• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 1029

    (GMT+08:00) 2013-11-05 17:49:55
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk wa S.L.P 906 Al Hamriya PC131 Oman, anaanza kwa kusema ningependa kutoa shukurani zangu za dhati kwenu kwa kupokea kijarida cha "DARAJA LA URAFIKI" kilichotolewa mwezi August mwaka huu wa 2013. Nimefurahishwa mno na kuona kwamba kijarida chetu hicho kimeweza kuchapishwa tena baada ya kupita muda mrefu tangu kuanzishwa kwake, na nimatumaini yangu makubwa kwamba kutakuwa na uwezekano wa kukichapisha tena kila baada ya muda fulani japo angalau mara mbili kwa mwaka au zaidi.

    Pia nimevutiwa mno na makala mbalimbali zilizomo ndani ya kijarida hicho kama vile Mwislamu kutoka Tanzania anayejitolea kutoa Huduma Msikitini katika mji wa Guangzhou mji ambao ni mashuhuri kwa biashara kwa wafanya biashara kutoka nchi mbalimbali zinazoinukia zikiwemo nchi zetu za Kiafrika. Mji huu wa Guangzhou kwa miaka kadhaa sasa umekuwa ni kitovu cha biashara kwa wafanyabiashara na wasafiri kutoka Afrika wanaoelekea nchini China kununuwa bidhaa mbalimbali zenye bei nafuu na zenye ubora unaolingana na hali ya maendeleo ya dunia kwa hivi sasa.

    Hapo miaka ya nyuma kwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita wafanyabishara wengi kutoka mataifa yetu na mengineyo yanayoendelea yalikuwa yakiutumia mji wa Dubai katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kama ni kituo chao kikubwa cha kibiashara kulingana na unafuu wa bei za bidhaa pamoja na kukuwa kwa sekta hiyo katika taifa hilo la Ghuba ya Uwajemi. Hata hivyo baada ya hatua kubwa za kimaendeleo na kiuchumi nchini China kufikia kwenye kiwango cha juu kabisa duniani , mji huu wa Guangzhou umekuwa ni kivutio kikubwa cha kibishara miongoni mwa miji ya Kusini mwa China kama vile kwenye miji ya Hong Kong na Macau .

    Tumekuwa tukisikia simulizi nyingi kutoka kwa wafanyabishara wa nchi zetu kwamba huko Guangzhou kwa hivi sasa kumekuwa na mandhari mbalimbali ya kigeni kama vile migahawa ya vyakula vya Kiafrika, Kiarabu, Kiajemi na mataifa mengine na hata kuna Waafrika na wafanyabiashara ambao wamehamia huko na kuendesha shughuli zao .

    Ni matumaini yangu makubwa kwamba kupitia kijarida chetu hicho cha "DARAJA LA URAFIKI " Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa itaendelea kutupasha habari na simulizi za kuvutia juu ya waafrika wenzetu wanaoishi na kufanya biashara katika mji huo wa Guangzhou na katika maeneo mengine ya Jamhuri ya Watu wa China. Ahsanteni sana.

    Nasi tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk kwa barua yako, ni kweli mji wa Guanzhou kwa sasa ni maarufu sana kwa wageni hususan kutoka Afrika, kwani huko wanapata mahitaji yao yote ya kibiashara tena kwa bei nafuu kabisa, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka ka msikilizaji wetu Mwanahija Bakiza wa SLP 3501 Tanzania, anasema kwa kweli lugha ndio msingi wa maendeleo duniani kote, nchi nyingi za bara la Asia zimendelea kwa kuzipa hadhi lugha zao. Lugha ya kufundishia ikieleweka, maarifa hupokelewa kwa wepesi na kutumika kwa wakati; usipoielewa lugha unayojifunza maarifa huchelewa kueleweka matokeo yake ni kuyatumia maarifa kwa kubahatisha. Kila kitu cha kitaaluma huhitaji kufika kwa anayejifunza na ni vyema maarifa hayo yakapata matumizi, vyenginevyo tunapotumia lugha za kigeni tunajidanganya tu.

    Sisi watanzania lugha yetu rasmi na ya taifa ni Kiswahili sielewi ni kwasababu gani serikali yetu inasita kutekeleza sera ya utamaduni kuhusu lugha kwa haraka ili nasi tukimbie kufikia maendeleo katika nyanja zote za maisha. Tukijifunza kilimo, uvuvi, ufugaji, ufundi, tiba na hata teknolojia nyengine za kisasa kwa Kiswahili tutafika mbali sana kimaendeleo.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Mwanahija Bakiza kwa barua yako fupi kuhusu lugha ya Kiswahili, kwa kweli umezungumzia jambo la maana sana, kwani lugha ni kitu muhimu, na ndio maana sisi wachina tunatumia kichina kwenye kila kitu, kwenye masomo, mikutano, shughuli rasmi na zisizo rasmi hii ndio njia pekee ya kukuza lugha na kuiendeleza, ahsante sana.

    Mwisho tunawaletea ujumbe tuliotumiwa kwenye tovuti yetu na kwanza ni Adad anasema naomba tu nchi ya China iendelee kuwekeza Africa.

    Naye Bethuel Muthomi wa SLP 345- Naivasha anasema naipenda sana ratiba yenu na ujumbe ambao mwapitisha kwa wakenya na dunia mzima.

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu kwa maoni yenu mliyotutumia kupitia kwenye tovuti yetu, tunawaomba muendelee kusikiliza matangazo na vipindi vyetu na kuweza kutoa maoni na mapendekezo yenu ahsanteni sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako