Baada ya kutangaza sera alimalizia kwa kumkabidhi funguo za jengo hilo lenye ghorofa tatu rais Jakaya kikwete na mwishowe kuzuru makaburi ya wataalamu wa China waliofariki Tanzania na kuweka mashada ya maua, ambapo jioni ya siku hiyo aliondoka kwa ndege ya Boeng 747 na kuelekea Afrika Kusini. Namtakia kila la heri kiongozi huyu, ahsante sana.
Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Gulam Haji Karim kwa barua yako kuhusu ujio wa rais Xi Jinping nchini Tanzania. kwa kweli hatua ya rais huyu, kuifanya Tanzania kuwa kituo chake cha kwanza katika nchi za Afrika inaonesha kuwa China inaithamini sana Tanzania na ni marafiki wakubwa sana, sisi kwa upande wetu tunauombea ushirikiano huu uendelee kudumu, ahsante sana.
Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Bi Halima Ijeiza wa S.L.P 14-40602 Ndori Kenya anasema pokeeni salamu zangu za dhati nikitumai hali yenu ni shwari, mimi huku sina neno mbali na kulilia mvua kwani jua sasa limewaka na kusababisha kiangazi kwa zaidi ya miezi mitatu. Nataka kutoa shukrani zangu kwenu kwa kunitumia kadi za salamu ambazo ndizo zimejaa kuliko zile zenye picha, bahasha iliyolipwa pamoja na kalenda ya mwaka huu wa 2013, nashukuru pia kwa mawasiliano ya mara kwa mara baina yetu.
Baada ya hapo ningependa kujua kwanini hamjaanzisha tena shindano la chemsha bongo mwaka huu? Chombo hiki hutuunganisha sisi mashabiki kote ulimwenguni, mbali na kutupa nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali na hata nafasi maalumu. Hata hivyo ninaendelea kufurahia vipindi vyenu mbalimbali. Ahsante sana.
Shukran za dhati msikilizaji wetu Bi Halima Ijeiza kwa barua yako, nasi tunashukuru kwa kuunga mkono, ila kuhusu chemsha bongo kwa sasa bado hatujatoa mpya, ila usiwe na wasiwasi tutakapotoa shindano jipya kila msikilizaji wetu atapata taarifa, ahsante sana.
Sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Sharif wa S.L.P 172 Bungoma Kenya anasema salamu kwa wafanyakazi wote wa CRI, bila kusahau wasikilizaji wote popote walipo, nawasihi mnipe masikio na macho yenu kwa dakika chache. Ningependa kuandika shairi hili kwani imekuwa jambo la kukera sana kwa visa vya wanawake kuwachapa waume zao vinaendelea hapa mjini hasa mkoa wa kati. Ninaamini kuwa sio vyema watu wapendanao kupigana kwa kiwango cha kuwaacha wenzao na majeraha mabaya ya moto, panga au kisu, hii yote ni dhambi, maovu na makosa makubwa. Waume mmewakosea nini wake zenu, na wewe mke ni vyema kweli hivyo mnavyofanya.
Kwa jina lake jalia, muumba aso na ila
Kwa ulingo najitia, kukemea waso mila
Pengine watasitia, kukemea fadhila
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Najua mke ni nguzo, kwa myumba ili kufaa
Husimama kwa mkazo, msingi wake ni bwana
Pindi huwa ni tatizo, msingi napoachana
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Haya nisingemaizi, ni mambo Kenya ya kati
Ni mke au jambazi, ama mnatuzwa vyeti
Mnaikata mizizi, na uzazi una kiti
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Mmekiuka unyago, dini na utamaduni
Raha mwaipa magongo, kiwa bado duniani
Hata awe ni utingo, mke ni mme nyumbani
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Sitawalaumu sana, pengine mwakosa funzo
Japo mngesoma sana, ndoa ina lake tunzo
Kuoana si hiyana, si kufanya mabonzo
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Sasa nina wausia, enyi mtokeao kati
Ya mume kikuzidia, mchape na lako titi
Mwishowe atasinzia, mbinu ya kumdhibiti
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Na nyumba iso msingi, hatimaye huanguka
Yatakutatiza mengi, mwishowe kufadhaika
Haikufai kwa wingi, ila unapumbazika
Mke achapaye bwana, ni nyumba iso msingi
Tunakushuru sana msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Sharif kwa shairi lako zuri lenye mafunzo kemkem, ni kweli si tabia njema kwa wanawake kuwapiga waume zao, kwani huo si uungwana hata kidogo, raha ya ndoa ni masikilizano na kama masikilizano hayapo ni vyema kuwashirikisha wazee ili watatue kasoro zilizopo na sio kutwangana mangumi ahsante.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |