• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya yaadhimisha miaka 50 tangu ipate uhuru

    (GMT+08:00) 2013-12-12 11:08:13
    Ama kweli baada ya dhiki faraja, Kenya inaadhimisha miaka 50 tangu ipate uhuru baada ya enzi za ukoloni wa waingereza uliokuwa na mateso.

    Siku hii husherekewa kila mwaka tangu mwaka 1963 wakati Kenya ilipoanza rasmi kujitawala. Safari ya uhuru wa Kenya ilikuwa na mateso na changamoto nyingi kupita kiasi, lakini wakenya wazalendo walioipenda nchi hii walijitolea kwa hali japo sio mali kupigana hadi uhuru ulipopatikana.

    Mwaka 1895 serikali ya Uingereza ilipiga kambi katika eneo la kanda ya Afrika mashariki. Punde baada ya kuwasili waingereza walinyakua ardhi iliyokuwa na rutuba na mashamba kutoka kwa wakenya na kujigawia huku wakenya wakilazimishwa kulima mashamba hayo. Ilipofika mwaka 1920 waingereza walitangaza rasmi kuwa Kenya ni moja ya himaya yake na ikawekwa chini ya ukoloni ama utawala wake.

    Mwezi Desemba mwaka 1952 hadi 1959 Kenya ilizinduka na hali ya dharura ya kudai ardhi yao mali yao na mashamba yao ikipinga utawala ukatili na unyama wa waingereza waliojidai kuitawala nchi hii. Makundi kama vile Mau Mau yaliundwa yakiongozwa na viongozi kama Dedan Kimathi, Stanley Mathenge, Musa Mwariama JM Kariuki. Makundi haya yalikuja na mwamko mpya ulioeneza msemo wa mzungu arudi ulaya na mwafrika apate uhuru.

    Kundi la Mau Mau na makundi mengine ya wakenya yalijitahidi sana kupigania Uhuru. Katika vita hivyo vya uhuru maelfu ya wakenya walipoteza maisha yao. Kuanzia Oktoba 1952 mpaka Desemba 1959, Kenya ilikuwa katika hali ya hatari kufuatia uasi wa Mau Mau dhidi ya utawala wa Uingereza. Uingereza iliomba msaada wa wanajeshi zaidi kutoka uingereza na waafrika, mnamo Januari 1953, Meja Jenerali Hinde aliteuliwa kuwa mkuu wa operesheni ya kuzima uasi. Hali hii haikuimarika kwa kukosa uchunguzi, kwa hivyo Jenerali George Erskine aliteuliwa kuwa kamanda msimamizi wa majeshi ya kikoloni mnamo Mei 1953, akiungwa mkono hasa na Winston Churchill. Kutiwa mbaroni kwa Warũhiũ Itote (aka General China) tarehe 15 Januari 1954, na kuhojiwa kwake kulifanya Waingereza kuuelewa vizuri usimamizi wa Mau Mau.

    Operesheni Anvil iliyoanzishwa tarehe 24 Aprili 1954 ilipangwa na jeshi kwa wiki kadhaa baada ya kukubaliwa na kamati kuu ya vita. Wakati wa operesheni hii, mji wa Nairobi ulidhibitiwa na wanajeshi na wakazi wake walihojiwa huku wafuasi wa Mau Mau wakikamatwa na kupelekwa vizuizini.

    Mnamo Mei 1953, walinzi wa nyumbani walitambulika rasmi kama askari wa usalama. Askari hawa wa nyumbani ndio waliounda kikosi cha kupambana na mikakati ya Mau Mau kwani walikuwa Waafrika waaminifu, na si majeshi ya kigeni kama Jeshi la Uingereza na King's African Rifles. Kufikia mwisho wa hali ya hatari, askari hawa 4886 walikuwa wamewaua, ambayo ni asilimia 42% ya waasi wote. Kukamatwa kwa Dedan Kimathi huko Nyeri tarehe 21 Oktoba 1956 kuliashiria kushindwa kwa Mau Mau na kukamaliza vita. Mwaka wa 1957 waafrika walichaguliwa moja kwa moja katika bunge la uwakilishi kwa mara ya kwanza. Waingereza walisita kuwakabidhi mamlaka wapinzani wao wakidai kuwa na siasa duni za kiafkrika, ni chama cha Kenya African National Union (KANU) kilichoongozwa na Jomo Kenyatta kilichounda serikali punde tu kabla ya Kenya kupata uhuru tarehe 12 Desemba 1963.

    Mwaka huo huo, jeshi la Kenya lilipambana na katika Vita vya Shifta dhidi ya kabila la Wasomali waliokusudia kuiona NFD inajiunga na Jamhuri ya Somalia. Mashifta walililemea jeshi la Kenya lakini baadaye mwaka wa 1967walishindwa.

    Tarehe 12 Desemba 1964 Kenya ilitangazwa kuwa jamhuri huku Kenyatta akiwa rais wa kwanza. Jomo Kenyata aliongoza Kenya kwa miaka 15 kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1978 wakati alipofariki. Kenyata atakumbukwa sana katika kuimairisha siasa na uchumi wa Kenya. Wakati wa uongozi wake alihimiza wakenya kuenzi utamaduni wao na kupuuza ukabila. Pia anakumbukwa na uongozi wake thabiti wa ushujaa, ujasiri na hotuba kali.

    Mzee Jomo Kenyatta alipoaga dunia 22 Agosti 1978 Daniel Arap Moi, aliapishwa kuwa Rais wa Kenya. Bw Moi alipendwa na watu wengi kote nchini, na alitembelea sehemu zote Kenya, na wananchi walimkaribisha kwa vifijo na nderemo .

    Mnamo 1 Agosti 1982, Wanajeshi waminifu kwa Moi, waliwaponda maofisa wa jeshi la anga wa kiongozwa na Hezekiah Ochuka ambao kwa kushirikiana na baadhi ya wanasiasa walijaribu kupendua serikali. Daniel arap Moi alichaguliwa bila kupingwa katika chaguzi za mwaka wa 1979, 1983 na 1988, Uchaguzi wa 1983 ulifanyika mwaka mmoja mapema kutokana na njama ya kupindua serikali iliyokosa kufaulu mnamo tarehe 1 Agosti 1982. Moi aliongoza kwenye kwa miaka 24.

    Tukiendelea katika safari ya miaka 50 ya Kenya ya uongozi ,Mwaka 2002 Moi hakuruhusiwa kugombea urais, na Mwai Kibaki wa chama cha upinzani cha "National Rainbow Coalition" — NARC akachaguliwa kuwa rais. Uchaguzi huu ulitambulikana kuwa wa kidemokrasia na wachunguzi wa humu nchini na wa kimataifa na hivyo kuwa chanzo cha mageuzi makubwa ya kidemokrasia nchini Kenya.

    Rais Mwai Kibaki akiwa rais wa tatu wa jamhuri ya Kenya ndie rais aliyengia kwenye vitabu vya kumbukumbu za historia kama rais aliyekuwa na mafanikio makubwa sana katika uongozi wa Kenya. Katika uongozi wake wa miaka 10 Kibaki alitoa fursa ya kila mtoto nchini Kenya kupata elimu kwani serikali yake ilianzisha mfumo wa elimu ya bure kwenye shule za msingi. Rais Kibaki aidha alifanikiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa sana miundo msingi nchini Kenya .Atakumbukwa na ufanisi wake wa kujenga barabara kuu ya Thika. Uongozi wa Kibaki ulitoa fursa ya kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kurekebshwa kwa katiba ya Kenya. Kibaki pia aliimarisha uhusiano thabiti wa kiuchumi na kirafiki baina ya Kenya na China. Kibaki aliongoza Kenya kwa miaka 10 kutoka mwaka 2002 hadi mwaka 2013.

    Baada ya uongozi wa kibaki hii leo wakenya wanasherekea uongozi mpya wa viongozi chipukizi wanaotamba kwa mbwembwe na maendeleo ya kasi ya mfumo wa dijitali. hawa ni viongozi wa Jubilee wanaoongozwa na Rais Uhuru Muigai Kenyata ambaye ni mtoto wa aliyekuwa rais wa kwanza Jomo Kenyata. Hii leo Uhuru Kenyata atawahutubia wakenya wote nchini kuhusu safari ya miaka 50 ya Kenya tangu ipate Uhuru. Huku safari ya Kenya ikifikia miaka 50, safari ya Uhuru Kenyatta kama kiongozi wa nne wa Kenya ndio inaanza.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako