Colombia ilikamilisha mechi zake za makundi kwa kishindo ilipoicharaza Japan mabao 4-1 na kuendelea kuwa vinara wa kundi C huku wakiwa na alama zote 9. Timu hiyo ambayo ilikuwa imekwisha fuzu raundi ya timu 16 bora, haikulegeza kamba baada ya Mainz Shinji Okazaki wa Japan kusawazisha goli la Juan Cuadrado wa Colombia lililopatikana kwa njia ya penalti baada ya Adrian Ramos kufanyiwa dhambi na Yasuyuki Konno mbele ya lango. Bao hili liliwatanabahisha Colombia ambao walikaza buti na kufunga mabao matatu bila ya jibu. Jackson Matinez aliifanya Colombia iongoze tena kabla ya kuingiza bao la tatu kwa Colombia katika dakika ya 82. James Rodriguez alihakikisha Colombia imejizolea alama zote tatu katika mechi za makundi na kuwa taifa la pili kufanya hivyo baada ya Uholanzi, kwa kufunga bao la nne mnamo dakika ya 89. Colombia itachuana na mshindi wa pili wa kundi D ambaye ni Uruguay baada ya timu hiyo ya Luis Suarez kuwafungasha virago mabingwa mara nne wa kombe la dunia Italia ilipoilaza kwa bao 1-0. Ugiriki ilifuzu kama mshindi wa pili katika kundi C na hivyo sasa itakwaruzana na washindi wa kundi D Costa Rica .
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |