• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0226

    (GMT+08:00) 2013-03-11 14:40:07

    Bila shaka yoyote Nyoka ni moja kati ya alama muhimu na yenye historia kubwa na ya muda mrefu katika maisha na utamaduni wa Kichina na eneo zima la Mashariki ya Mbali, kwa vile tafsiri na maana ya mnyama huyo katika mzunguko wa kalenda ya kijadi ya Kichina ni mkubwa sana. Kwani mzunguko huo umekuwa ukitofautisha Nyoka tokea miaka mingi iliyopita ambapo inapowadia mwaka wa Nyoka huwa ni nyoka wa aina fulani kama vile Nyoka wa Mbao, Nyoka wa Moto, Nyoka wa Udongo, Nyoka wa Dhahabu na Nyoka wa Maji, hawa wote ni nyoka wanaotafsiriwa kwa maana tofauti katika kila mzunguko wa wanayama 12 unapofikia mwaka wa alama ya Nyoka, jambo ambalo mimi binafsi nalihisabu ni kama hazina kubwa ya utamaduni wa kijadi wa Kichina juu ya mwenendo huu wa kufuata kalenda zao.

    Bila shaka ni matarajio yangu kwamba mwaka huu nao utakuwa ni mwaka wa baraka, heri na mafanikio kwa Wachina wote na Walimwengu kwa ujumla katika kujiletea maendeleo na ufanisi .

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk kwa barua yako ya pongezi na heri ya mwaka mpya, tunamshukuru mungu kwani tumeuingia kwa usalama mwaka wa nyoka, tunatumai kuwa malengo yetu yote tuliyoyaweka kwa mwaka huu yatatimia. Ahsante sana

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Choma wa Choma au kamanda wa mashambulizi ya Salamu S.L.P 108 Mawamkulu, Mpanda, Tanzania anasema mimi nawashukuru, Radio China kimataifa, kwa vipindi mbali mbali kuazia Salamu na jifuze kichina, cheche zetu, na kuelimisha. mapishi mbali mbali, chemsha bongo, na matangazo bora. Anauliza je? upo uwezekano wa kunitumia kalenda. ya mwaka 2013 pia na picha za watangazaji, maana hizo ni kumbukumbu za kesho, itakua simulizi ya kihistoria kwa wajukuu zetu karne ijayo. Kwa mfano kama babu wa baba yangu alikua mtu maarufu sana. Alikua anaitwa Njishosha mwana malundi, yeye mpaka sasa historia yake bado ipo.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Choma wa Choma kwa barua yako fupi, kuhusu ombi lako la kutaka kutumiwa kalenda tutajaribu kuongea na muhusika ili aweze kukutumia, ila kuhusu picha za watangazaji hatuwezi kukuahidi, ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Mogire Machuki wa Bogeka Village S.L.P. 646, Kisii Kenya anasema natuma salamu za dhati kutoka Kisii Kenya nikiwa na wingi wa matumaini kuwa mko shwari kabisa. Aidha nina furaha pamoja na marafiki zangu kutuma salamu zetu za dhati hususani za mwaka mpya wa jadi wa Kichina mwaka huu ukiwa ni wa Nyoka. Binafsi nawatumia raia wote wa China salamu za kila la kheri kwa vile China imekuwa na urafiki wa muda mrefu na wa kuaminika na taifa langu kenya. Kheri ya mwaka mpya kwa taifa la China. Nina imani kwamba CRI itakuwa na mengi ya kutufahamisha kuhusu sherehe hii ya kufana zaidi duniani kote. Shukrani na kila la kheri kwa mara nyingine tena.

    Shukran za dhati Bwana Mogire Machuki kwa barua yako, kwa kweli tunapokea kwa furaha heri ya mwaka mpya, tunatumai utakuwa umefurahia mfulululizo wa vipindi vya mwaka mpya tulivyowaletea, ambavyo vimekusanya mambo mengi kuhusu mwaka huu wa nyoka. Ahsante sana.

    Na mwisho tunawaletea shairi kutoka kwa msikilizaji wetu James Mutwiri ambaye pia anajiita "Malenga Msifika" shairi lake linaitwa

    KWAHERI 2012, KARIBUNI 2003.

    Narai murwa kibali, nijitume jukwaani,

    Naja imi fulifuli, nifumbue la moyoni,

    Kawa mwaka idhilali, loeneza visirani,

    Vioja vikakabili, kabaki wazi vinywani,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Swala lo nyeti muhali, lilifurika nchini,

    Mini-sketi skuli, wengi kawa kimakoni,

    Uhalifu najadili, pakubwa kushika kani,

    Wanaume kikatili, bibi kawapiga shani,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Zikawa nomi ajali, ndugu zetu kaburini,

    Mitihani walofeli, kadha kitanzi jamani!

    Migomo iso halali, kalola yetu machoni,

    Ikavuruga shughuli, za uchumi sadikini,

    Kwaheri mwaka 2012.

    Bunge si afadhali, kawa nuhusi yakini,

    Sarakasi mbalimbali, zikajiri hadharani,

    Katiba mpya dalili, za kubadili bungeni,

    Kundi la MRC kamili, katukera niamini,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Mapigano wasojali, kayanzisha mipakani,

    Wakenya mamia kweli, kafa haya mautini,

    Wakayachoma manzili, wizi mifugo baini,

    Shanga mlo akili, polisi kabwagwa chini,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Saitoti, Ojode hali, lowafisha ya huzuni,

    Michuki, Karume tuli, katuliya pa peponi,

    Shikuku lokuwa nguli, mteteya wa amani,

    Nawengine ni nakuli, katwaga wa buriani,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Wanasiasa lo mali, kaenda miunganoni,

    Ndoa syasa kakubali, ili kuingia bungeni,

    Al– Shabaab majangili, kalipuwa kanisani,

    Marufuko kalikali, Kenya kawa gharikani

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Twakusihi E Jalali, utuvushe muakani,

    Tusahau mishikeli, ilotughasi nyoyoni,

    Rehema sizo kalili, zitupe kuntu amani,

    Tamaa nitie kufuli, Wallah! Tena sineni ,

    Kwaheri mwaka wa 2012.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu James Mutwiri kwa shairi lako murua kabisa, tunatumai kuwa wale mashabiki wa mashairi pia nao watahamasika na kuandika zaidi, mwisho tunawaomba wasikilizaji wetu waendelee kusikiliza matangazo na vipindi vyetu na kuweza kutoa maoni na mapendekezo ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako