Uwanja utakaotumika siku ya mechi ya ufunguzi kati ya waandaaji wa kombe la dunia Brazil na Croatia Juni 12, Arena de Sao Paulo sasa upo tayari kwa mashindano ambayo yanashughulikiwa na FIFA na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo nchini Brazil LOC. Uwanja huo ambao ni wa mwisho kujaribiwa ulichezewa mechi ya kwanza Jumapili kati ya wenyeji Corinthians na Figueirense, ambapo wageni waliibuka na ushindi wa 1-0. Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mkurugenzi wa kamati ya maandalizi Ricardo Trade amesema ameridhishwa na kufurahishwa na namna operesheni ilivyokwenda. Akizungumza kwa niaba ya wenyeji Corinthians baada ya mechi hiyo, Andres Sanchez amesema mechi hiyo imeipatia uzoefu mpya klabu yake. Kwa upande wake msimamizi maalumu wa kombe la dunia wa sekretariet ya FIFA huko Sao Paulo Raquel Verdenacci pia ameeleza kuridhishwa na jinsi mashabiki walivyowasili na kuondoka katika mechi ya majaribio.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |