• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mtanzania anayetimiza ndoto yake nchini China

    (GMT+08:00) 2013-07-16 16:54:29

    Siku moja mchana, wakati wa majira ya joto mkoani Zhejiang China, Michael Mwalupindi kutoka Tanzania ambaye anaishi mjini Hangzhou, mji mkuu wa mkoa huo, alipanda treni kwenda Yiwu, kilomita 100 kutoka Hangzhou. Ofisi za kampuni yake ziko Yiwu.

    Mwalupindi amefika ofisi kwake. Simu zake mbili zinaita mara kwa mara. Kabla hata ya kujifuta jasho, alipokea simu, huku akiwasha kompyuta na kupokea fax iliyotumwa na wateja wake.

    Hizi ni kazi za kawaida kwa Mwalupindi tangu aanzishe kampuni yake nusu mwaka uliopita. Mwalupindi, mwenye umri wa miaka 31, anatoka Mbeya, Tanzania, na ameishi nchini China kwa miaka minane. Mwezi Novemba mwaka jana, yeye, mtanzania mwingine Ombeni Nanyaro ambaye pia anatokea Mbeya, na mwenzi wake wa China Bw. Huang Jianqiang, walishirikiana kuanzisha kampuni ya biashara ya nje. Kampuni hiyo iko katika mtaa maarufu wa kibiashara mjini Yiwu. Wageni wengi wameanzisha makampuni yao huko, na mameneja kutoka Afrika kama Bw. Mwalupindi si wachache.

    Ingawa Yiwu si mji wa bandari, lakini zaidi ya makampuni 3000 ya nchi za nje yamefungua ofisi zao huko, zaidi ya wafanyabiashara 15,000 wa nchi za nje wanafanya kazi huko, na kila mwaka wageni zaidi ya laki 3.8 wanakwenda huko kufanya biashara, kati yao, elfu 80 wanatoka Afrika. Bidhaa mbalimbali kama vilr vifaa vya usanii, mapambo, vitu vya kuchezea watoto, vitu vya kiutamaduni, michezo, na bidhaa ndogo za metali zinazouzwa katika soko la Yiwu, zinauzwa tena kote duniani. Mji huo unasifiwa kuwa kituo cha kwanza cha soko la bidhaa ndogondogo duniani.

    Bw. Mwalupindi anasema, kufanya biashara ni ndoto yake tangu utotoni. Mwaka 2005 alikuja China kusomea kozi ya biashara ya kimataifa. Baada ya kuhitimu chuo kikuu, aliamua kutimiza ndoto yake hapa hapa China. Alitembelea miji mbalimbali iliyoko pwani nchini China ili kuona ni wapi anaweza kufanya biashara itakayomletea faida, na aliua kuanzisha shughuli zake mjini Yiwu. Pia alisema, licha ya fursa nyingi za kibiashara mjini Yiwu, sababu nyingine ya kuchagua mji huo ni mke wake ambaye ni mchina, na ni mwenzi wake wakati aliposoma katika Chuo kikuu cha Zhejiang.

    "Mimi nina familia, ndoto yangu ni kufanya kazi Hangzhou, Yiwu na Hangzhou ni jirani, kilomita mia moja kutoka hapa mpaka Hangzhou, kwa treni pengine dakika arobaini."

    Bw. Mwalupindi alisema rafiki yake mzuri wa China pia ni sababu muhimu. Ingawa amejifunza nchini China kwa miaka mingi na kuweza kuongea Kichina vizuri, lakini bado haelewi mambo mengi hapa China, na mke wake ambaye ni mfanyakazi wa kampuni nyingine hana nia ya kufanya biashara, hivyo kufanya biashara peke yake itakuwa kazi ngumu. Alipokuwa akijiuliza ni vipi ataweza kufanya hilo, rafiki yake Huang Jianqiang alimwondoa wasiwasi.

    "Mimi ni mkazi wa Yiwu. Wafanyabiashara wengi hapa Yiwu wanatoka Afrika. Ilikuwa ni bahati tu kwangu kukutana na Michael. Wakati huo mteja wangu kutoka Afrika alifariki hapa China, nilipokuwa nashughulikia mazishi yake, nilikutana na Michael, urafiki wetu ulianzia hapo."

    Miaka mitatu baada Mwalupindi na Huang Jianqiang kukutana, walishirikiana na Mtanzania mwingine, Nanyaro, kuanzisha kampuni yao ya biashara ya nje. Washirika hao wanafanya kazi tofauti, Mwalupindi anashughulikia usambazaji wa bidhaa, Nanyaro ambaye bado hajaolewa anashughulikia kuagiza bidhaa kutoka sehemu mbalimbali nchini China, na Huang Jianqiang anafanya kazi za mawasiliano na uhasibu. Ushirikiano wao umewafanya kama ndugu. Bw. Huang alisema,

    "Wanawasiliana na wateja wa nchi za nje, na nashughulikia mambo ya China. Simchukulii Miachael kuwa mgeni, sisi ni kama familia moja, tunakula, kusafiri, kukaa na kujadili pamoja mara kwa mara. Mimi ni kijana zaidi, baadhi ya wakati ninalalamika mbele yao kama vile wao ni kaka zangu. Tunashirikiana vizuri."

    Wakati mwandishi wetu wa habari alipokutana na Mwalupindi, Ombeni Nanyaro alikuwa amekwenda Guangzhou kuagiza bidhaa. Mwalupindi alishughulikia orodha za usambazaji wa bidhaa kwenye kompyuta yake, huku akijadili na Huang kuhusu safari yao mjini Shanghai siku inayofuata.

    Kampuni yao haijaanzishwa kwa muda mrefu, lakini inaendeshwa vizuri na inapata orodha nyingi za uagizaji. Hivi sasa si kama tu ina wateja kutoka Tanzania, bali pia ina wateja kutoka nchi za maziwa makuu na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.

    Saa kumi jioni, Mwalupindi hana simu nyingi, na wakati wa kunywa chai umefika. Anakwenda sebuleni kunywa chai ya kijani na kupumzika. Alisema,

    "Sisi kwetu tunakunywa chai nyeusi, na mara nyingi ina sukari, na pia muda wa kunywa mara nyingi ni asubuhi. Lakini chai ya China ni tofauti, chai ni sehemu ya mazungumzo kama kwenye biashara. Kwa hiyo utamaduni wa kunywa chai ni tofauti na kwetu. Tunaongea kwa simu, kwa Weixin, unaona, ukiwa China ni lazima ujue Weixin(software inayofanana na WhatsApp), ujue Weibo(microblog), vitu kama hivyo."

    Baada ya kupumzika kidogo, anarudi ofisini na kuendelea na kazi yake mpaka amalize. Saa mbili usiku, Mwalupindi na Huang walikwenda kula chakula katika mkahawa mmoja wa vyakula vya kiarabu.

    Mkahawa huo una mapambano na vyakula vya mtindo wa kiarabu, hivyo unapendwa na wafanyabiashara wengi kutoka nchi mbalimbali walioko mjini Yiwu. Wanapenda kula chakula kitamu huku wakibadilishana habari na kufahamiana. Mwalupindi anaona kuwa, kila mgeni anayefanya biashara mjini Yiwu ana ndoto nzuri, na kama akifanya juhudi, atapata mafanikio mazuri.

    "Napanga Ombeni kusimamia ofisi ya Guangzhou, mwaka huu kwanza tunataka tuone mwelekeo wa ofisi ya hapa. Ikiimarika, tutafungua tawi lingine, kwa sababu hatuwezi kufungua matawi mengi, wakati uendeshaji wa ofisi moja bado hatujaufahamu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako