Kwa mara ya kwanza katika historia timu ya taifa ya Algeria imefuzu kucheza raundi ya pili katika kombe la dunia. Mbweha wa Jangwani waliokuwa nyuma kwa bao moja kwa nunge dhidi ya Urusi katika kipindi cha kwanza walifanikiwa kusawazisha na hivyo kufuzu kama mshindi wa pili katika kundi H nyuma ya Ubeljiji. Hii ni mara yao ya kwanza kuvuka raundi ya kwanza. Algeria itaingia katika kumbukumbu za historia ya Soka Afrika kuwa mwakilishi wa 6 kuwahi kufuzu kwa raundi hiyo ya 16 bora nyuma ya Cameroon, Ghana Nigeria, Morocco na Senegal. Wadau watachunguza tukio ambalo shabiki mmoja anadaiwa kumulika kifaa cha Laser usoni mwa kipa wa Urusi Igor Akinfeev kabla ya bao hilo la kusawazisha. Kocha Capello amelalamikia hatua ya refarii kupuuza tukio hilo akisema kuwa huenda marefarii wananjama ya kuihujumu timu ya Urusi. Algeria sasa itacheza na Ujerumani katika mechi ya 16 bora siku ya jumatatu.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |