• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano wa kilele wa kuhusu uchumi wa Afrika wajadili njia ya maendeleo ya Afrika

    (GMT+08:00) 2014-05-10 15:46:05

    Mkutano wa kilele kuhusu Afrika wa Baraza la uchumi wa dunia ulimalizika jana huko Abuja, Nigeria. Katika mkutano huo wa siku 3, wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wapatao 900 kutoka nchi zaidi ya 70 duniani walijadili mada mbalimbali zikiwemo namna ya kupata maendeleo ya haki na usawa, jinsi kuongeza nafasi za ajira na mwelekeo wa uchumi wa Afrika.

    Katika miongo ya karibuni, uchumi wa Afrika umekuwa unakua kwa kasi, huku hali ya kisiasa na mazingira ya uwekezaji vinaboreshwa kwa kiasi kikubwa. Waliohudhuria mkutano huo wa kilele wamekubaliana kuwa, ili kudumisha ongezeko la uchumi lililopatikana, ni lazima maendeleo yenyewe yawe ya haki na usawa.

    Mwanauchumi mkuu wa benki ya dunia katika sehemu ya Afrika Mashariki Apula Sangi alisema, Afrika inapaswa kuhamasisha ongezeko la uchumi linalowapa watu wake fursa sawa ya kupata utajiri na kunufaika na matunda ya maendeleo. Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alitoa wito kwa nchi za Afrika zitilie mkazo katika kukabiliana na suala la kutokuwa na usawa, ili haki na maslahi ya wanyonge yafuatiliwe zaidi. Na rais Paul Kagame wa Rwanda pia alisema, kampuni za watu binafsi zinafanya kazi muhimu katika kufanikisha maendeleo ya haki na usawa nchini Rwanda, na serikali za nchi mbalimbali zinapaswa kuzihamasisha kampuni ziwekeze zaidi katika sekta zinazoweza kuleta nafasi nyingi za ajira, hatua ambayo itasaidia kuongeza pato la watu wengi.

    Hivi sasa uchumi wa nchi nyingi za Afrika zilizoko kusini mwa Sahara unategemea kuuza nje mali ghafi za kilimo na madini, hali ambayo inazifanya zishindwe kupata uhuru wa kiuchumi na sekta ya viwanda kukwama.

    Mwanauchumi Sangi alichambua akisema, watu wamezoea nadharia kwamba, kuendeleza viwanda ni njia pekee ya kuleta maendeleo ya uchumi, na nchi nyingi pia zinafuata njia hiyo ya kuboresha muundo wa uchumi yaani kutoka kilimo hadi sekta za utengenezaji na huduma. Hata hivyo mtaalamu huyo alisema njia nyingine pia zilitoa mfano wa kuigwa, kama vile kukuza sekta ya huduma za mambo ya fedha, sekta ya upashanaji habari, hata sekta ya utengenezaji filamu.

    Mkurugenzi wa idara ya Afrika katika shirika la fedha la kimataifa IMF Roger Node alitoa pendekezo kuwa Afrika inapaswa kufanya mageuzi katika mambo matatu, kujenga miundo mbinu ya kisasa, kuendeleza kilimo cha kisasa na kuimarisha uchumi wa watu binafsi. Pia aliona kuboresha miundo mbinu kati ya sehemu tofauti barani Afrika kutachangia kuhimiza biashara kati ya nchi za bara hilo, kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa nchi, kuhimiza ongezeko la uchumi na kuongeza biashara ndani ya bara la Afrika.

    Afrika ina asilimia kubwa ya vijana, ambao ni nguvu kazi na wanunuzi wa siku za baadaye. Katika Afrika kusini mwa Sahara, inakadiriwa kuwa hadi ifikapo mwaka 2040, idadi ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24 itaongezeka kwa asilimia 15 hadi 20 kila baada ya miaka 10. Kwa mujibu wa ripoti ya benki ya maendeleo ya Afrika, hivi sasa vijana wa umri huo wanachukua asilimia 60 ya watu wasio na ajira barani humo, ndiyo maana ajira kwa vijana ni suala kuu linalozikabili serikali za nchi mbalimbali za Afrika.

    Mwanauchumi mkuu wa benki ya maendeleo ya Afrika Stephen Mule alipendekeza serikali za nchi za Afrika zitilie mkazo kuzihamasisha kampuni binafsi kuleta nafasi za ajira kwa vijana, kuwaelekeza vijana watumie teknolojia mpya katika mambo ya kilimo, na kutoa sera za kuwafundisha kiufundi vijana. Mtaalamu huyo alisema, Afrika inaweza kuwaandaa vijana nafasi nyingi zaidi za ajira kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kuvutia mitaji katika sekta za utengenezaji na shughuli zinazohitaji wafanyakazi wengi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako