitabu vya kutambua herufi na matamshi lakini pia nimepokea kijarida kinachoonesha watangazaji, washindi wa nafasi maalumu pamoja na zawadi ya kioo na kalamu yenye kuvutia. Hivyo ongezeni muda katika vipindi hasa cha jifunze kichina ili tuweze kupata zaidi uhondo wa vipindi vya vya CRI. Nawatakia kazi njema na makaribisho mema ya mwaka mpya.

    Kwanza tunakushukuru sana msikilizaji wetu Omari Athumani kwa barua ya shukurani. Pia nasi kwa upande wetu tunakupongeza kwa kupata nafasi ya tatu kwenye chemsha bongo mwisho nasi pia tunakupa heri ya mwaka mpya wa 2013 ahsante sana.

    Barua ya sasa inatoka kwa msikilizaji wetu Busolo W Daniel wa S.L.P 1584-50200 Bungoma Kenya, anasema ningependa kuwapongeza wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa na kuwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mimi ni shabiki mgeni ingawa sio sana lakini nafurahishwa sana na matangazo yenu, hivyo ningependa mnikumbuke kwani mimi nimekuwa nikifuatilia matangazo yenu kwa muda mrefu. Nikiwa kama mwanafunzi wa shule ya upili kidato cha nne natarajia kuwa nitafaulu mtihani wangu ili nami pia nijiunge na taaluma ya uandishi wa habari. Mwisho natumai tutaendelea kuwasiliana kwani huu ni mwanzo tu wa kujuana mimi nayapenda matangazo yenu sana. Mungu awabariki ili tuwe nanyi kwa muda mrefu, ahsante sana.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Busolo W Daniel kwa barua yako. Kwanza tunakuombea kwa Mungu ufaulu vizuri mtihani wako, ili uendelee na masomo ya juu zaidi, lakini pia ukumbuke bila jitihada hutofanikiwa kwa hiyo kaza buti upate mafanikio katika masomo yako, ahsante sana.

    Na mwisho tunawsomea ujumbe tuliotumiwa na wasikilizaji wetu kupitia kwenye tovuti yetu kwanza ni msikilizaji wetu Sali Bunzali Sali wa Kahama Shinyanga Tanzania, anasema kwanza nitangulize shukrani zangu za dhati kwa uongozi wote ulioko hapo radio China kimataifa. Mimi Sali Bunzali Sali lakini watanzania huniita waziri wa shida na mipango ya ghafla. shukrani zangu nitaendelea kuzitoa pia kwa serikali ya china kwa kazi inazozifanya, mpaka kufikia leo hii nchi zote zinajivunia na mipangilio mizuri ya serikali, mfano hapa kwangu nina vitu vingi vya mchina, familia yangu inatumia kwaraha na furaha kimatumizi ya nyumbani, Pikipiki zangu ziko 2 zote kutoka China, jembe la kulimia la ng'ombe ninalo la mchina. Mafuta yataa sinunuwi kwa miaka mitano sasa kwani natumia taa za mchina, simu zote hapa kwangu zipo 5 za mchina, radio ninayotumia kusikiliza matangazo na matukio yote ya ulimwengu ni mchina. Kwahiyo nina kila sababu ya kuishukuru serikali ya China. Kwa yote haya wala sio yako kwangu tu, bila shaka nikote duniani. mengi ninayo yakuweza kuipongeza CRI. Nihitimishe kwa kuwashukuru watangazaji, Mungu azidi kuwapa nguvu na ubunifu zaidi mkishirikiana na serikali ya China, ahsanteni.

    Naye Mohamed Khamis wa Zanzibar, Tanzania anasema naomba mtuwekee peji ndani ya facebook kama inawezekana ili tupate kupata habari na pia kuchangia chochote maana kuna siku hatupati kusikiliza radio, kazi njema.

    Mwisho ni ujumbe kutoka kwa Ulrick Kyara Mweka anasema tunaomba tamthilia ya Mao Dodo na wakwe zake iwekwe kwenye YouTube, ahsante sana.

    Tunawashukuru wasikilizaji wetu wote mliotoa maoni yenu kupitia kwenye tovuti yetu, lakini tunapenda kumjibu Bw. Mohamed Khamis kuwa kutokana na sera za serikali hivi sasa facebook imefungwa na haipatikani kabisa nchini China, hivyo hata kama tutaanzisha ukarasa itakuwa vigumu kuwapata wasikilizaji wetu, kwa hivi sasa unaweza kutumia tovuti yetu hadi hapo itakapofunguliwa, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako