Wataalamu nchini Kenya wanatabiri kuwa, serikali mpya ya Kenya haitaleta mageuzi makubwa kwenye sera zake za uchumi na za kimataifa, bali itaweka msisitizo kwenye kuongeza uhusiano na nchi zinzoinuka kwa kasi kiuchumi duniani.
Profesa Munene Macharia, mtaalam wa masuala ya uhusiano wa kimataifa amesema, hakuna matarajio kuwa rais mpya Uhuru Kenyatta wa Kenya, aliyekuwa waziri wa fedha kwenye serikali iliyopita ya rais mstaafu Mwai Kibaki, atafanya mageuzi makubwa ya sera za uchumi, lakini anatazamiwa kuongeza ushirikiano na nchi jirani za Afrika Mashariki. Amesema sera za uchumi huenda zikasisitiza zaidi sera zitakazoleta utajiri zaidi ili wananchi wa Kenya wapate kunufaika kwa pamoja na rasilimali za nchi yao. Macharia anasema, baada ya kufanya kazi kwenye serikali ya Mwai Kibaki, ni rahisi kwa Uhuru Kenyatta, mtoto wa muasisi wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta, kuendeleza sera za uchumi zilizopo sasa. Aidha, mtaalamu huyo amesema, ilikuwa ni rahisi kutabiri kuwa Kenyatta ataendeleza mpango wa Vision 2030 iliyoasisiwa na rais Kibaki. Mpango huo unalenga kuifanya Kenya kuwa nguzo ya uchumi wa kanda ya Afrika Mashariki kwa kuwa kituo cha mawasiliano, mambo ya fedha, na upashanaji habari. Mpango huo unaonyesha kuwa Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini zimekubaliana kwa pamoja kutekeleza ujenzi wa bandari nyingine mjini Lamu, hivyo kuwa na aina mpya ya usafiri kwa kanda ya Afrika Mashariki.
Mtaalamu huyo amesema anatarajia jumuiya ya kimataifa, hususan Marekani na Umoja wa Ulaya kuchukua tahadhari kubwa kwenye mtazamo wa uhusiano wa kidiplomasia na Kenya. Hali hii inatokana na kuwa rais Kenyatta na makamu wake William Ruto wanatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC kuhusika na machafuko yaliyotokea nchini Kenya mwaka 2007/2008 yaliyosabaisha vifo vya watu zaidi ya 1,300 na wengine wengi kupoteza makazi yao. Viongozi hao wanatuhumiwa kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji, kutumia nguvu kuondoa watu, pamoja na ubakaji. Wanasiasa waliobobea wanasisitiza kuwa, keshi hiyo dhidi ya Kenyatta na Ruto itakuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi na siasa za Kenya za siku zijazo. Mahakama hiyo ambayo makao yake makuu yako mjini The Hague, inawataka Kenyatta na Ruto kuwepo mahakamani wakati kesi hiyo itakapotajwa kwa mara ya kwanza, tarehe 28 mwezi ujao na Julai 9.
Wachambuzi wanaeleza kuwa, kesi hizo zinaweza kuchukua muda mrefu kusikilizwa, hivyo kuleta hali ya wasiwasi kwa utulivu wa Kenya. Hata hivyo Macharia anatarajia kuwa Umoja wa Afrika utachukua hatua sahihi na kutaja jina la Kenyatta kwenye salamu za pongezi za umoja huo. Amesema kuchaguliwa kwa Kenyatta kunaonyesha kuwa Kenya si nchi inayoweza kuyumbishwa, bali kumeonesha kuwa wakenya wana uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe.
Chini ya utawala wa Kenyatta, Kenya inaonekana kufanya juhudi za kujenga uhusiano mpya na nchi nyingine barani Afrika ambako baadhi ya nchi zinazoinuka kwa kasi kiuchumi zinapatikana. Katika kujibu tuhuma za ICC, Kenyatta na Ruto wamesisitiza tena kuwa Kenya ni nchi huru, na ni haki ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka wao, sawa na katiba ya nchi hiyo inavyoelekeza. Profesa Macharia ameongeza kuwa, itakuwa ni vizuri zaidi kudumisha uhusiano mzuri na nchi zinazoinuka kiuchumi maarufu kama nchi za BRICS, yaani Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini. Amesema nchi hizo zimeonyesha utayari wao wa kuongeza nguvu ya uhusiano kati yao na Afrika, na zimetoa ahadi ya kuendeleza ushirikiano wa kunufaishana. Biashara kati ya Kenya na China, India, na Brazil imekua kwa kiasi kikubwa katika miaka michache iliyopita, na kuchukua nafasi ya washirika wake wa zamani kama Marekani na Uingereza, ingawa nchi zenye nguvu za Magharibi bado zinadhibiti sekta muhimu za uchumi nchini Kenya.
Profesa Macharia amasema, uhusiano kati ya vyama vya Jubilee cha Kenyatta na CORD kinachoongozwa na Odinga unategemea kama wanasiasa watakuwa tayari kuweka mahitaji ya nchi kwanza badala ya ajenda binafsi. Amesema dalili zozote za mgogoro wa kisiasa zinaweza kutoa dalili mbaya kwa wawekezaji wa nje ambao wako tayari kufanya uwekezaji nchini Kenya.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |