Sekta ya utalii ni mojawapo ya kitega uchumi muhimu nchini Kenya na pia kwa mataifa mengi duniani, na wanyama pori ni nguzo muhimu katika utalii. Mataifa mengi yameanzisha harakati za kulinda wanyama pori ambao wako katika hatari ya kuangamia kama vile Ndovu na Faru. Kenya nayo pia haijabaki nyuma katika mapambano hayo, nchi hiyo imezidisha vita dhidi ya uwindaji haramu wa wanyamapori. Kuokana na juhudi hizo, askari 32 wa kikosi cha Wanyamapori nchini Kenya - KWS wamesimamishwa kazi ili kuruhusu uchunguzi ufanyike kutokana na kuongezeka kwa shughuli za ujangili katika mbuga za wanyama. Mark Muli, mwandishi wetu aliyeko Nairobi, Kenya, amefuatilia jambo hilo na anatufahamisha kuwa, wakati akitangaza kusimamishwa kazi kwa maafisa hao mwishoni mwa juma, Mkurugenzi wa KWS William Kibet Kiprono amesema kuwa miongoni mwa waliosimamishwa kazi ni pamoja na maafisa wenye dhamana ya mbuga nchini kote pamoja na maafisa kadhaa wa makao makuu ya KWS. Kiprono anasema kuwa, maafisa hao wametakiwa kukaa nje ya ofisi ili uchunguzi ufanye dhidi yao kutokana na tuhuma za kushirikiana na wawindaji haramu. Aidha, amesema katika maeneo mengi ambayo maafisa hao wamekuwa wakifanya kazi, visa vya uwindaji haramu vimekuwa vikiendelea kuongezeka kila kukicha, jambo linaendelea kuifanya sekta ya utalii ya Kenya kupoteza watalii kutokana na kupungua kwa Ndovu na wanyama wengine wanaoendelea kuangamia kama Faru. Kibet Kiprono Mkurugenzi wa Huduma za Wanyamapori nchini Kenya anasema, maofisa hao wamesimamishwa kazi, sio kwamba wana makosa, bali ni kuruhusu uchunguzi ufanyike ili kujua ikiwa wanaweza kuwa na taarifa zozote kuhusu uwindaji haramu.
Hivi karibuni, Kenya, pamoja na mataifa mengine ya Afrika, yamekuwa mstari wa mbele katika kupiga kampeni dhidi ya uwindaji haramu, jambo ambalo limekuwa likihatarisha kuangamia kwa wanyama muhimu sana katika mataifa haya. Kiprono ameonya kuwa, wale watakao patikana na hatia watafutwa kazi na pia kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Amesema Baraza la mawaziri lilikutana hivi karibuni na kueleza mpango mzuri wa usalama ambao utamaliza uwindaji haramu wa wanyamapori. Amesema Kenya iko imara kabisa, na kutokana na usaidizi wa serikali, anapenda kuwahakikishia ya kwamba siku za wawindaji haramu zinahesabiwa.
Kibet Kiprono amesema kuwa, KWS imeomba kuongezewa bajeti yake kutoka hazina ili kukabiliana na tishio la ujangili na uwindaji haramu katika mbuga za wanyama. Askari wa Wanyamapori – KWS mnamo Januari mwaka huu walimuua jangili mmoja na kuwakamata wengine wawili katika mapambano kwenye Mbuga ya Taifa ya Tsavo na kukamata bunduki moja aina ya G3 na risasi 11, msumeno, na vifaa vingine vya uwindaji haramu kwenye eneo hilo.
Katika harakati za kumaliza uwindaji haramu na ujangili katika mbuga za wanyama nchini Kenya, KWS limeweka kamera za upelelezi kwenye Eneo la Hifadhi ya Tsavo ili kusaidia vita dhidi ya ujangili na uwindaji haramu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Hifadhi ya Wanyama ya Tsavo, Francis Kimani, ni kwamba kamera hizo zenye mionzi isiyoonekana aina ya 'infrared' zimewekwa kwenye maeneo muhimu yenye maji ambako majangili huyatumia kuwashambulia wanyamapori katika mbuga hiyo. Mwaka jana, Kenya ilipoteza zaidi ya ndovu 360 kutokana na uwindaji haramu, ikiwa imeongezeka kutoka 289 mwaka 2011, jambo ambalo linaendelea kuleta wasi wasi katika sekta ya utalii. Mapema mwaka huu, Bodi ya hifadhi za wanyama pori ilitangaza kuwa itaajiri walinzi 500 mwezi Julai mwaka huu kusaidia vita dhidi ya uwindaji haramu na ujangili katika mbuga za wanyama. Kiprono anaeleza kuwa, wanaendelea kufanya kila liwezekanalo kumaliza uwindaji haramu kote nchini. Kibet Kiprono amesema, watawachukua maafisa wa kwanza 500 kutoka kitengo cha utumishi wa vijana kwa taifa kwa mwaka huu wa kifedha, ingawa kuna upungufu wa maafisa takribani 3000. Amesema pia kuwa wanafuatilia kuhusu vifaa vya kisasa kwa sababu wawindaji haramu wameerevuka sana.
Upungufu wa walinzi na fedha ndio mambo ambayo yametajwa kama kikwazo kukumbwa katika vita dhidi ya uwindaji haramu kote nchini.
Mnamo Machi mwaka huu, KWS na wahifadhi maliasili walitangaza teknolojia mpya ambayo itawasaidia waangalizi wa hifadi na jamii kupambana na maovu yote ambayo yamekuwa yakilenga wanyama pori hapa nchini. Kifaa cha Ufuatiliaji na Utoaji ripoti cha Anga kitawasaidia waangalizi wa hifadhi kufuatilia na kutathimini umadhubuti wa jitihada za kupambana na ujangili. Kifaa hiki kinaendelea na kuimarishwa na mashirika mengi ya hifadhi yakiwemo Chama cha Zuolojia cha Frankfurt Ujerumani, Hifadhi ya Wanyama ya North Carolina nchi ya Marekani, Chama cha Hifadhi ya Wanyamapori Duniani, Mfuko wa Wanyamapori Duniani na Chama cha Zuolojia cha London Uingereza.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |