• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Zaidi ya watu 70 wauawa katika mlipuko kwenye kituo cha mabasi nchini Nigeria

    (GMT+08:00) 2014-04-15 17:00:29

    Mauaji ya kinyama ya zaidi ya watu 70 katika kitongoji cha Nyanya, pembezoni mwa mji mkuu wa Nigeria, Abuja, jumatatu asubuhi, ni ishara ya kukumbushia kuwa, nchi hiyo inaelekea katika jamii iliyozungumzwa na mwanafalsafa Thobas Hobbes, kuwa maisha ni magumu, ya kikatili, na mafupi.

    Watu wengi wamefariki baada ya bomu lililotegwa kwenye gari aina ya Volkswagen Golf lililokuwa limeegeshwa kwenye stendi ya mabasi kulipuka na kusababisha vifo vya watu 71 na wengine 123 kujeruhiwa. Majeruhi wanapata matibabu kwenye hospitali zilizopo Nyanya na maeneo mengine ya mji mkuu wa Nigeria, Abuja. Karibu mabasi 16 yaliteketea kwa moto na magari mengine 24 ya aina mbalimbali yaliharibika. Hakuna kundi lililokiri kuhusika na mlipuko huo, lakini asili ya mlipuko inaendana na milipuko mingine inayofanywa na kundi la Boko Haram, kundi la kigaidi la kiislam linalofanya mashambulizi kutokea eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria. Kundi hilo limekuwa ni tishio kubwa kwa usalama nchini Nigeria tangu mwaka 2009.

    Mauaji ya Abuja ni ishara kuwa, kampeni ya matumizi ya nguvu imevuka mpaka. Na swali ambalo linaweza kuulizwa ni je, watu wanaofanya vitendo hivyo wanategemea kupata nini kwa mauaji ya kikatili ya vijana na wanafunzi wasio na hatia? Swali lingine linaloweza kuulizwa ni je, kuna itikadi na sababu gani ya kufanya mauaji ya kutisha kama haya? Wakati umefika sasa kwa raia wa Nigeria wanaoitakia mema nchi yao kusimama kidete na kulaani mauaji haya ya kinyama kabla nchi hiyo haijaingia kwenye hali ya kukosa utawala. Huu si wakati wa kutoa maneno matupu na yasiyo na ukweli ndani yake.

    Serikali inatakiwa kutoa maamuzi makali sasa. Rais Goodluck Jonathan anatakiwa kufanya mabadiliko muhimu katika mchakato wa usalama ili kumaliza mauaji ya raia wasio na hatia, na kuondoa wingu la ukosefu wa amani lililotanda nchini Nigeria. Wananchi wa Nigeria wamesikia ahadi kem kem zilizotolewa na serikali ya sasa, kwamba itachukua hatua zote zinazotakiwa kuzuia vifo na majeruhi vinavyosababishwa na milipuko. Kwanza, serikali inatakiwa kufanya uchunguzi wa wazi, wa haraka, na wa uhakika kuhusu mauaji hayo, kutoa taarifa za uchunguzi huo kwa wananchi, na kuwafikisha wale wote wanaoshukiwa kuhusika na vitendo hivyo mbele ya vyombo vya sheria. Serikali ya rais Goodluck Jonathan inatakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maafa kama yale yaliyotokea Nyanya hayatokei tena.

    Katika hatua nyingine, kunaelekea kuwa na mambo mengi zaidi ya umwagaji damu nchini Nigeria kutokana na kwamba, kundi la Boko Haram linaendeleza mfululizo wa mauaji. Jumapili iliyopita, wapiganaji wa kundi hilo wameua watu wasiopungua 60 katika vijiji vya Ngoshe na Kaigamari, vilivyoko kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno, karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon. Kabla ya hapo, jumamosi iliyopita, magaidi hao waliua zaidi ya watu 200, wakiwemo wanafunzi waliokuwa wakifanya mitihani yao kwenye jimbo hilohilo. Pia waliteketeza kwa moto nyumba, maduka, na vibanda kadhaa vya mawasiliano, pamoja na mali nyingine zenye thamani ya mamilioni ya Naira.

    Wakati familia za marehemu zikijitahidi kukubaliana na mauaji ya kikatili ya wapendwa wao wasio na hatia, wanaweza kupata faraja kidogo kutokana na kauli za kulaani shambulizi hilo zinazotolewa na maofisa wa serikali za ngazi mbalimbali, jambo ambalo ni kawaida katika mfululizo wa mauaji ya kikatili ya wanigeria wasio na hatia katika siku za hivi karibuni.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako