• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0423

    (GMT+08:00) 2013-04-23 15:01:03
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa S.L.P 504 Lindi Tanzania, anaanza kusema tafadhali pokea salamu za mwaka mpya wa 2013 kwa wafanyakazi na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa CRI nawatakia furaha na amani mwaka mzima. Mwaka uliopita CRI iliadhimisha miaka 70 ya kuanzishwa kwake, CRI imetoka mbali tangu pangoni mpaka kufikia jijini Beijing na kuendelea na matangazo.

    Mimi katika pekuapekua yangu nilikutana na matangazo ya idhaa ya Kiswahili yakijulikana kama redio Peking, nikifuatana nayo hadi imekuwa redio China na bado naendelea kuwa msikilizaji veterani. CRI imetufahamisha na kutujuvya mengi kupitia vipindi vyake na watangazaji wake mahiri. Naipongeza CRI katika mwaka mpya pia natoa shukrani kwa kunitumia zawadi mbalimbali pamoja na bahasha iliyolipiwa, kadi za salamu na mengine mengi mazuri, ahsante sana.

    Tunakushuru kwa dhati msikilizaji wetu Gulam Haji Karim kwa barua yako fupi, pia kwa kuwa msikilizaji wetu wa zamani yaani miongoni mwa mavetereni wa Idhaa ya Kiswahili. Nasi pia tunakutakia furaha amani na mafanikio katika mambo yako na usikilizaji wako wa idhaa yetu, tunashukuru sana kwa kutuunga mkono kwa muda mrefu, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi wa Eveready Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya anasema ingawa nimepokea nakala yenye maswali yanayohusu shindano la chemsha bongo ambalo limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuadhimisha miaka 70 tangu idhaa hii ya CRI ianze kurusha matangazo yake hewani. Ukweli ni kwamba nimeshalifanya shindano hili kwa njia ya maandishi na kwa kweli mimi limenifurahisha na kunipendeza kwasababu hii ni mara yangu ya pili kushiriki kwenye shindano kama hili.

    Nakumbuka vyema kuwa mnamo mwaka 2006 pia tulikuwa na shindano kama hili lililoadhimisha miaka 65 tangu CRI ianzishwe, ingawa nimeshiriki mashindano mengi ya chemsha bongo yanayoandaliwa na CRI, katika mchakato huo nimewahi kujishindia vyeti viwili ambapo kwa sasa namulika macho yangu kwa ile nafasi maalumu ambayo itaniwezesha kuitembelea China. Ingawa simaanishi sasa lakini kama sio sasa basi hivi karibuni, kwangu mimi hainijalishi ni lini, lakini ipo siku itafika.

    Katika mtazamo wangu hili shindano ama hii chemsha bongo kwangu ni shindano la tisa tangu nijiunge na CRI. Furaha na fahari yangu ni kuwa mingoni mwa wanaoshiriki, na lengo langu kuu ni kushiriki. Hii ndio fursa ya kipekee inayotupa sisi wasikilizaji kujua na kufahamu hisoria ya CRI wahenga walisema ukiviona vinaelea ujue vimeundwa. Tunapoona CRI ikitambaa na kuelekea kote duniani ni ishara kuwa imeundwa na imeundika sawasawa kimatangazo na kiurafiki pamoja na Uhusiano wa karibu na wa kiwenzi. Hongera CRI.

    Shukrani za dhati msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi kwa barua yako, ni kweli tulitoa shindano la chemsha bongo wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa CRI lakini sasa muda mrefu umeshapita, na matokeo yameshatolewa, hivyo kama hujabahatika usichoke kujaribu, hata hivyo tunafurahishwa na moyo wako wa kutokata tamaa, kwani kama ulivyosema kama hukushinda leo unaweza kushinda kesho, ahsante sana.

    Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Epafra Stanley Deteba baruapepe yake ni epst01@hotmail.com anasema leo napenda kujadili habari kuhusu "Botswana kuanzisha Internet ya kasi iliyotolewa na redio China kimataifa ninaendelea kuwapongeza CRI kwa habari motomoto kupitia redio hii na hata kwa njia ya mtandao wa CRI.

    Mimi binafsi ninaendelea kupata habari, napenda kusema kuwa hatua iliyochukuliwa na nchi ya Botswana kuanzisha huduma ya internet ni nzuri sana na italeta tija, hasa ukizingatia kuwa nchi nyingi zinazidi kuendelea kisanyansi na teknolojia, naamini kuwa hata uchumi wa taifa hilo utaendelea kukua kwa sababu watu wa ndani ya nchi hiyo itakuwa rahisi kuwasiliana wao kwa wao na hata nchi nyingine pia kwa urahisi mno. Nchi nyingine hazina budi kujifunza kutoka kwa Botswana.

    Shukran za dhati msikilizaji wetu Epafra Stanley Deteba kwa barua yako, kwa kweli Botswana imepiga hatua kubwa ya kuhakikisha nchi hiyo inakuwa na mawasiliano mazuri na ya haraka hususana kwenye mambo ya internate. Kama ulivyosema huo ni mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo huo. Asante sana.

    Sasa tunawaletea maoni tuliyotumiwa na wasikilizaji wetu kwenye tovuti yetu msikilizaji wetu wa kwanza ni Irene baruapepe yake ni irene@yahoo.com anasema tamthilia ya Doudou na wakwe zake iendelee kwa sababu ni nzuri sana pia inafundisha

    Labui Ubi Fresh anasema kwanza kabisa natoa pongezi sana kwa watangazaji wa CRI na najiskia faraja kuielewa radio yenu. Pili huku nilipo mimi mbali sana nipo ZANZIBAR ila nawasikia vizuri sana nawaomba muandae kipindi cha historia za maraisi ulimwenguni kote

    Issa Saidi baruapepe yake ni issamahamba@gmail.com anasema naipenda idhaa ya kiswahili ya China hasa habari.

    Na ujumbe wa mwisho ni kutoka kwa Kioro Bernard S.L.P 19927 ujumbe wangu ni kuhusu "Tamthiliya ya Kichina"Doudou na Mama Wakwe Zake " kwa kweli ni nzuri sana tumeifurahia familia nzima

    Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu wote mliotutumia ujumbe kwenye tovuti yetu, tunawaomba muendelee kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yenu, ahsanteni sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako