Argentina na Nigeria zote zimefuzu raundi ya timu 16 kwenye kombe la dunia licha ya Nigeria kufungwa magoli 3-2 katika mechi yao ya mwisho kwenye hatua ya makundi. Mabingwa hao wa Afrika waliomaliza wakiwa nafasi ya pili na zawadi ya pointi 4 katika kundi lao F, walifahamu fika kuwa iwapo Iran itaifunga Bosnia basi wao walilazimika kuilaza Argentina. Lionel Messi alifanikiwa kuifanya Argentina iongoze katika kipindi cha kwanza baada ya kufunga magoli mawili. Goli la kwanza la Messi lililofungwa katika dakika ya 3 lilisawazishwa na Ahmed Mussa ndani ya sekunde 80. Hata hivyo Messi hakutetereka kwani katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza alipachika bao la pili na kuifanya nchi yake iongoze hadi wanakwenda mapumziko. Katika kipindi cha pili Mussa aliendeleza ari zake na kuhakikisha Nigeria wanondoka kiwanjani wakiwa mabingwa baada ya kusawazisha tena goli Messi katika dakika ya 47. Lakini waswahili wanasema kifo cha nyani majani hupukutika kwani Rojo Marcos aliiongezea machungu Nigeria baada ya kuifungia Argentina goli la 3 na kuifanya itoke kifua mbele. kwa matokeo hayo Argentina imemaliza ikiwa nafasi ya kwanza katika kundi F huku ikiwa na pointi zote 9. Nigeria sasa itakabiliana na Ufaransa Jumatatu ijayo huku Argentina ikicheza na Uswisi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |