• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0108

    (GMT+08:00) 2013-01-18 15:28:33
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Yohana Marwa wa Kemogemba Club S.L.P 71, Tarime Mara Tanzania. Anaanza kwa kusema wapendwa ndugu zangu wafanyakazi wa Idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, wakati huu tunapoelekea sikukuu za krismas na mwaka mpya napenda kuwatakia sikukuu njema ziwe za heri na mafanikio pamoja na kumshukuru na kumwomba Mungu atuvushe salama ili tuuone mwaka wa 2013 wote tukiwa wenye afya njema na kuendelea kuchapa kazi zetu za kila siku kila mmoja kwa nafasi yake pale alipo.

    Tunapoumaliza mwaka wa 2012 tunapaswa kukaa chini na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyotulinda hadi kufika hapa tulipo sasa, kwani ni wengi walitamani kufika hapa tulipo leo lakini haikuwezekana bali kwetu sisi hatuna budi kumpa Mungu shukrani zetu kwa yale yote aliyoyafanya juu yetu. Mwaka ndio huo unaishia na sisi tujaribu kutafakari jinsi mwaka ulivyoanza tulijiwekea malengo yapi na tumejaribu kuyafanya kwa kiwango gani na pengine tumeshindwa wapi ili tuongeze jitihada kwa mwaka wa 2013 tuyatekeleze kwa vitendo na sio kwa maneno tu, maana wahenga walinena maneno matupu hayavunji mfupa.

    Kadhalika CRI ijitahidi kutuboreshea matangazo kwa mwaka huu zaidi ya hapo ilipo sasa ijapokuwa matangazo ni mazuri lakini kumbuka kuwa mshindani ni yule anayekubali kwenda na wakati uliopo. Naungana na maelfu ya wasikilizaji wa CRI idhaa ya kiswahili popote pale walipo kuiombea heri na mafanikio mema idhaa yetu hii ya Radio China Kimataifa ili iendelee kufanya vyema katika nyanja hii ya utangazaji kitaifa na kimataifa kama tunavyoyapata matangazo ya CRI kupitia njia mbalimbali kutegemea na msikilizaji mwenyewe. Nipo pamoja nanyi ndugu zangu wala msiwe na shaka kila la kheri.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Yohana Marwa kwa barua yako ya kututakia heri ya mwaka mpya. Kwanza tunamshukuru Mungu kwa kuumaliza mwaka 2012 kwa salama na kuingia mwaka 2013 kwa amani na furaha. Ingawa mwaka 2012 ulikuwa na misukosuko mingi lakini tunategemea mwaka huu utakuwa wenye mafanikio makubwa, hususan kwenye shughuli zetu mbalimbali tunazozifanya. Nasi idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa, tunasema mwaka huu tutajaribu kurekebisha pale tulipokosea mwaka uliopita. Na mwisho tunawatakia wasikilizaji wetu wote heri ya mwaka mpya, ahsanteni sana kwa kutuunga mkono katika miaka yote iliyopita.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Xavier L. Telly-Wambwa wa S.L.P 1993-50200, Bungoma Kenya, anasema ujumbe kuhusu "Shule ya msingi ya bweni mlimani " Shule hii ni ya maana sana katika sehemu hiyo. Mimi ningelipenda kuomba waziri wa elimu wa China kuchukua hatua kabambe ili watoto wapendwa wawe na elimu kwa kupitia misaada kutoka kwa Wachina. Kwani siku Moja viongozi wengi watatoka katika Mkoa huo. Nawaombea mafanikio ya kielimu na mafanikio zaidi na pia nami ninatoa mchango maalumu kwa kuwaombea jamii na watoto hawa kwa Mungu waweze kuwafungulia milango ya ufanisi. Xie Xie

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Xavier L. Telly-Wambwa kwa barua yako, waswahili wanasema elimu ni ufunguo wa maisha, tunaamini shule hiyo siku moja itatoa viongozi wazuri, hususan kama watoto watatayarishwa vizuri kimasomo. Tunawaombea maendeleo makubwa katika masomo yao ahsante sana.

    Davis Mpuso Sekomu S.L.P 370, anasema kwa vile tunaelekea mwisho wa mwaka, maoni yangu ni kwamba, ningependa matangazo yenu yasikike kwa masafa ya shortwave, kwani sisi tunaotegemea masafa ya medium wave toka Kenya mara nyingine hatuyapati kutokana na mambo mengine yanayojitokeza kama mpira na vipindi vingine. pia muongeze radio washirika hizi za FM. Na muda huo saa nne wengi wanakuwa wamelala. nawatakia maboresho mema tunapoanza mwaka mpya. xie xie na. vitabu nilipata vya JIFUNZE KICHINA.

    Nawe tunakushukuru sana msikilizaji wetu Davis Mpuso Sekomu, kwa barua yako, lakini kuhusu matangazo itakuwa vigumu kubadilisha muda, kwani wasikilizaji wetu wengi wanapendelea muda huo kwasababu wengi wao wanakuwa wamesharudi nyumbani kutoka kwenye pilika za kila siku, hivyo tunaomba utuwie radhi, asante sana.

    Barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Mogire Machuki wa Bogeka Village S.L.P. 646 Kisii Kenya anasema salamu za dhati na mwaka mpya ziwafikie wote wahudumu wa CRI. Nina furaha kusikia kupita Redio China Kimataifa kwamba Mama Chen Li Yiang tayari ametuzwa miongoni mwa kumi bora kutoka China kama Mchina ambaye ametoa mchango mkubwa sana wa kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika. Ni furaha sana kupata taarifa za aina hii na kweli wasikilizaji wengi wa CRI hapa Kisii wamepokea taarifa hizi kwa furaha na kwa niaba yao wameniomba nikuletee salamu za pongezi. Kweli Mama Chen kapendwa na wengi. Kila la kheri kwa kufikia hilo na pia kuendelea kuiongoza Idhaa ya Kiswahili ya CRI japo umestaafu. Sauti yako bado twaithamini na kila kukicha tunakuombea afya njema ili tuendelee kupata huduma yako. Ni matumaini yangu kuwa ushirikiano uliopo kati ya CRI na wasikilizaji wake utaendelea kuimarika zaidi mwaka 2013. Nawatakia kila lililo jema na udumu urafiki kati yetu. Shukrani。

    Nasi tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mogire Machuki kwa barua yako ya pongezi, kwa kweli hata mimi pia nimefurahi sana kupata tuzo hiyo ambayo inaonesha jinsi mchango wangu wa kudumisha urafiki kati ya Afrika ya China unavyothaminiwa. Na hata wafanyakazi wenzangu pia wamefurahi kuona tuzo hiyo imekuja kwenye idhaa yetu ya Kiswahili, kweli tunaona fahari kubwa sana, hapa ni lazima nawashukuru wasikizaji wetu wote popote pale walipo ambao kila mara mnatutia moyo na kutuunga mkono na kututia moyo kuchapa kazi kwa ajili yia kuongeza urafiki kati ya China na Afrika. Mwisho napokea pongezi hizo kwa mikono miwili, na kuwaomba wasikilizaji wote tuendelee kushirikiana zaidi ili urafiki wetu udumu milele, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako