• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mikoa iliyoko kando ya njia ya hariri ya baharini yatarajia kupata mafanikio mapya

    (GMT+08:00) 2014-07-09 14:05:53

    Mji wa Quanzhou mkoani Fujian China ukiwa ni mwanzo wa njia ya hariri ya baharini, si kama tu una barabara za zamani zilizojengwa kwa mawe na mnara mrefu wa Liusheng, bali pia una bandari ya kisasa inayostawi sana.

    Bandari ya Quanzhou yenye historia ya zaidi ya miaka 1,500, iliwahi kushuhudia wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali wakifika mji huo katika zama za kale. Hivi sasa imeanzisha zaidi ya njia 30 za biashara na nchi na sehemu 28 duniani.

    Kutokana na viongozi wa China kutoa taswira ya kujenga ukanda wa kiuchumi wa njia ya hariri katika nchi kavu na njia ya hariri baharini, miji iliyoko kando ya njia ya hariri ya baharini imeng'ara tena, na mikoa mbalimbali ya pwani inatarajia kupata maendeleo tena katika mkondo wa mageuzi na ufunguaji mlango.

    Katika mkahawa mmoja wa chai mjini Quanzhou, mzee mmoja anapiga ala ya muziki huku akiimba wimbo wa kienyeji wa mji huo. Wazee wengine wanakunywa chai aina ya Tieguanyin na kusikiliza wimbo huo.

    Nyimbo za kienyeji za mji wa Quanzhou zinaitwa Nanyin, zina historia ndefu ya miaka elfu kadhaa, na mpaka sasa bado zinapendwa na watu wanaoishi kusini mwa mkoa wa Fujian.

    Katika enzi za Jin, Tang(618—907) na Song(960—1279), muziki za sehemu ya katikati mwa China uliingia mkoa wa Fujian, na huo ndio mwanzo wa nyimbo za Nanyin. Katika enzi za Song na Yuan, njia ya hariri baharini ilipata maendeleo makubwa, wafanyabiashara wa China wamepeleka nyimbo za Nanyin katika nchi za Asia Kusini Mashariki, na hivi sasa pia zinasikika katika nchi za Ulaya na Marekani. Mwaka 2009, Shirika la Elimu, Sayansi, Utamaduni la Umoja wa Mataifa liliziweka nyimbo za Nanyin kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana.

    Mrithi wa nyimbo za Nanyin Bw. Xia Yongxi anasema, katika nchi za ng'ambo, watu kutoka mkoa wa Fujian wakisikia nyimbo hizi, wanafurahi sana, kwa sababu wanakutana na watu wengine kutoka mkoa wa Fujian.

    Urithi wa utamaduni si kama tu unawakumbuka na watu wa mkoa wa Fujian, pia ni fursa ya kueneza utamaduni wa China duniani. Opera ya Yue, vitu vya sanaa, na muziki wa kienyeji vimeingia kwenye soko la utamaduni la nchi za Asia Kusini Mashariki, na zinapendwa na watu wa huko. Vyombo vya kauri ambavyo ni vitu muhimu zaidi vya kiutamaduni nchini China, bado vina soko zuri katika nchi za Asia Kusini Mashariki, Ulaya na Marekani.

    Kaunti ya Dehua mjini Quanzhou ni maarufu kutokana na vyombo vya kauri. Kuanzia enzi ya Song, vyombo vya kauri vilivyotengenezwa Dehua viliuzwa kwa wingi katika nchi za Asia Kusini Mashariki na Mashariki ya Kati, na vilikuwa bidhaa muhimu zilizouzwa nje kupitia njia ya hariri baharini katika zama za kale. Sasa Dehua bado ni kituo muhimu cha utengenezaji na biashara ya nje ya vyombo vya kauri nchini China, ambavyo vinauzwa katika nchi za sehemu zaidi ya 180 duniani.

    Meneja mkuu wa kampuni ya Shunmei ya Quanzhou Bw. Zheng Pengfei anasema, katika zama za kale njia ya hariri ya baharini ilivifanya vyombo vya kauri vya China kuuzwa katika nchi za nje, lakini si vizuri kuridhika na historia tu, wanaviwanda wa Quanzhou wanatakiwa kutambua mahitaji ya soko la kimataifa, na kuvifanya vyombo vingi zaidi vya kauri kuingia soko la kimataifa.

    Kuhimiza maendeleo ya uchumi na biashara kwa vitu vya utamaduni ni maoni ya pamoja ya mikoa na miji iliyoko kando ya njia ya hariri ya baharini. Mji wa Quanzhou, ukitumia nguvu yake bora katika mambo ya uchumi, biashara, bandari na utamaduni, unatarajia kuendeleza biashara kupitia njia ya hariri ya baharini. Mji huo unajenga utaratibu wa huduma ya uwekezaji wa pande mbili unaofungua mlango zaidi, kuzifanya huduma za serikali zikidhi mahitaji ya kimataifa, kurahisisha hatua za kupita forodha, kufanya majaribio katika benki zinazofanya shughuli na nje, kuyahimiza makampuni binafsi yaanzishe shughuli zao katika nchi za nje, na kutoa idhini kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kwa usawa.

    Bibi Lin Mingci mwenye umri zaidi ya miaka 30 aliyewahi kuwa mhasibu nchini Indonesia alijiuzulu kazi hiyo na kusoma kozi ya elimu ya lugha ya Kichina katika chuo kikuu cha Jinan mjini Guangzhou. Akiwa ni Mwindonesia mwenye asili ya China, kabla ya kuanza masomo yake mjini Guangzhou, hajawahi kuja China.

    Anasema ana hamu ya kujifunza lugha ya kichina kutokana na ukosefu wa walimu wa lugha ya kichina huko Indonesia, tena anaona analo jukumu la kurithi utamaduni wa jadi wa China. Wakati China na nchi za nje zinapokuwa na uhusiano wa karibu zaidi katika mambo ya uchumi na biashara, watoto wengi wa Wachina wanaoishi nchi za nje wameanza kujifunza lugha ya kichina, na kujenga daraja la mawasiliano kati ya China na nchi za nje.

    Wachina milioni 30 wanaishi katika nchi za Asia Kusini Mashariki. Miongoni mwa nchi hizo, Wachina milioni 10 wanaishini nchini Indonesia, milioni 7 Thailand, na milioni 5.6 wanaishi Indonesia. Shule mbalimbali za lugha ya kichina zimeanzishwa katika nchi hizo ili kukidhi mahitaji ya Wachina wanaoishi huko ya kurithi utamaduni wa China.

    Naibu mkuu wa kitivo cha lugha ya kichina cha Chuo Kikuu cha Jinan Bw. Shao Yi anasema, nguvu ya China imeongezeka hatua kwa hatua, mawasiliano kati ya China na nchi za Asia Kusini Mashariki yameimarika siku hadi siku, na mafunzo ya lugha ya kichina kwa Wachina wanaoishi nchi za nje imetiliwa mkazo tena. Kitivo hiki kimeanzisha matawi karibu 30 nchini Indonesia, Philippines, Thailand na Singapore. Wanafunzi zaidi ya 1,700 wamehitimu, na wanafunzi 1,500 wanapata mafunzo katika matawi hayo. Licha ya hayo, kitivo hicho pia kinatekeleza miradi ya mafunzo ya kichina nchini Cambodia na Brunei, kuzisaidia nchi za Asia Kusini Mashariki kutunga vitabu vya masomo ya kichina, na kupeleka walimu wa lugha ya Kichina kufanya kazi katika nchi hizo.

    Njia ya hariri baharini si kama tu ni njia ya usafiri baharini, bali pia inaonesha moyo wa upendo kwa China kwa Wachina wanaoishi nchi za nje, na kuonesha ufuatiliaji wa nchi mbalimbali kuhusu China.

    Mjumbe wa shirika la wanawake wanaojitegemea kiuchumi la Myammar Bibi Zhang Yinmei aliyewahi kujifunza lugha ya kichina ameshiriki kwenye semina ya maofisa vijana wa Umoja wa Nchi za Asia Kusini Mashariki ASEAN hapa China. Si kama tu ana hamu ya kujua utamaduni wa China, bali pia anafuatilia mchakato wa mageuzi na maendeleo ya kisasa ya China.

    Katibu wa kamati ya chama cha kikomunisiti cha China katika chuo cha kimataifa cha mawasiliano ya vijana cha mkoa wa Guangxi Bw. Wang Zhili amesema, baadhi ya maofisa vijana wa nchi za Asia Kusini Mashariki wana hamu ya kujifunza uzoefu wa China katika kujenga maeneo maalumu ya kiuchumi. Bw. Wang ameongeza kuwa, nchi za ASEAN zikitaka kutimiza maendeleo ya kudumu ya ushirikiano wa kiuchumi kati yao, zinahitaji mawasiliano ya kiutamaduni.

    Katibu wa kamati ya chama cha Kikomunisti cha China mjini Quanzhou Bw. Huang Shaoping anaona kuwa, mikakati ya kujenga ukanda wa kiuchumi wa njia ya hariri katika nchi kavu na njia ya hariri baharini ni fursa nzuri kwa mji wa Quanzhou kuharakisha maendeleo yake. Mji huo umeharakisha kufuata njia mpya ya maendeleo kwa kujenga eneo la majaribio la mageuzi ya huduma za fedha na uchumi halisi, na kujenga kituo cha kiutamaduni cha Asia ya Mashariki.

    Wakati mikakati ya kujenga njia ya hariri baharini inapotekelezwa, baadhi ya makampuni ya biashara na nje pia yamerekebisha mikakati yao ya masoko, na kufuatilia zaidi masoko mapya yakiwemo yale ya nchi za Asia kusini Mashariki. Nchi hizo zina nguvu kazi nafuu na njia nyingi za usafiri, hivyo zinatiliwa maanani na wafanyabiashara wanapoanzisha shughuli zao kando ya njia ya hariri ya baharini.

    Naibu meneja mkuu wa kampuni ya hariri ya mkoa wa Guangdong Bw. Zhu Mingyi anasema, mwaka jana asilimia 40 ya bidhaa za kampuni yake ziliuzwa katika masoko mapya, na ongezeko la mauzo ya bidhaa katika masoko hayo ni kubwa kuliko ongezeko la wastani.

    Mikakati ya kujenga ukanda wa kiuchumi wa njia ya hariri baharini itahimiza maendeleo ya shughuli husika zikiwemo utengenezaji wa vifaa vinavyotumiwa baharini na usambazaji wa bidhaa, na hakika itasukuma mbele utandawazi wa kikanda na maendeleo ya kanda hiyo.

    Mwanzoni mwa mwaka 2007, mkoa wa Guangxi uliidhinisha kuanzisha kampuni ya mambo ya bandari ya kimataifa ya ghuba ya Beibu, kuunganisha bandari ya Beihai, Fangcheng na Qinzhou, na kuzifanya shughuli za bandari ziamuliwe na soko badala ya serikali. Mwaka 2013 wakati usafiri baharini ulipodidimia duniani, upakiaji na upakuaji wa mizigo katika bandari ya Beihai uliongezeka kwa asilimia 18.5, na kufikia tani milioni 2.1358.

    Hivi sasa miji na mikoa mbalimbali ya pwani ya China inajitahidi kushiriki katika mikakati ya kujenga njia ya hariri baharini, na biashara kupitia baharini inastawi zaidi siku hadi siku.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako