Winga wa Argentina Angel Di Maria ameenguliwa katika kikosi chake kitakachocheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi leo hii, lakini mchezaji mwingine Sergio Aguero yupo fiti kwa ajili ya mchezo huo baada ya kupona maumivu ya misuli. Aguero alionekana mwenye afya njema katika mazoezi ya timu hiyo, lakini Di Maria hakuonekana kutokana na kuendelea kupata matibabu baada ya kuumia katika mechi waliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 wa robo fainali dhidi ya Ubelgiji. Hii ni nusu fainali yao ya kwanza tangu 1990, na miamba hiyo ya Amerika Kusini itacheza na Uholanzi leo mjini Sao Paulo. Daktari wa timu hiyo amesema Di Maria ana tatizo moja mguuni. hivyo hataweza kucheza katika mechi dhidi ya Argentina. Mshambiliaji wa Manchester City Aguero alikosa michezo miwili kutokana na maumivu ya misuli, lakini kutokana na mazoezi aliyofanya juzi asubuhi mjini Belo Horizonte, mshambuliaji huyo anaweza hata kuanzia benchi katika mchezo wa leo. Kutokuwepo kwa Di Maria, winga mbunifu wa miamba hiyo ya Amerika Kusini ukiachilia mbali nahodha Lionel Messi, kunaweza kuwa tatizo, lakini kurudi katika ubora kwa mshambuliaji Gonzalo Higuain kunaweza kusaidia. Bao la Higuain dhidi ya Ubelgiji lilisaidia kuivusha Argentina katika hatua ya nusu fainali, ambapo sasa inakutana na kibarua kigumu cha kuing'oa Uholanzi katika hatua hiyo. Maelfu ya mashabiki kutoka Argentina tayari wamevuka mpaka nchini Brazil kwa ajili ya kwenda kuishangilia timu hiyo kutinga hatua ya fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |