Pendekezo la serikali ya Kenya kwa kila familia nchini humo kupata watoto wasiozidi wawili limeendelea kuzua hisia tofauti kwa wananchi wake.
Baadhi ya wakenya wanadai kuwa serikali haifai kuingilia swala la kupata watoto huku wengine wakiunga mkono pendekezo hilo.
Mwandishi wetu kutoka studio zetu za Nairobi Mark Muli aliongea na baadhi ya wakenya na kutuandalia taarifa ifuatayo.
Kulingana na serikali ni kwamba idadi ya wananchi humu nchini inaendelea kukua kwa haraka na huenda idadi hii ikapita ile serikali inaweza kukidhi katika mahitaji ya kimsingi ikiwa haito chukua hatua.
Sababu za idadi ya wakenya kuongezeka kwa wingi serikali imesema zimetokana na kuimarika kwa hali ya maisha humu nchini na sasa ongezeko hili linafaa kushugulikiwa.
"Serikali ya Kenya kwa sasa inalenga kudhibiti ongezeko la wananchi wake kwa kupunguza watoto ambao kila familia inafaa kuapata, kutoka watoto 4.6 kwa kila mwanamke hadi watoto 2.6 ifikapo mwaka wa 2030, na kisha watoto 2.1 ifikapo mwaka wa 2050."
Kwa sasa idadi ya wananchi humu nchini inakua kwa asilima 3 kila mwaka ambayo ni idadi ya watu milioni moja kila mwaka.
Ikiwa idadi ya wakenya itaendelea kukua kwa asilimia hio ifikapo mwaka wa 2030 nchini hii itakuwa na wananchi takribani milioni 55 na kufikia viwango ambavyo serikali inasema.
Baada ya serikali kutoa pendekezo la kila familia humu nchini kupata watoto wasiozidi wawili, pendekezo hili limeanza kuzoa hisi tofauti tofauti miongoni mwa wakenya.
Baadhi ya wakenya wanaounga mkono pendekezo hili ni wale wanaoishi katika miji na walio elimika.
Vincent Ouma ni mkaazi wa jiji kuu la Nairobi na kwake pendekezo hili limekuja katika wakati unaofaa.
Ouma anasema kuwa katika hali ya sasa ya ukosefu wa fursa za kazi, ukosefu wa chakula na pia maisha bora hatua hiyo inafaa kabisa.
Vincent Ouma
"Katika hali ya sasa watu wanaendelea na kuongezeka, ukosefu wa kazi pia upo kwa wingi, chakula ndio hicho kimepotea, unaona sasa ukipata watoto wengi sasa bila shaka utashindwa kuwalea"
Katika maeneo ya mashambani hali ni tofauti sana.
Mzee Matumoni Lelkuoni ni mwenyeji wa Samburu na kulingana na yeye ni kwamba watoto wengi ni baraka na udhibitisha uwezo wa mwanaume katika jamii.
Anaeleza kuwa serikali inafaa kuachia mzigo wa uzazi, wazazi pekee sababu kuu ikiwa yeye ana wawtoto zaidi ya 16 na wake zaidi ya 3.
Mzee Matumoni anazidi kueleza kuwa katika mila za jamii yake lazima mwanaume apate wake wengin na watoto ili aweze kutambulika na kupewa hadhi katika jamii yao.
Aidha anasema azma ya jamii yake ni wao kuwa wengi.
Matumoni Lolkueni.
"Sisi tunataka kuwa wengi, mimi niko na watoto kumi na sita, mimi ninawalisha hao wototo wote mzuri sana.Hakuna mtu anayenisaidia hata kidogo.
Sisi katika kimila yetu kama wasamburu ikiwa una mke mmoja wewe hauna manyatta na hautambuliki"
Kando na mzee Matumoni Daniel Juma ambaye ni kijana wa umri wa miaka 24 anasema yeye haoni shida ya serikali kutoa pendekezo hilo.
Anasema kwake hata motto mmoja anatosha ukilinganisha na hali ya maisha ilivyo kwa sasa.
Daniel Juma.
"Mimi naona kwamba hata moto mmoja ni tosha, kwa sababu bora uitwe mzazi.Naamini kuwa ukipata mtoto mmoja utakuwa na uwezo wa kumshughulikia katika maisha yake vilivyo hata katika masomo.
Mambo sasa imekuwa ni ngumu sana.Kwa hivyo mtoto mmoja kwangu ninaona anatosha."
Mzee Odongo Randa ni mzee aliye na umri wa miaka 72 kutoka eneo la Nyanza humu nchini.
Kulingana na yeye ni kwamba wananchi wanafaa kuachiliwa wajichagulie idadi ya watoto kila familia inataka kupata katika ndoa.
Mzee Odongo anashangaa ni kwa nini hilo lifanyike ilhali watu wanafariki kutokana na majanga tofauti humu nchini, akihoji kuwa pengo hilo linafaa kuzibwa.
Odongo Randa.
"Wachaneni na watu waendelee kuzaana, kwa sababu siku hizi watu wanakufa kama inzi, watu wanakufa na Ukimwi katika nchi yetu hii, na sasa kama mtasema kila mwanamke apate watoto wawili nani anajua kwamba hao watoto wataweza kuishi?"
Vivian Wanjiku kijana wa miaka 26 na mkaazi wa Nairobi anasema kuwa wanotaka kuendelea kupata watoto wengi ni wale bado hawajaweka mpango mahususi wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata maisha mazuri ya baadaye.
Wanjiku anasema wazo hilo la serikali kwa familia kupata watoto wasiozidi 2 linafaa kutekelezwa pasipo pingamizi.
Vivian Wanjiku
"Mimi nafikiria ni wazo nzuri, kwa sababu ni vyema mtu kupata watoto ambao anaweza kulea vizuri pasipo na taabu."
Hatua hii ya serikali ya kutoa pendekezo hilo imekuja hata baada ya kuweko kwa mpango wa kupanga uzazi uliokuwa ukitiliwa mkzo na serikali kwa muda wa miaka kadha sasa.
Serikali inasema mpango huo wa kupanga uzazi ulikuwa umewapa wanandoa fursa ya kuamua idadi ya watoto watakao pata laini sasa itabidi serikali kuweka idadi hii kama watoto 2.
Mark Muli CRI Nairobi.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |