Jeshi la Thailand limetangaza kuwashikilia kwa wiki moja waziri mkuu aliyeondolewa mamlakani Yingluck Shinawatra, mawaziri wa zamani na viongozi wa maandamano. Naibu msemaji wa jeshi kanali Vinthai Suvari amesema Yingluck na wafungwa hao wako salama na wataendelea kushikiliwa na jeshi kwa wiki moja baada ya kuhojiwa na baraza la kitaifa la amani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya uangalizi. Hata hivyo kanali Vinthai amesema jeshi halitatumia nguvu dhidi ya makundi ya watu yatakayofanya maandamano kupinga mapinduzi hayo ya kijeshi. Baraza la kitaifa la amani na utulivu linaloongozwa na mkuu wa majeshi Generali Prayuth Chan-ocha limewataka maofisa wote wa serikali kufuata amri ya utawala mpya wa kijeshi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |