Kocha wa Brazil Luiz Scolari amesema timu yake itaweza kucheza vizuri bila ya mshambuliaji wake aliyejeruhiwa Neymar wakati watakapocheza nusu fainali dhidi ya Ujerumani leo hii. Neymar mwenye miaka 22 amefunga magoli manne kati ya nane iliyopata Brazil kwenye mashindano hayo, lakini hatocheza tena baada ya kuvunjika mfupa unaoshikana na uti wa mgongo katika mechi ya robo fainali ambapo Brazil iliibuka na ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Colombia. Scolari amesema timu yake kwa sasa ipo makini na kazi iliyopo mbele yao, kwani Neymar amefanya sehemu yake na sasa ni juu yao kumalizia sehemu yao. Neymar amejeruhiwa mgongo na mchezaji wa Colombia Juan Zuniga na jana Fifa ilitangaza kuwa haitachukua hatua yoyote ya kinidhamu dhidi ya mshambuliaji huyo kwasababu kosa lilionekana na likashughulikiwa na refari kiwanjani hapohapo. Wakati huohuo chombo hicho kikubwa cha soka duniani kimesema hakitabatilisha kadi ya njano aliyopewa nahodha wa Brazil Thiago Silva walipocheza na Colombia, kikisema hakuna sheria inayorohusu kukubaliwa ombi la kutengua kadi ya njano. Brazil leo itavaana na Ujerumani katika mechi ya nusu fainali kuanzia saa 3 usiku kwa saa za nchi hiyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |