• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Madereva wa usiku nchini Kenya kupata leseni maalum

    (GMT+08:00) 2013-12-26 11:23:42

    Kufuatia visa vingi vya ajali za barabarani nchini Kenya ,serikali imeanzisha kanuni ya kutoruhusu magari ya usafiri wa umma kubeba abiria kati ya saa 12 jioni na saa 12 alfajiri kabla ya kupata leseni maalum kutoka kwa Mamlaka ya kitaifa ya usafiri na Usalama nchini humo (NTSA).

    Katibu Mkuu wa Wizara ya uchukuzi nchini Kenya Bw.Nduva Muli amesema kuwa hatua hiyo ni kufuatia kanuni zilizochapishwa katika gazeti rasmi la serikali tarehe 17 mwezi huu,na zimeanza kutekelezwa kuanzia jana usiku.

    Katibu wa Wizara ya uchukuzi nchini Kenya Bw.Nduva Muli amesema kuwa ajali nyingi hutokea wakati wa usiku,na aliwalimbikizia lawama wahudumu wa magari ya umma kwa kutofuata sheria.

    Katika mwezi huu wa Desemba zaidi ya watu 190 wamepoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani.

    Muli alisisitiza kauli ya usalama barabarani na kutoa ilani kwa madereva wa usafiri wa umma kuwa watachukuliwa hatua kuanzia usiku wa jana iwapo hawatafuata sheria.

    "Iwapo wahudumu wa magari ya usafiri wa umma hawatatii kanuni kuhusu udhibiti wa usafiri wa usiku -kutosafiri kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi watakiona cha mtema kuni.Kanuni hizi zinafaa kufuatwa kikamilifu.Tunatumia fursa hii kutoa ujumbe huu kwa watu wote kwamba kanuni hizi zinafaa kufuatwa.Tafadhali musiabiri magari ambayo hayana leseni maalum ya kuhudumu usiku."

    Haya yamejiri kufuatia ajali iliyotokea juzi usiku kati ya basi la kampuni ya Horizon na lile la kampuni ya Spring iliyosababisha vifo vya watu 17 eneo la Mtito Andei.

    Katika mwezi huu wa Desemba ajali tofauti zimeweza kushuhudiwa.Watu zaidi ya 190 wamepoteza maisha yao katika ajali za barabarani mwezi huu wa Desemba.

    Hata hivyo wakenya watasubiri kuona utekelezwaji wa sheria hiyo,hasa kutokana na kuwa hakuna hata leseni moja ya usiku iliyotolewa kwa kampuni yoyote ya usafiri wa umma.

    Kwa mujibu wa kanuni chini ya Ilani ya sheria nambari 219 ya Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Taifa na Usalama,kila mhudumu wa wa magari ya usafiri wa umma wa mwendo mrefu,kwanza anahitajika kuhakikisha kwamba ameajiri madereva wawili waliothibitishwa na kupasishwa na mamlaka hiyo.

    "Makampuni yote yanayotoa huduma za usafiri wa umma wa mwendo mrefu nyakati za usiku yanafaa kuajiri madereva waliopasishwa na mamlaka kuendesha gari usiku kwa kufuata vikwazo vilivyowekwa na mamlaka ya usafiri."

    Aidha wenye kampuni za usafiri wa umma wanafaa kuhakikisha kwamba dereva hataendesha gari kwa zaidi ya masaa manane na kwamba atapumzika kwa masaa manane kabla ya kuanza zamu nyengine.

    "Wenye kampuni wanafaa kuhakikisha kwamba dereva wa masafa marefu hawafanyi kazi kwa zaidi ya masaa manane.Wanafaa kuhakikisha kwamba dereva anapumzika kwa masaa manane kabla ya kuanza zamu nyengine na pia wapange safari kwa njia ambayo itaruhusu pumziko la nusu saa kwa abiria na dereva baada ya kuendesha gari kwa masaa 3 hadi manne na pia wanafaa kuajiri madereva wawili kwa kila basi."

    Katibu Nduva Muli amewataka abiria pia kuwasaidia wasimamizi wa sheria kwa kutoabiri magari ya umma ambayo hayana leseni maalum inayohitajika ambayo amesema ni lazima ibandikwe katika gari.

    Alisema Wizara ya Usafiri tayari imechapisha kanuni hizo kwenye magazeti na kuwasihi wenye makampuni ya magari ya usafiri wa usiku kutii amri na kuchukua leseni hizo.

    Mwezi Agosti mwaka huu,mojawapo wa ajali mbaya zaidi za barabarani iliyohusisha basi la kampuni ya City to City ilisababisha vifo vya watu 41 katika eneo la Ntulele kwenye barabara ya Mai Mahiu-Narok.

    Kampuni ya basi iliyohusika kwenye ajali ilipigwa marufuku na kushtakiwa na serikali.Hata hivyo hii haikuchukuliwa kama funzo na kampuni zengine za mabasi.

    Maafisa wa polisi wa trafiki pia wamelaumiwa kwa kupokea hongo kutoka kwa wanaokiuka sheria za barabarani,ambao baadaye husababisha ajali.

    Lakini sasa macho yote yanalekezwa katika sheria hizi mpya na jinsi zitakavyotekelezwa. Kufuatia kuongezeka kwa ajali barabarani humu nchini serikali kupitia waziri wa uchukuzi mhandisi Michael Kamau imerejesha tena kifaa maalum cha kupima ulevi hasa kwa wale wanaoendesha magari barabarani.

    Zaidi ya watu 3000 nchini Kenya wamepoteza maisha yao katika ajali za barabarani mwaka huu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako